The chat will start when you send the first message.
1Yesu akaendelea kuwaambia, “Kweli nawaambieni, wako wengine papa hapa ambao hawatakufa kabla ya kuuona ufalme wa Mungu ukija kwa enzi.”[#9:1 Tamko hilo la Yesu (taz pia Mat 16:28) ni kitendawili kikubwa kwa wafafanuzi wa maandishi ya Biblia. Yaonekana lakini kwamba mbali na wengi wanavyoelewa tamko hilo, yahusu hasa tukio la kufa na kufufuka kwake Yesu. Hilo ndilo tukio lililofanyika kwa utukufu mwingi na wengi wa wasikilizaji wake Yesu walipata kushuhudia tukio hilo.]
2Baada ya siku sita, Yesu aliwachukua Petro, Yakobo na Yohane juu ya mlima mrefu peke yao. Huko, Yesu akageuka sura mbele yao,[#9:2 Habari tunazopewa hapa ni jaribio la kueleza mabadiliko ya ngazi ya juu sana kuhusu mambo ya mbinguni kwa lugha ya binadamu (taz Rom 12:2; 2Kor 3:18; Fil 3:21).]
3mavazi yake yakang'aa, yakawa meupe sana, jinsi dobi yeyote duniani asingeweza kuyafanya meupe.
4Elia na Mose wakawatokea, wakazungumza na Yesu.[#9:4 Mal 4:5-6; taz Mat 17:3. Kuhusu Elia yafaa kukumbuka kwamba katika mapokeo, yeye anasemekana kwamba atakuja tena kabla ya nyakati za mwisho, yaani kabla ya kufika ile siku ya Bwana. Naye Mose itakumbukwa kwamba alikuwa mhusika mkuu katika mpango wa Mungu wa kuwatoa Waisraeli utumwani Misri na pia yeye ni nabii wa pekee aliyehusika na Agano la Mungu na Waisraeli.]
5Petro akamwambia Yesu, “Mwalimu, ni vizuri sisi kuwapo hapa. Basi, afadhali tujenge vibanda vitatu: kimoja chako, kimoja cha Mose na kimoja cha Elia.”[#9:5 Hapa twakumbushwa labda sikukuu ya vibanda (Lawi 23:39-43) ambayo iliadhimishwa kukumbuka wazee wa Waisraeli walipotangatanga jangwani baada ya kutoka Misri. Kuhusu sikukuu hiyo taz Lawi 23:33-43.]
6Yeye na wenzake waliogopa hata hakujua la kusema.
7Kisha likatokea wingu likawafunika, na sauti ikasikika kutoka katika hilo wingu, “Huyu ni Mwanangu mpendwa, msikilizeni.”[#9:7 Katika A.K. wingu lilitumika pale ambapo mwandishi alitaka kuelezea kutokea na kuweko kwake Mungu (Kut 13:21-22; 16:10; 19:9; 2Nya 5:13-14).; #9:7 Neno hili latukumbusha Kumb 18:15.]
8Mara wanafunzi hao wakatazama tena, lakini hawakumwona mtu mwingine, ila Yesu peke yake pamoja nao.
9Basi, walipokuwa wanashuka mlimani, Yesu aliwakataza wasimwambie mtu yeyote mambo waliyoyaona, mpaka Mwana wa Mtu atakapokuwa amefufuka kutoka kwa wafu.[#9:9 Taz maelezo ya 1:34.]
10Basi, wakashika agizo hilo, lakini wakawa wanajadiliana wao kwa wao maana ya kufufuka kutoka kwa wafu.
11Wakamwuliza Yesu, “Mbona waalimu wa sheria wanasema ni lazima kwanza Elia aje?”
12Naye akawajibu, “Naam, Elia anakuja kwanza kutayarisha yote. Hata hivyo, kwa nini basi imeandikwa katika Maandiko Matakatifu kwamba Mwana wa Mtu atapatwa na mateso mengi na kudharauliwa?[#9:12-13 Taz Mat 17:12-13. Yesu anaeleza dhahiri kwamba unabii uliotangazwa katika Malaki 4:5 umekamilika kwa huduma ya Yohane Mbatizaji.; #9:12 Sio swali la kujibu ila mtindo huo wa kuuliza una shabaha ya kutilia mkazo kwamba kuteswa kwake ni jambo lililoazimiwa (na Mungu). Taz 8:31 na rejea 14:21; Luka 24:44,46; Mate 13:29.]
13Lakini nawaambieni, Elia amekwisha kuja, nao wakamtendea walivyotaka kama ilivyoandikwa juu yake.”
14Walipowafikia wale wanafunzi wengine, waliona umati mkubwa wa watu hapo. Na baadhi ya waalimu wa sheria walikuwa wanajadiliana nao.
15Mara tu ule umati wa watu ulipomwona, wote walishangaa sana, wakamkimbilia wamsalimu.
16Yesu akawauliza, “Mnajadiliana nini nao?”
17Hapo mtu mmoja katika ule umati wa watu akamjibu, “Mwalimu, nimemleta mwanangu kwako, ana pepo aliyemfanya kuwa bubu.
18Kila mara anapomvamia, humwangusha chini na kumfanya atokwe na povu kinywani, akisaga meno na kuwa mkavu mwili wote. Niliwaomba wanafunzi wako wamtoe huyo pepo lakini hawakuweza.”
19Yesu akawaambia, “Enyi kizazi kisicho na imani! Nitakaa nanyi mpaka lini? Nitawavumilia mpaka lini? Mleteni kwangu.”
20Wakampeleka. Mara tu huyo pepo alipomwona Yesu, alimtia mtoto kifafa, naye mtoto akaanguka chini, akagaagaa na kutoka povu kinywani. Yesu akamwuliza baba yake huyo mtoto,
21“Amepatwa na mambo hayo tangu lini?” Naye akamjibu, “Tangu utoto wake.
22Na mara nyingi pepo huyo amemwangusha motoni na majini, ili amwangamize kabisa. Basi, ikiwa waweza, utuhurumie na kutusaidia!”
23Yesu akamwambia, “Ati ikiwa waweza! Mambo yote yanawezekana kwa mtu aliye na imani.”[#9:23 Taz maelezo ya 2:5 na pia 11:22-23. Ni dhahiri kwamba maneno haya yana lengo la kuonesha umuhimu wa kuamini.]
24Hapo, huyo baba akalia kwa sauti, “Naamini! Lakini imani yangu haitoshi, nisaidie.”
25Yesu alipouona umati wa watu unaongezeka upesi mbele yake, alimkemea yule pepo mchafu “Pepo unayemfanya huyu mtoto kuwa bubu na kiziwi, nakuamuru, mtoke mtoto huyu wala usimwingie tena!”
26Hapo huyo pepo alipaza sauti, akamwangusha huyo mtoto chini, kisha akamtoka. Mtoto alionekana kama maiti, hata wengine walisema, “Amekufa!”
27Lakini Yesu akamshika mkono, akamwinua, naye akasimama.
28Basi, Yesu alipoingia nyumbani, wanafunzi wake walimwuliza kwa faragha, “Kwa nini sisi hatukuweza kumtoa?”
29Naye akawaambia, “Pepo wa aina hii hawezi kutoka isipokuwa kwa sala.”[#9:29 Hati nyingine za kale zina: “na kufunga.”]
30Yesu na wanafunzi wake waliondoka hapo, wakaendelea na safari kupitia wilaya ya Galilaya. Yesu hakupenda watu wajue alipokuwa,
31kwa sababu alikuwa anawafundisha wanafunzi wake. Aliwaambia, “Mwana wa Mtu atakabidhiwa kwa watu ambao watamuua; lakini siku ya tatu baada ya kuuawa atafufuka.”
32Wanafunzi hawakufahamu jambo hilo. Wakaogopa kumwuliza.
33Basi, walifika Kafarnaumu. Na alipokuwa nyumbani, aliwauliza, “Mlikuwa mnajadiliana nini njiani?”[#9:33 Labda nyumbani kwa Simoni Petro (Marko 1:29) au, nyumbani kwake Yesu mwenyewe (Mat 9:1).]
34Lakini wao wakanyamaza, maana njiani walikuwa wamebishana ni nani aliyekuwa mkubwa kati yao.[#9:34 Luka 22:24]
35Yesu akaketi chini, akawaita wale kumi na wawili, akawaambia, “Mtu akitaka kuwa wa kwanza lazima awe wa mwisho na mtumishi wa wote.”[#9:35 Taz Mat 20:26-27 na sehemu sambamba.]
