Zaburi 14

Zaburi 14

Uovu wa watu

1Wapumbavu hujisemea moyoni:[#14:1 Neno la Kiebrania lililotafsiriwa hapa kama “mpumbavu” katika mazingira haya linamtaja mtu ambaye kimsingi ni mwovu. Mpumbavu hamtegemei Mungu na hana upendo kwa watu, na hana hekima (Mhub 2:14).]

“Hakuna Mungu.”

Wote wamepotoka kabisa,

wametenda mambo ya kuchukiza;

hakuna hata mmoja atendaye jema!

2Mwenyezi-Mungu anawaangalia wanadamu kutoka mbinguni,

aone kama kuna yeyote mwenye busara,

kama kuna yeyote anayemtafuta Mungu.

3Lakini wote wamekosa,

wote wamepotoka pamoja;

hakuna atendaye mema,

hakuna hata mmoja.

4“Je, hao watendao maovu hawana akili?

Wanawatafuna watu wangu kama mikate;

wala hawanijali mimi Mwenyezi-Mungu.”

5Hapo watashikwa na hofu kubwa,

maana Mungu yu pamoja na waadilifu.

6Unaweza kuvuruga mipango ya maskini,[#14:6 Taz 9:8-9 na 12:5 maelezo.]

lakini Mwenyezi-Mungu ndiye kimbilio lake.

7Laiti ukombozi wa Israeli ungefika kutoka Siyoni!

Mwenyezi-Mungu atakaporekebisha hali ya watu wake,

wazawa wa Yakobo watashangilia;

Waisraeli watafurahi.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania