Zaburi 41

Zaburi 41

Sala ya mgonjwa

1Heri mtu anayewajali maskini;

Mwenyezi-Mungu atamwokoa wakati wa shida.

2Mwenyezi-Mungu atamlinda na kumweka hai,

naye atafanikiwa katika nchi;

Mungu hatamwacha makuchani mwa maadui zake.

3Mwenyezi-Mungu atamsaidia awapo mgonjwa,

atamponya maradhi yake yote.

4Nami nilisema: “Unifadhili, ee Mwenyezi-Mungu,

unihurumie maana nimekukosea wewe.”

5Madui zangu husema vibaya juu yangu:

“Atakufa lini na jina lake litoweke!”

6Wanitembeleapo husema maneno matupu;

wanakusanya mabaya juu yangu,

na wafikapo nje huwatangazia wengine.

7Wote wanichukiao hunong'onezana juu yangu;

wananiwazia mabaya ya kunidhuru.

8Husema: “Maradhi haya yatamuua;

hatatoka tena kitandani mwake!”

9Hata rafiki yangu wa moyoni niliyemwamini,

rafiki ambaye alishiriki chakula changu,

amegeuka kunishambulia!

10Ee Mwenyezi-Mungu, unionee huruma!

Unipe nafuu, nami nitawalipiza.

11Hivyo nitajua kwamba unapendezwa nami,

maadui zangu wasipopata fahari juu yangu.

12Wewe umenitegemeza kwani natenda mema;

waniweka mbele yako milele.

13Asifiwe Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli,

tangu milele na hata milele!

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania