Zaburi 149

Zaburi 149

Wimbo wa ushindi

1Msifuni Mwenyezi-Mungu!

Mwimbieni Mwenyezi-Mungu wimbo mpya;

msifuni katika kusanyiko la waaminifu!

2Furahi ee Israeli kwa sababu ya Muumba wako,

wakazi wa Siyoni shangilieni kwa sababu ya Mfalme wenu.

3Lisifuni jina lake kwa ngoma,

mwimbieni kwa ngoma na zeze.

4Maana Mwenyezi-Mungu hupendezwa na watu wake;

yeye huwapamba wanyonge kwa ushindi.

5Watu waaminifu wafurahi kwa fahari;

washangilie hata walalapo.

6Wabubujike sifa kuu za Mungu,

na panga zenye makali kuwili mikononi mwao,

7wawalipe kisasi watu wa mataifa,

wawaadhibu watu wasiomjua Mungu;

8wawafunge wafalme wao kwa minyororo,

na viongozi wao kwa pingu za chuma,

9kusudi watekeleze adhabu iliyoamriwa![#149:6-9 Hapa sifa na kelele za shangwe na panga vinaonekana kama vita vya kulipiza kisasi. Ufafanuzi wa aya hizi si dhahiri. Katika Agano Jipya picha ya namna hiyo haitajwi na waandishi wake ila tu nguvu ya Mungu inayofanya kazi miongoni mwao (2Kor 10:3-5; Efe 6:12-17; Ebr 4:12) na kuwawezesha kuwa mfano hai wa upendo wake Mungu.]

Hiyo ndiyo fahari ya waaminifu wa Mungu.

Msifuni Mwenyezi-Mungu!

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania