Marko 1

Marko 1

Mahubiri ya Yohane Mbatizaji

(Mat 3:1-12; Luka 3:1-18; Yoh 1:19-28)

1Habari Njema ya Yesu Kristo, Mwana wa Mungu.[#1:1 Tafsiri nyingine ni “Injili” (Kigiriki: “eungelion”). Kwa maelezo zaidi taz utangulizi wa Injili hii.; #1:1 Au, “Masiha”.; #1:1 Jina la sifa muhimu sana katika Injili ya Marko (1:11; 3:11; 5:7; 9:7; 12:6; 14:61-62; 15:39). Marko, hatua kwa hatua, anaonesha hali yake Yesu ya kimasiha na kimungu.]

2Ilianza kama ilivyoandikwa katika kitabu cha nabii Isaya:

“Mungu alisema, ‘Namtuma mjumbe wangu akutangulie,

ambaye atakutayarishia njia yako.’

3Sauti ya mtu anaita jangwani:

‘Mtayarishieni Bwana njia yake,

nyosheni barabara zake.’”

4Yohane Mbatizaji alitokea jangwani, akahubiri kwamba watu watubu na kubatizwa ili Mungu awasamehe dhambi zao.[#1:4 Neno “kutubu” linatafsiri neno la Kigiriki “metanoein” ambalo maana yake, neno kwa neno, ni “kubadili mwenendo” (yaani mbaya) na, kibiblia, lajumuisha aghalabu kumrudia Mungu (taz Mat 3:2 maelezo). Ubatizo huo wa Yohane haukuwa tu kitendo cha utakaso wa kidini kama vile kutawadha bali ulikuwa ishara ya uongofu wa kweli. Rejea Mate 2:38; 13:24.]

5Watu kutoka sehemu zote za Yudea na wenyeji wote wa Yerusalemu walimwendea, wakaziungama dhambi zao, naye akawabatiza katika mto Yordani.

6Yohane alikuwa amevaa vazi lililofumwa kwa manyoya ya ngamia, na ukanda wa ngozi kiunoni mwake. Chakula chake kilikuwa nzige na asali ya mwituni.[#1:6 Yohane alijivalia kama Elia (2Fal 1:8; rejea pia Zek 13:4). Tunaambiwa pia kwamba chakula chake kilikuwa nzige na asali ya mwituni. “Nzige” huko Mashariki ya Kati na hata sehemu nyingi za bara la Afrika walitumiwa kama chakula.]

7Naye alihubiri akisema, “Baada yangu anakuja mwenye nguvu zaidi kuliko mimi, ambaye mimi sistahili hata kuinama na kufungua kamba za viatu vyake.[#1:7 Yoh 1:15,27,30. Kumfungulia mtu kamba za viatu vyake ilikuwa huduma iliyomaanisha hali ya chini ya mwenye kufanya hivyo, nayo aghalabu ilifanywa na watumwa.]

8Mimi ninawabatiza kwa maji, lakini yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu.”[#1:8 Taz Yoh 1:33; Mate 1:5; 2:1-4. Jambo la Roho Mtakatifu kuhusika hapa si geni katika Maandiko Matakatifu. Roho wa Mungu alitazamiwa nyakati za mwisho (taz 1:10,12; taz pia Isa 11:1-2; Yoe 2:28-32).]

Kubatizwa na kujaribiwa kwa Yesu

(Mat 3:13—4:11; Luka 3:21-22; 4:1-13)

9Siku hizo, Yesu alifika kutoka Nazareti, mji wa Galilaya, akabatizwa na Yohane katika mto Yordani.[#1:9 Eneo la kaskazini mwa Palestina, kaskazini-magharibi mwa ziwa Galilaya.]

10Mara tu alipotoka majini, aliona mbingu zimefunguliwa, na Roho akishuka juu yake kama njiwa.[#1:10 Maneno haya, mara nyingi katika Biblia, yanatumika pale ambapo Mungu mwenyewe anajidhihirisha au kujitambulisha kwa watu. Taz kwa mfano Isa 64:1; Eze 1:1; Yoh 1:51; Mate 7:56.]

