Nehemia 1

Nehemia 1

1Lifuatalo ni simulizi la Nehemia, mwana wa Hakalia.[#1:1 Jina hili ambalo katika Kiebrania lina maana ya “Mwenyezi-Mungu hufariji” lilikuwa jina la kawaida sana nyakati za kale za Waisraeli (Ezra 2:1-2; Neh 3:16).; #1:1—7:73 Sehemu hii ya kwanza ya kitabu cha Nehemia inahusu kurejea kwake Yerusalemu ili kujenga upya kuta za mji huo. Kama vile Ezra (Ezra 7—10) safari ya Nehemia iliruhusiwa na mfalme wa Persia. Ujenzi wa ukuta wa Yerusalemu ulipingwa na wengine lakini kwa ujasiri, uongozi bora na hasa tegemeo lake kwa Mungu, Nehemia aliweza kufaulu. Sehemu hii inaelezwa kwa kutumia nafsi ya kwanza, jambo ambalo limewafanya wengi kudhani yahusu kumbukumbu ya mambo yaliyomsibu Nehemia mwenyewe.]

Jukumu la Nehemia kuhusu Yerusalemu

Ikawa, nilipokuwa katika mji mkuu wa Susa, katika mwezi wa Kislevu wa mwaka wa ishirini,

2Hanani, mmoja wa ndugu zangu, akaja pamoja na baadhi ya watu toka nchini Yuda. Nikawauliza kuhusu Wayahudi wenzetu waliosalimika, yaani ambao hawakuhamishiwa Babuloni na kuhusu mji wa Yerusalemu.[#1:2 Hapa yamkini yahusu wale Wayahudi ambao hawakupelekwa uhamishoni Babuloni na pia wale ambao walikuwa katika kundi la kwanza lililorejea wakati mfalme Koreshi alipowaruhusu warejee makwao.]

3Wao wakaniambia, “Wayahudi waliosalimika na kubaki katika mkoa ule, wako katika taabu na aibu. Ukuta wa mji wa Yerusalemu umebomolewa na malango yake yameteketea.”[#1:3 Baadhi ya wafafanuzi wanafikiri hapa yahusu tukio lililofanyika karibuni na sio lile la kuteketezwa kwa mji wa Yerusalemu na majeshi ya Nebukadneza mwaka 587 K.K.]

4Niliposikia hayo nilikaa chini na kulia, nikaomboleza kwa siku kadhaa. Nikafunga na kumwomba Mungu wa mbinguni,

5nikisema, “Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa mbinguni, wewe u Mungu aliye mkuu na wa kutisha, unalishika agano lako na unawafadhili wale wakupendao na kuzishika amri zako.

6Yasikilize kwa makini maombi yangu, na uniangalie mimi mtumishi wako, ninapokuomba kwa ajili ya watumishi wako, watu wa Israeli, usiku na mchana. Ninaungama dhambi za watu wa Israeli, tulizofanya mbele yako. Mimi pamoja na watu wa jamaa yangu tumefanya dhambi.

7Tumetenda mabaya mbele yako, hatujazishika amri zako, kanuni na maagizo yako uliyomwagiza mtumishi wako Mose.[#1:7 Kama vile mtangulizi wake, yaani Ezra (Ezra 9:6-15), Nehemia naye anakiri kwamba yeye na familia yake wanashiriki dhambi ya Waisraeli.]

8Kumbuka sasa lile ulilomwambia mtumishi wako Mose, uliposema, ‘Kama hamtakuwa waaminifu, nitawatawanya miongoni mwa mataifa.

9Lakini mkinirudia, mkazishika amri zangu na kuzifuata hata ingawa nitakuwa nimewatawanya mbali kabisa, nitawarudisha mahali nilipochagua kuwa mahali pangu pa kuabudiwa.’

10Watu wa Israeli ni watumishi wako na watu wako uliwakomboa kwa uwezo wako na mkono wako wenye nguvu.

11Ee Bwana, yasikie maombi yangu mimi mtumishi wako na ya watumishi wako wanaofurahia kukutii wewe. Nakuomba unifanikishe leo, mimi mtumishi wako, na kunijalia kuhurumiwa na mfalme.”

Basi, mimi nilikuwa na jukumu la kumpa mfalme kinywaji.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania