The chat will start when you send the first message.
1Yesu alipomaliza kusema hayo yote, aliwaambia wanafunzi wake,
2“Mnajua kwamba baada ya siku mbili tutakuwa na sikukuu ya Pasaka, na Mwana wa Mtu atatolewa ili asulubiwe.”[#26:2 Taz Mat 26:17 maelezo.; #26:2 Kutoka mahala pengine tunajua kwamba Mungu ndiye anayemtoa Mwanawe auawe (Rom 4:25; 1Kor 11:23); Yesu naye anasemwa kwamba yeye mwenyewe alijitoa auawe (Gal 2:20; Efe 5:2).]
3Wakati huo makuhani wakuu na wazee wa watu walikutana pamoja katika ukumbi wa Kayafa, kuhani mkuu.
4Wakashauriana jinsi ya kumtia Yesu nguvuni kwa hila wamuue.
5Lakini wakaamua jambo hilo lisifanyike wakati wa sikukuu, kusije kukatokea ghasia kati ya watu.[#26:5 Taz Marko 14:1-2.]
6Yesu alipokuwa Bethania, nyumbani kwa Simoni, aitwaye Mkoma,[#26:6-13 Simulizi hili linafanana sana na lile la Luka 7:37-38.; #26:6 Labda huyo alikuwa na ugonjwa wa ukoma wakati mmoja kisha akapona, lakini jina “Mkoma” likamkaa.]
7mama mmoja aliyekuwa na chupa ya alabasta yenye marashi ya thamani kubwa, alimjia pale mezani alipokuwa amekaa kula chakula, akammiminia hayo marashi kichwani.[#26:7 Tazama Yoh12:3 ambapo anaitwa Maria, dada yake Lazaro na Martha. Kitendo chake kilikuwa cha heshima kwa Yesu; naye Yesu anakifafanua kuwa ni kitendo cha matayarisho kwa mazishi yake (26:12). Kisa tunachopewa katika Luka 7:36-50 ni tofauti na hiki.]
8Wanafunzi wake walipoona hayo wakakasirika, wakasema, “Ya nini hasara hii?
9Marashi haya yangaliweza kuuzwa kwa bei kubwa, maskini wakapewa hizo fedha.”
10Yesu alitambua mawazo yao, akawaambia, “Mbona mnamsumbua huyu mama? Yeye amenitendea jambo jema.
11Maskini mnao daima pamoja nanyi, lakini mimi sitakuwapo pamoja nanyi daima.
12Huyu mama amenimiminia marashi ili kunitayarisha kwa maziko.
13Nawaambieni kweli, popote ulimwenguni ambapo hii Habari Njema itahubiriwa, kitendo hiki alichofanya mama huyu kitatajwa kwa kumkumbuka yeye.”
14Kisha, Yuda Iskarioti, mmoja wa wale kumi na wawili, akaenda kwa makuhani wakuu,
15akawaambia, “Mtanipa kitu gani kama nikimkabidhi Yesu kwenu?” Wakamhesabia vipande thelathini vya fedha;[#26:15 Katika Kut 21:32 tunasoma kwamba hiyo ndiyo bei ya mtumwa. Hapa haisemwi ni fedha za namna gani, lakini 27:9-10 inakariri Zek 11:12-13, ambapo nabii anasema juu ya vipande thelathini vya fedha ambazo ziliitwa “shekeli” sarafu yenye thamani ya dinari nne (20:2).]
16na tangu wakati huo Yuda akawa anatafuta nafasi ya kumsaliti.
17Siku ya kwanza kabla ya sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu, wanafunzi walimwendea Yesu wakamwuliza, “Unataka tukuandalie wapi chakula cha Pasaka?”[#26:17 Taz Marko 14:12. Sikuuu ya Kiyahudi ambayo iliadhimishwa kwa siku saba kuanzia sikukukuu ya Pasaka. Kuhusu wakati wenyewe wa matukio ya wakati wa mateso ya Bwana rejea tamko la Yoh 18:28 kwamba kifo cha Yesu kilitokea wakati kondoo wa tambiko ya Pasaka walikuwa wanachinjwa.; #26:17 Sikukuu maalumu kabisa katika kalenda ya Wayahudi; ilihusikana na kukumbuka wakati Mungu alipowaokoa Waisraeli kutoka Misri. Neno “pasaka” ni andiko la Kiswahili la neno la Kiebrania “pesakh” linavyotumiwa katika Kut 12:13: “Nitawapitia ninyi, na hamtapatwa na dhara lolote wakati nitakapoichapa nchi ya Misri”. Tangu mwanzo wa Kanisa Wakristo waliona “Pasaka” yao kuwa kumbukumbu la kuokolewa kwao kwa kifo na ufufuo wake Yesu.]
18Yeye akawajibu, “Nendeni mjini kwa mwanamume fulani, mkamwambie: ‘Mwalimu anasema, wakati wangu umefika; kwako nitakula Pasaka pamoja na wanafunzi wangu.’”[#26:18 Maagizo ya Yesu yalivyo inaonekana alikwisha fanya mpango kwa ajili ya karamu ya Pasaka.; #26:18 Hapa panagusiwa mipango ya Mungu inayotekelezwa kwa wakati maalumu; huo ndio wakati ambao Yohane anautaja kama “saa yake” (Yoh 7:30; 13:1).]
19Wanafunzi wakafanya kama Yesu alivyowaagiza, wakaandaa Pasaka.
20Kulipokuwa jioni, Yesu akakaa mezani pamoja na wanafunzi wake kumi na wawili.
21Walipokuwa wakila, Yesu akasema, “Nawaambieni kweli, mmoja wenu atanisaliti.”
22Wanafunzi wakahuzunika sana, wakaanza kuuliza mmojammoja, “Bwana! Je, ni mimi?”
23Yesu akajibu, “Anayechovya mkate pamoja nami katika bakuli ndiye atakayenisaliti.[#26:23 Lugha inayotumika hapa inakumbusha Zab 41:9. Hicho ni kitendo kinachomaanisha pia urafiki wa karibu. Hivyo, msaliti alikuwa tayari kabisa kuvunja uhusiano huo wa karibu ambao uliashiriwa kwa kitendo hicho cha kula pamoja.]
24Naam, Mwana wa Mtu anakwenda zake kama Maandiko Matakatifu yasemavyo, lakini ole wake mtu yule atakayemsaliti Mwana wa Mtu! Ingalikuwa afadhali kwa mtu huyo kama hangalizaliwa.”
25Yuda, ambaye ndiye aliyetaka kumsaliti, akamwuliza, “Mwalimu! Je, ni mimi?” Yesu akamjibu, “Wewe umesema.”
26Walipokuwa wanakula, Yesu akatwaa mkate, akamshukuru Mungu, akaumega, akawapa wanafunzi wake akisema, “Twaeni mle; huu ni mwili wangu.”[#26:26 Kwa kumwaga damu yake msalabani Yesu anakamilisha maneno ya Yer 31:31-34, agano ambalo sasa linawahusu binadamu wote (Isa 53:12).]
27Kisha akatwaa kikombe cha divai, akashukuru, akawapa akisema, “Kunyweni nyote;
28maana hii ni damu yangu inayothibitisha agano, damu inayomwagwa kwa ajili ya watu wengi ili kuwaondolea dhambi.[#26:28 Baadhi ya hati za kale zina: agano “jipya”. Rejea Kut 24:6-8; Yer 31:34; Zek 9:11; 13:20; taz Luka 22:20 maelezo.]
29Nawaambieni, sitakunywa tena divai ya zabibu mpaka siku ile nitakapoinywa mpya pamoja nanyi katika ufalme wa Baba yangu.”[#26:29 Taz Mat 8:12 maelezo.]
30Baada ya kuimba wimbo, wakaondoka, wakaenda katika mlima wa Mizeituni.[#26:30 Labda ni Zaburi za 113—118 ambazo ziliimbwa baada ya chakula cha Pasaka.]
31Kisha Yesu akawaambia, “Usiku huu wa leo, nyinyi nyote mtakuwa na mashaka nami, maana Maandiko Matakatifu yasema:[#26:31 Au, “Mtapata kikwazo kwa sababu yangu”.]
‘Nitampiga mchungaji,
na kondoo wa kundi watatawanyika.’
32Lakini baada ya kufufuka kwangu, nitawatangulieni Galilaya.”[#26:32 Mat 28:7,10,16; Marko 16:7; rejea Yoh 21:1.]
33Petro akamwambia Yesu, “Hata kama wote watakuwa na mashaka nawe na kukuacha, mimi sitakuacha kamwe.”
34Yesu akamwambia, “Kweli nakuambia, usiku huu kabla jogoo hajawika, utanikana mara tatu.”
35Petro akamwambia, “Hata kama ni lazima nife pamoja nawe, sitakukana kamwe.” Wale wanafunzi wengine wote wakasema vivyo hivyo.
36Kisha Yesu akaenda pamoja nao bustanini Gethsemane, akawaambia wanafunzi wake, “Kaeni hapa nami niende pale mbele kusali.”[#26:36 Mahali penyewe hapajulikani, lakini wengi wanafikiri ni upande wa magharibi mwa mteremko wa Mlima wa Mizeituni, mkabala na Yerusalemu. Katika Yoh 18:1 panaitwa bustani.]
37Akawachukua Petro na wana wawili wa Zebedayo, akaanza kuwa na huzuni na mahangaiko.[#26:37 Yaani, Yakobo na Yohane (4:21).]
38Hapo akawaambia, “Nina huzuni kubwa moyoni hata karibu kufa. Kaeni hapa mkeshe pamoja nami.”
39Basi, akaenda mbele kidogo, akaanguka kifudifudi, akasali: “Baba yangu, kama inawezekana, kikombe hiki kinipite; lakini isiwe nitakavyo mimi, ila utakavyo wewe.”[#26:39 Ishara au kielelezo cha huzuni kuu, majaribio na mateso makali (taz Isa 51:17,22; Eze 23:31-34).]
40Akawaendea wale wanafunzi, akawakuta wamelala. Akamwambia Petro, “Ndio kusema hamkuweza kukesha pamoja nami hata saa moja?
41Kesheni na kusali ili msije mkaingia katika majaribu. Roho inataka lakini mwili ni dhaifu.”[#26:41 Kuhusu majaribu Taz Luka 22:40 maelezo.]
42Akaenda tena mara ya pili akasali: “Baba yangu, kama haiwezekani kikombe hiki kipite bila mimi kukinywa, basi, utakalo lifanyike.”
43Akawaendea tena, akawakuta wamelala, maana macho yao yalikuwa yamebanwa na usingizi.
44Basi, akawaacha, akaenda tena kusali mara ya tatu kwa maneno yaleyale.
45Kisha akawaendea wale wanafunzi, akawaambia, “Je, mngali mmelala na kupumzika? Tazameni! Saa yenyewe imefika, na Mwana wa Mtu atatolewa kwa watu wenye dhambi.[#26:45 Si dhahiri kujua matumizi ya swali hili; hakika si lenye kutaka majibu ila yamkini ni Mtindo wa kukejeli au msemo wa mshangao.]
46Amkeni; twendeni zetu. Tazameni! Anakuja yule atakayenisaliti.”
47Basi, Yesu alipokuwa bado anasema nao, mara akaja Yuda, mmoja wa wale kumi na wawili. Pamoja naye walikuja watu wengi wenye mapanga na marungu ambao walitumwa na makuhani wakuu na wazee wa watu.
48Huyo aliyetaka kumsaliti Yesu, alikuwa amekwisha kuwapa ishara akisema: “Yule nitakayembusu ndiye; mkamateni.”[#26:48-49 Kumbusu mtu usoni ilikuwa wakati huo ishara ya salamu na heshima ambayo mwanafunzi au mfuasi alimpa aliyemfundisha na kumtambua kama mwalimu wake.]
49Basi, Yuda akamkaribia Yesu, akamwambia, “Shikamoo, Mwalimu!” Kisha akambusu.
50Yesu akamwambia, “Rafiki, fanya ulichokuja kufanya.” Hapo wale watu wakaja, wakamkamata Yesu, wakamtia nguvuni.
51Mmoja wa wale waliokuwa pamoja na Yesu akanyosha mkono, akauchomoa upanga wake, akampiga mtumishi wa kuhani mkuu, akamkata sikio.
52Hapo Yesu akamwambia, “Rudisha upanga wako alani, maana yeyote anayeutumia upanga, atakufa kwa upanga.
53Je, hamjui kwamba ningeweza kumwomba Baba yangu naye mara angeniletea zaidi ya vikosi kumi na viwili vya malaika?[#26:53 Katika jeshi la Kiroma kikosi kimoja kilikuwa na askari 6,000.]
54Lakini yatatimiaje Maandiko Matakatifu yasemayo kwamba ndivyo inavyopaswa kuwa?”
55Wakati huohuo Yesu akauambia huo umati wa watu waliokuja kumtia nguvuni, “Je, mmekuja kunikamata kwa mapanga na marungu kana kwamba mimi ni mnyang'anyi? Kila siku nilikuwa hekaluni nikifundisha, na hamkunikamata![#26:55 Luka 19:47; 21:37; Yoh 18:19-21.]
56Lakini haya yote yametendeka ili maandiko ya manabii yatimie.” Kisha wanafunzi wote wakamwacha, wakakimbia.
57Basi, hao watu waliomkamata Yesu walimpeleka nyumbani kwa Kayafa, kuhani mkuu, walikokusanyika waalimu wa sheria na wazee.[#26:57 Kayafa alikuwa kuhani mkuu au kiongozi wa makuhani au makasisi wa Kiyahudi miaka ya 18-36 B.K. Mathayo na Marko wanataja kikao cha kwanza cha Halmashauri kuu ya Wayahudi (Mat 26:57-75 Marko 14:53-72) kikao ambacho kilifanyika usiku ili kuweka vizuri mashtaka dhidi ya Yesu. Kikao kingine kilichofanyika asubuhi (Mat 27:1-2; Marko 15:1) kilikuwa kwa madhumuni ya kuidhinisha mapatano yaliyofanyika usiku katika kikao cha kwanza.]
58Petro alimfuata kwa mbali mpaka uani kwa kuhani mkuu, akaingia ndani pamoja na walinzi ili apate kuona mambo yatakavyokuwa.
59Basi, makuhani wakuu na Baraza lote wakatafuta ushahidi wa uongo dhidi ya Yesu wapate kumuua,
60lakini hawakupata ushahidi wowote, ingawa walikuja mashahidi wengi wa uongo. Mwishowe wakaja mashahidi wawili,[#26:60 Kulingana na sheria za Kiyahudi, ilikuwa lazima mashahidi wawili au watatu waafikiane katika ushuhuda wao (Hes 35:30; Kumb 19:15).]
61wakasema, “Mtu huyu alisema: ‘Ninaweza kuliharibu hekalu la Mungu na kulijenga tena kwa siku tatu.’”
62Kuhani mkuu akasimama, akamwuliza Yesu, “Je, hujibu neno? Watu hawa wanashuhudia nini dhidi yako?”
63Lakini Yesu akakaa kimya. Kuhani mkuu akamwambia, “Nakuapisha kwa Mungu aliye hai, tuambie kama wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu!”
64Yesu akamwambia, “Wewe umesema! Lakini nawaambieni, tangu sasa mtamwona Mwana wa Mtu ameketi upande wa kulia wa yule Bwana Mwenye Nguvu, akija juu ya mawingu ya mbinguni.”[#26:64 Jibu hili ni kama fumbo ambalo laweza kueleweka kwa maana ya: “Ni wewe umesema” au, “Naam, ni kama ulivyosema” (rejea Mat 27:11 maelezo).; #26:64 Swali la Kuhani Mkuu (aya ya 62) lina baadhi ya maneno yaleyale ya Petro ya kumkiri Yesu kuwa Masiha (16:16). Yesu hajibu swali hilo moja kwa moja kama ilivyo katika Marko 14:62 (taz maelezo ya hapo).]
65Hapo, kuhani mkuu akararua mavazi yake, akasema, “Amekufuru! Tuna haja gani tena ya mashahidi? Sasa mmesikia kufuru yake.
66Nyinyi mwaonaje?” Wao wakamjibu, “Anastahili kufa!”
67Kisha wakamtemea mate usoni, wakampiga makofi. Wengine wakiwa wanampiga makofi,
68wakasema, “Tubashirie basi, wewe Kristo; ni nani amekupiga!”
69Petro alikuwa ameketi nje uani. Basi, mtumishi mmoja wa kike akamwendea, akasema, “Wewe ulikuwa pamoja na Yesu wa Galilaya.”
70Petro akakana mbele ya wote akisema, “Sijui hata unasema nini.”
71Alipokuwa akitoka mlangoni, mtumishi mwingine wa kike akamwona, akawaambia wale waliokuwa pale, “Mtu huyu alikuwa pamoja na Yesu wa Nazareti.”
72Petro akakana tena kwa kiapo: “Simjui mtu huyo.”
73Baadaye kidogo, watu waliokuwa pale wakamwendea Petro, wakamwambia, “Hakika, wewe pia ni mmoja wao, maana msemo wako unakutambulisha.”
74Hapo Petro akaanza kujilaani na kuapa akisema, “Simjui mtu huyo!” Mara jogoo akawika.
75Petro akakumbuka maneno aliyoambiwa na Yesu: “Kabla jogoo hajawika, utanikana mara tatu.” Basi, akatoka nje, akalia sana.[#26:75 Kulingana na desturi ya Waroma jogoo aliwika mara ya kwanza usiku wakati ambao waliuchukua kuwa mwisho wa mkesha wa tatu wa usiku; lakini hapa kuwika kwa huyo jogoo ilikuwa ni ishara ya kukumbukwa na Petro (aya 74-75).]