11Sauti ikasikika kutoka mbinguni: “Wewe ni Mwanangu mpendwa, nimependezwa nawe.”[#1:11 Tafsiri nyingine yamkini: “Mwanangu wa pekee”. Maneno haya kutoka mbinguni yanakumbusha Zab 2:7,12; Isa 42:1. Taz pia Marko 9:7; Mat 12:18; 2Pet 1:17.]

12Mara akaongozwa na Roho kwenda jangwani,

13akakaa huko siku arubaini akijaribiwa na Shetani. Alikuwa huko pamoja na wanyama wa porini, nao malaika wakawa wanamhudumia.[#1:13 Taz Mat 4:2 maelezo.; #1:13 Jina ambalo lamaanisha “mshtaki” au “mpinzani” na linatumiwa kumtaja Ibilisi.; #1:13 Hapa panaonesha aghalabu uangalizi wa Mungu kwa Yesu.; #1:13 Jambo la Yesu kuwa na wanyama wa porini halieleweki kwa urahisi lakini huenda lataka kukumbusha hapa kwamba “sura mpya” inafunguliwa juu ya kuumbwa upya kwa hali ile ya awali, wakati ulimwengu ulipoumbwa Mwa 1:28; 2:19-20; Yobu 5:22; Isa 11:6-9; 65:17-25; Hos 2:18.]

Yesu anawaita wavuvi wanne

(Mat 4:12-22; Luka 4:14-15; 5:1-11)

14Yohane alipokwisha fungwa gerezani, Yesu alikwenda Galilaya, akahubiri Habari Njema ya Mungu, akisema,[#1:14 Yohane Mbatizaji alifungwa gerezani na Herode Antipa (taz Mat 4:12 maelezo; 6:17-18).]

15“Wakati umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia. Tubuni na kuiamini Habari Njema!”[#1:15 Yahusu muda muhimu na maalumu uliowekwa na Mungu.; #1:15 Au, “Utawala wa Mungu”; au, “Utawala wa Mbinguni”. Yahusu kitendo cha Mungu ambacho kwa uwezo wake anawaokoa watu na kusimika mamlaka yake kati yao (taz 4:11; 9:1; 15:43). Ufalme wa Mungu katika Injili ni sawa na Ufalme wa Mbinguni; Mathayo ndiye hasa anayetumia Ufalme wa Mbinguni kwa kuepa kumtaja Mungu mara nyingi.; #1:14-15 Katika aya hizi mbili tunapewa kwa muhtasari na kwa kuzingatia mambo kitovu juu ya huduma ya Yesu. Taz pia 1:21-22,32-34. Jambo kitovu ni: Habari Njema kutoka kwa Mungu ambayo inahusu kuwasili kwa wakati maalumu wa ujio wa ufalme wa Mungu utakaosababisha watu watubu na kuiamini hiyo Habari Njema ya wokovu.]

16Alipokuwa anapita kando ya ziwa Galilaya, aliwaona wavuvi wawili: Simoni na Andrea ndugu yake wakivua samaki kwa wavu.[#1:16—8:30 Katika sehemu ya kwanza ya Injili tunaoneshwa kwa hatua mbalimbali ambazo Yesu anajidhihirisha kwa wanafunzi wake. Ufunuo huo, kwa matendo na maneno yake, unafikia kilele chake pale Petro anapomkiri Yesu kuwa ndiye Kristo (8:29).]

17Yesu akawaambia, “Nifuateni nami nitawafanya nyinyi kuwa wavuvi wa watu.”

18Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata.

19Alipokwenda mbele kidogo, aliwaona Yakobo na Yohane, wana wa Zebedayo. Nao pia walikuwa ndani ya mashua yao wakizitengeneza nyavu zao.

20Yesu akawaita mara, nao wakamwacha baba yao Zebedayo katika mashua pamoja na wafanyakazi, wakamfuata.[#1:16-20 Visa vyote viwili (Simoni na Andrea; Yakobo na Yohane - na baba yao) vina madhumuni ya kutilia mkazo umuhimu wa kumfuata Yesu, kubadili kazi na kuachana na jamaa!]

Mtu mwenye pepo mchafu

(Luka 4:31-37)

21Wakafika mjini Kafarnaumu, na mara ilipofika Sabato, Yesu akaingia katika sunagogi, akaanza kufundisha.[#1:21 Mji kaskazini-magharibi mwa pwani ya ziwa Galilaya.; #1:21 Nyumba ya mikutano na mafunzo ya Wayahudi. Kwa desturi, humo mtu yeyote mwenye uzoefu aliweza kualikwa wakati wa mikutano hiyo, akafafanua na kueleza Maandiko (rejea Luka 4:16-21; Mate 13:14-15).]

22Watu wote waliomsikia walishangazwa na mafundisho yake, maana hakuwa anafundisha kama waalimu wao wa sheria, bali kama mtu mwenye mamlaka.[#1:22 Taz orodha ya maneno. Katika Marko hao waalimu wa sheria ambao walikuwa wafafanuzi rasmi wa maandiko ya Wayahudi wanachukuliwa kuwa kundi moja na wapinzani wa Yesu (k.m. 2:6,16).]

23Mara akatokea mle ndani ya sunagogi mtu mmoja mwenye pepo mchafu,[#1:23 Nyakati hizo za kale watu waliona kwamba mikasa mbalimbali ya magonjwa n.k. ilisababishwa na shetani au pepo wabaya. Yesu alitaka kuwafungulia wanadamu vifungo vya shetani vilivyojitokeza katika maisha yao kwa namna mbalimbali.]

24akapaza sauti, “Una nini nasi, wewe Yesu wa Nazareti? Je, umekuja kutuangamiza? Najua wewe ni nani: wewe ni Mtakatifu wa Mungu!”[#1:24 Matumizi ya wingi hapa yamkini yahusu si tu mmoja, ila jumla yote ya utawala au himaya ya pepo wabaya.; #1:24 Msemo ambao unataja uhusiano wa pekee wa Yesu na Mungu.]

25Yesu akamkemea huyo pepo akisema, “Nyamaza! Mtoke mtu huyu.”

26Basi, huyo pepo mchafu akamtikisatikisa mtu huyo, kisha akalia kwa sauti kubwa, akamtoka.

27Watu wote wakashangaa, wakaulizana, “Ni mambo gani haya? Je, ni mafundisho mapya? Mtu huyu anayo mamlaka ya kuamuru hata pepo wachafu, nao wanamtii!”

28Habari za Yesu zikaenea upesi kila mahali katika eneo la Galilaya.

Yesu anawaponya watu wengi

(Mat 8:14-17; Luka 4:38-41)

29Wakatoka katika sunagogi, wakaenda moja kwa moja hadi nyumbani kwa Simoni na Andrea; Yakobo na Yohane walikwenda pamoja nao.

30Basi, mama mmoja, mkwewe Simoni, alikuwa kitandani ana homa kali. Wakamwarifu Yesu mara alipowasili.

31Yesu akamwendea huyo mama, akamshika mkono, akamwinua. Na ile homa ikamwacha, akaanza kuwatumikia.

32Jioni, jua lilipokwisha tua, wakamletea Yesu wagonjwa wote na watu waliopagawa na pepo.[#1:32 Yaani wakati Sabato ya Wayahudi na miiko yake ilipokwisha (rejea 1:21). Hivyo watu waliweza kubeba wagonjwa wao na kuwapeleka kwa Yesu bila kushtakiwa kwamba wamevunja miiko ya Sabato, kwani kutembea kiasi fulani na kubeba kitu kama vile mgonjwa kulifikiriwa kuwa ni kufanya kazi.; #1:32-34 Aya hizi zinatumika kuipa Injili hii mshikamano wa wasimulizi. Ni muhtasari wa matendo ya Yesu. Rejea pia 1:39; 3:7-12; 4:33-34; 6:53-56.]