36Kisha akamchukua mtoto mdogo, akamsimamisha kati yao, akamkumbatia, halafu akawaambia,
37“Anayempokea mtoto kama huyu kwa jina langu, ananipokea mimi; na anayenipokea mimi, hanipokei mimi tu, bali anampokea yule aliyenituma.”
38Yohane akamwambia, “Mwalimu, tumemwona mtu mmoja akitoa pepo kwa kulitumia jina lako, nasi tukajaribu kumkataza kwa kuwa yeye si mmoja wetu.”
39Lakini Yesu akasema, “Msimkataze, maana hakuna mtu anayefanya mwujiza kwa jina langu, na papo hapo akaweza kusema mabaya juu yangu.
40Maana, asiyepingana nasi, yuko upande wetu.[#9:40 Taz Mat 12:30; Luka 11:23.]
41Mtu yeyote atakayewapeni kikombe cha maji ya kunywa, kwa sababu nyinyi ni watu wake Kristo, hakika hatakosa kupata tuzo lake.[#9:41 Taz Mat 10:42.]
42“Yeyote atakayemkosesha mmoja wa hawa wadogo wanaoniamini, ingekuwa afadhali kwa mtu huyo kufungiwa shingoni mwake jiwe kubwa la kusagia na kutupwa baharini.[#9:42 Neno kwa neno “Jiwe la punda la kusagia”. Lilikuwa jiwe ambalo liliburutwa na punda wakati wa kuponda vikonyo vya nafaka ili kuotenganisha punje zake.]
43Mkono wako ukikukosesha, ukate! Afadhali kuingia katika uhai bila mkono mmoja, kuliko kuwa na mikono miwili na kwenda katika moto wa Jehanamu.[#9:43 Hapa na 9:45,47, bila shaka ni msemo ambao una shabaha ya kutilia mkazo umuhimu wa kuondoa kila kitu ambacho kinaweza kusababisha upotovu. Taz pia Mat 5:29-30, maelezo.; #9:43 Yaani uhai wa milele (taz 10:17).; #9:43 Neno lenyewe latokana na mahali paitwapo “Gehinomu” au bonde la Hinomu, karibu na Yerusalemu (2Fal 23:10) mahali ambapo hapo kale palikuwa mashuhuri kama mahali watu walipotambika watoto wao. Mahali hapo palitiwa unajisi na Mfalme Yosia na baadaye palitumiwa kama mahali pa kutupa takataka na moto uliwaka huko daima. Kwa hiyo “jehanamu” au “jehunumu” limekuwa jina mahsusi la kutaja mahali waovu watakapoadhibiwa katika hukumu ya mwisho.]
45Na mguu wako ukikukosesha, ukate! Afadhali kuingia katika uhai bila mguu mmoja, kuliko kuwa na miguu yote miwili na kutupwa katika moto wa Jehanamu.[#9:45 Baadhi ya hati za kale zinaongeza hapa aya ya 46. “Humo, wadudu wake hawafi na moto hauzimiki”.]
47Na jicho lako likikukosesha, ling'oe! Afadhali kuingia katika ufalme wa Mungu ukiwa na jicho moja tu, kuliko kuwa na macho yako yote mawili na kutupwa katika moto wa Jehanamu.
48Humo wadudu wake hawafi, na huo moto hauzimiki.
49“Maana kila mmoja atatiwa chumvi kwa moto.[#9:49 Tafsiri nyingine: “Kila mmoja atatiwa chumvi kwa moto”. Hatuna ufafanuzi unaoridhisha wa msemo huu. Baadhi ya wafafanuzi wanaona yawezekana kuelewa msemo huu kimfano: Wote watatakaswa kwa moto kama vile dhahabu, na kwa chumvi. Chumvi ilitumika katika matambiko kuitakasa hiyo tambiko ikubalike kwa Mungu (Lawi 2:13; Eze 43:24).]
50Chumvi ni nzuri, lakini ikipoteza ladha yake, itakolezwa na nini? Muwe na chumvi ndani yenu na kudumisha amani kati yenu.”[#9:50 Licha ya kwamba chumvi ilitumika kuhifadhi vyakula na pia kuvitia ladha, inawezekana kwamba Yesu anawataka wafuasi wake wawe miongoni mwao na ladha nzuri ya amani na utengemano. Kwa hiyo maana ya msemo huo inakaribia ile ya Mat 5:13 (taz pia Luka 14:34-35).]