The chat will start when you send the first message.
1Baada ya Sabato, karibu na mapambazuko ya siku ile ya Jumapili, Maria Magdalene na yule Maria mwingine walikwenda kutazama lile kaburi.
2Ghafla kukatokea tetemeko kubwa la nchi; malaika wa Bwana alishuka kutoka mbinguni, akalivingirisha lile jiwe, akalikalia.
3Alionekana kama umeme na mavazi yake yalikuwa meupe kama theluji.
4Walinzi wa lile kaburi wakatetemeka kwa hofu kubwa, hata wakawa kama wamekufa.
5Lakini yule malaika akawaambia wale wanawake, “Nyinyi msiogope! Najua kwamba mnamtafuta Yesu aliyesulubiwa.
6Hayupo hapa maana amefufuka kama alivyosema. Njoni mkaone mahali alipokuwa amelala.[#28:6 Mat 16:21; 17:23; 20:19 (rejea Luka 24:6-7)]
7Basi, nendeni upesi mkawaambie wanafunzi wake kwamba amefufuka kutoka kwa wafu, na sasa anawatangulieni kule Galilaya; huko mtamwona. Haya, mimi nimekwisha waambieni.”
8Wakiwa wenye hofu na furaha kubwa, hao wanawake walitoka upesi kaburini, wakakimbia kwenda kuwaambia wanafunzi wake.
9Mara, Yesu akakutana nao, akasema: “Salamu.” Hao wanawake wakamwendea, wakapiga magoti mbele yake, wakashika miguu yake.
10Kisha Yesu akawaambia, “Msiogope! Nendeni mkawaambie ndugu zangu waende Galilaya, na huko wataniona.”[#28:10 Bwana Yesu aliyefufuka anawaita wafuasi wake “ndugu zake” (rejea Mat 12:48-50; Yoh 20:17).]
11Wale wanawake walipokuwa wanakwenda zao, baadhi ya walinzi wa lile kaburi walikwenda mjini kutoa taarifa kwa makuhani wakuu juu ya mambo yote yaliyotukia.
12Basi, wakakutana pamoja na wazee, na baada ya kushauriana, wakawapa wale askari kiasi kikubwa cha fedha
13wakisema, “Nyinyi mtasema hivi: ‘Wanafunzi wake walikuja usiku, wakamwiba sisi tukiwa tumelala.’
14Na kama mkuu wa mkoa akijua jambo hili, sisi tutasema naye na kuhakikisha kuwa nyinyi hamtapata matatizo.”
15Wale walinzi wakazichukua zile fedha, wakafanya kama walivyofundishwa. Habari hiyo imeenea kati ya Wayahudi mpaka leo.[#28:15 Yaani wakati Injili hii ilipoandikwa.]
16Wale wanafunzi kumi na mmoja walikwenda Galilaya kwenye ule mlima aliowaagizia Yesu.
17Walipomwona wakamwabudu, ingawa wengine walikuwa na mashaka.
18Yesu akaja karibu, akawaambia, “Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani.
19Nendeni basi, mkawafanye watu wa mataifa yote wawe wanafunzi wangu, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na la Mwana, na la Roho Mtakatifu.[#28:19 Katika aya hii majina ya Baba, Mwana na Roho Mtakatifu yanaunganishwa katika msemo mmoja ambao ulianza kutumiwa katika Kanisa kama maneno rasmi ya Ubatizo. Taz hasa 2Kor 13:13 maelezo. Inamaanisha kuweko uhusiano wa pekee (taz 1Kor 1:13; 10:2) na hivyo kuweka uhusiano wa pekee kati ya huyo mbatizwa na Baba, Mwana na Roho Mtakatifu.]
20Wafundisheni kushika maagizo yote niliyowapeni. Nami nipo pamoja nanyi siku zote; naam, mpaka mwisho wa nyakati.”