33Watu wote wa mji ule wakakusanyika nje ya mlango.

34Naye Yesu akawaponya watu wengi waliokuwa na magonjwa mbalimbali; aliwafukuza pepo wengi, lakini hakuwaruhusu kusema kitu maana walikuwa wanamjua yeye ni nani.[#1:34 Katika Injili ya Marko mara kwa mara Yesu anawakataza watu na hata pepo wasiseme juu yake na uwezo wake (1:44; 3:11-12; 5:43; 7:36; 8:30; 9:9). Lakini, Yesu, akiwa faraghani pamoja na wanafunzi wake aliongea nao wazi wazi kwamba itampasa kuteseka, kuuawa na kufufuka (Marko 8:31; 9:31; 10:32-34). Aliwapa picha ya ujumbe wa kazi yake ulio tofauti kabisa na matazamio ya Wayahudi ambao walifikiria juu ya Masiha mshindi wa kisiasa.]

Yesu anahubiri Galilaya

(Luka 4:42-44)

35Kesho yake, kabla ya mapambazuko, Yesu alitoka, akaenda mahali pa faragha kusali.[#1:35 Mahali ambapo hapakuwa na watu, mazingira ya kawaida ya sala katika Marko (6:46; 14:32,35,39. Taz pia Luka 5:16; 6:12).]

36Simoni na wenzake wakaenda kumtafuta.

37Walipomwona, wakamwambia, “Kila mtu anakutafuta.”

38Yesu akawaambia, “Twendeni katika miji mingine ya jirani nikahubiri huko pia, maana nimekuja kwa sababu hiyo.”

39Basi, akaenda kila mahali huko Galilaya akihubiri katika masunagogi na kufukuza pepo.

Yesu anamponya mtu mwenye ukoma

(Mat 8:1-4; Luka 5:12-16)

40Mtu mmoja mwenye ukoma alimwendea Yesu, akapiga magoti, akamwomba: “Ukitaka, waweza kunitakasa!”[#1:40 Kwa fikira za watu nyakati hizo ukoma ulikuwa ugonjwa wa kuambukiza, uliosababisha mhusika kuwa najisi kidini (Lawi 13—14); aidha ugonjwa huo uliweza kuponywa tu kwa uwezo wa Mungu (2Fal 5:7; rejea pia Mat 11:5; Luka 7:22).; #1:40 Ishara ya kukiri uwezo na nguvu yake Yesu. Katika Injili ya Luka tunaambiwa kwamba huyo mtu alianguka kufudifudi (Luka 5:12) lakini Marko na Mathayo wanapatana kwamba huyo mtu alipiga magoti ingawa ni maeneo tofauti yanatumika.; #1:40 Rejeo kwa utakaso wa kiibada. Sheria za utakaso zimo katika Lawi 13—14.]

41Yesu akamwonea huruma, akanyosha mkono wake, akamgusa na kumwambia, “Nataka! Takasika!”[#1:41 Twasoma hivyo katika hati za kale. Nyingine zina: “akakasirika”.]

42Mara ukoma ukamwacha mtu huyo, akatakasika.

43Kisha Yesu akamwambia aende zake upesi na kumwambia,

44“Angalia usimwambie mtu yeyote jambo hili, ila nenda ukajioneshe kwa kuhani na ukatoe sadaka kwa ajili ya kutakasika kwako kama alivyoamuru Mose kuwathibitishia kwamba umepona.”[#1:44 Taz Lawi 14:2-32 na pia Mat 8:4.]

45Lakini huyo mtu akaenda, akaanza kueneza habari hiyo kila mahali na kusema mambo mengi hata Yesu hakuweza tena kuingia katika mji wowote waziwazi; ikamlazimu kukaa nje, mahali pa faragha. Hata hivyo, watu wakamwendea kutoka kila upande.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania