Mathayo 20

Mathayo 20

Wafanyakazi katika shamba la mizabibu

1“Ufalme wa mbinguni unafanana na mtu mwenye shamba la mizabibu, ambaye alitoka asubuhi na mapema kuwaajiri wafanyakazi katika shamba lake.

2Akapatana nao kuwalipa fedha denari moja kwa siku, kisha akawapeleka katika shamba lake la mizabibu.[#20:2 Kiasi cha fedha alicholipwa kibarua kwa siku.]

3Akatoka mnamo saa tatu asubuhi, akaona watu wengine wamesimama sokoni, hawana kazi.

4Akawaambia, ‘Nendeni nanyi mkafanye kazi katika shamba la mizabibu, nami nitawapeni haki yenu.’

5Basi, wakaenda. Huyo mwenye shamba akatoka tena mnamo saa sita na saa tisa, akafanya vivyo hivyo.

6Hata mnamo saa kumi na moja jioni, akatoka tena; akakuta watu wengine wamesimama pale sokoni. Basi, akawauliza, ‘Mbona mmesimama hapa mchana kutwa bila kazi?’

7Wakamjibu: ‘Kwa sababu hakuna mtu aliyetuajiri.’ Naye akawaambia, ‘Nendeni nanyi mkafanye kazi katika shamba la mizabibu.’

8“Kulipokuchwa, huyo mwenye shamba alimwambia mtunza hazina wake, ‘Waite wafanyakazi ukawalipe mshahara wao, ukianzia na wale walioajiriwa mwisho, na kumalizia na wale wa kwanza.’

9Basi, wakaja wale walioajiriwa mnamo saa kumi na moja, wakapokea kila mmoja fedha dinari moja.

10Wale wa kwanza walipofika, walikuwa wanadhani watapewa zaidi; lakini hata wao wakapewa kila mmoja dinari moja.

11Wakazipokea fedha zao, wakaanza kumnung'unikia yule bwana.

12Wakasema, ‘Watu hawa walioajiriwa mwisho walifanya kazi kwa muda wa saa moja tu, mbona umetutendea sawa na wao hali sisi tumevumilia kazi ngumu kutwa na jua kali?’

13“Hapo yule bwana akamjibu mmoja wao, ‘Rafiki, sikukupunja kitu! Je, hukupatana nami mshahara wa dinari moja?

14Chukua haki yako, uende zako. Napenda kumpa huyu wa mwisho sawa na wewe.

15Je, sina haki ya kufanya na mali yangu nipendavyo? Je, unaona kijicho kwa kuwa mimi ni mwema?’”[#20:15 Neno kwa neno: “una jicho baya” taz Mat 6:22-23.]

16Yesu akamaliza kwa kusema, “Hivyo, walio wa mwisho watakuwa wa kwanza na wa kwanza watakuwa wa mwisho.”

Yesu anasema mara ya tatu kuhusu kifo na ufufuo wake

(Marko 10:32-34; Luka 18:31-34)

17Yesu alipokuwa anakwenda juu Yerusalemu, aliwachukua wale wanafunzi kumi na wawili faraghani, na njiani akawaambia,

18“Sikilizeni! Tunakwenda Yerusalemu, na huko Mwana wa Mtu atakabidhiwa kwa makuhani wakuu na waalimu wa sheria, nao watamhukumu auawe.

19Watamkabidhi kwa watu wa mataifa mengine ili adhihakiwe, apigwe viboko na kusulubiwa; lakini siku ya tatu atafufuliwa.”[#20:19 Hapa yahusu watawala wa Kiroma.]

Ombi la mama wa Yakobo na Yohane

(Marko 10:35-45)

20Hapo mama yao wana wa Zebedayo alimjia Yesu pamoja na wanawe, akapiga magoti mbele yake na kumwomba kitu.[#20:20 Yaani, Yakobo na Yohane (rejea Mat 4:21).]

21Yesu akamwuliza, “Unataka nini?” Huyo mama akamwambia, “Ahidi kwamba katika ufalme wako, hawa wanangu wawili watakaa mmoja upande wako wa kulia na mwingine upande wako wa kushoto.”[#20:21 Katika Marko 10:35 inatajwa kuwa walioomba moja kwa moja ni Yakobo na Yohane, wana wa Zebedayo (taz 1:19,29; 3:17; 5:37; 9:2; 13:3; 14:33).; #20:21 Wanafunzi walidhani kwamba Yesu angeanzisha utawala wa kidunia ambao ungekuwa na nyadhifa na nafasi mbalimbali za heshima.]

22Yesu akajibu, “Hamjui mnaomba nini. Je, mnaweza kunywa kikombe nitakachokunywa mimi?” Wakamjibu, “Tunaweza.”[#20:22 Msemo “kunywa kikombe” una maana ya kushiriki mateso au majaribu magumu (taz maelezo ya 26:39).]

23Yesu akawaambia, “Kweli mtakunywa kikombe changu, lakini kuketi kulia au kushoto kwangu si kazi yangu kupanga; jambo hilo watapewa wale waliowekewa tayari na Baba yangu.”[#20:23 Yakobo aliuawa na Herode Agripa mwaka wa 42 B.K. (Mate 12:1-3).]

24Wale wanafunzi wengine kumi waliposikia hayo, wakawakasirikia hao ndugu wawili.

25Hivyo Yesu akawaita, akawaambia, “Mnajua kwamba watawala wa mataifa hutawala watu wao kwa mabavu, na wakuu hao huwamiliki watu wao.

26Lakini kwenu isiwe hivyo, ila anayetaka kuwa mkuu kati yenu sharti awe mtumishi wa wote;

27na anayetaka kuwa wa kwanza kati yenu sharti awe mtumishi wenu.

28Jinsi hiyohiyo, Mwana wa Mtu hakuja kutumikiwa, bali kutumikia na kutoa maisha yake kuwa fidia ya watu wengi.”[#20:28 Luka 22:27; Yoh 13:12-15; Fil 2:5-7.; #20:28 Yawezekana kwamba hapa mwandishi anagusia Isa 52:13—53:12 mahali ambapo yahusu mateso ya Mtumishi wa Bwana. Taz Marko 10:45 maelezo. Rejea pia Yoh 10:11; Efe 1:7; Kol 1:13-14; 1Tim 2:5-6; Tito 2:14; Ebr 2:9; 1Pet 1:18-19.]

Yesu anawaponya vipofu wawili

(Marko 10:46-52; Luka 18:35-43)

29Yesu alipokuwa anaondoka mjini Yeriko, umati wa watu ulimfuata.

30Basi, kulikuwa na vipofu wawili wameketi kando ya njia, na waliposikia kwamba Yesu alikuwa anapitia hapo, walipaza sauti: “Bwana, Mwana wa Daudi, utuhurumie!”[#20:30 Jina la sifa ambalo linatumiwa pia na wale vipofu wawili ambao Yesu alikuwa amewaponya (9:27). Katika Marko (10:46) na Luka (18:35) tuna kipofu mmoja tu.]

31Ule umati wa watu ukawakemea na kuwaambia wanyamaze. Lakini wao wakazidi kupaza sauti: “Bwana, Mwana wa Daudi, utuhurumie!”

32Yesu akasimama, akawaita na kuwauliza, “Mnataka niwafanyie nini?”

33Wakamjibu, “Bwana, tunaomba macho yetu yafumbuliwe.”

34Basi, Yesu akawaonea huruma, akawagusa macho yao, na papo hapo wakaweza kuona, wakamfuata.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania