Ufunuo 1

Ufunuo 1

1Huu ni ufunuo aliotoa Yesu Kristo, ambao Mungu alimpa awaoneshe watumishi wake mambo ambayo yanapaswa kutukia karibuni. Kristo alimtuma malaika wake amjulishe mtumishi wake Yohane mambo hayo.[#1:1 Neno kwa neno: Ufunuo wa Yesu Kristo. Yesu Kristo ndiye anayemjulisha Yohane mambo hayo, na chanzo cha ufunuo huo ni Mungu mwenyewe.; #1:1 Tazama Dan 2:28; taz pia Ufu 4:1; 22:10.; #1:1 Si dhahiri ni malaika yupi anahusika hapa. Malaika wengi tofauti wanatajwa katika maono ya kitabu hiki. Wanatokea mmojammoja, au katika kikundi cha watatu (14:6-9), wa nne (7:1), saba (sura 15 na 16).; #1:1-8 Hiki kisehemu ni utangulizi wa kitabu chenyewe. Tunaambiwa mambo matatu muhimu: Ujumbe wa ufunuo watoka kwa Mungu na kwa Kristo mkuu wa watawala wote wa dunia; kifo chake ni kitovu cha yote nacho kimetukomboa kutoka dhambi zetu (aya 5).]

2Naye Yohane ameshuhudia yote aliyoyaona kuhusu ujumbe wa Mungu na ushahidi wa Yesu Kristo.[#1:2 Hapa yamkini yahusu ujumbe kuhusu Yesu Kristo au pia ushahidi alioutoa yeye mwenyewe na kuuthibitisha kwa kifo chake (aya 5).]

3Heri yake mtu anayesoma kitabu hiki chenye maneno ya ujumbe wa kinabii; na heri yao wanaosikia na kushika yaliyoandikwa humu, maana wakati wa mambo haya umekaribia.[#1:3 Kuna Heri saba zinazotajwa katika kitabu hiki, hapa ikiwa ni mara ya kwanza (14:13; 16:15; 19:9; 20:6; 22:7,14). Tazama pia Mat 5:3-11 na sehemu sambamba katika Luka (6:20-23) ambapo neno Heri linatumika vilevile. Taz Zab 1:1.; #1:3 Rejea Ufu 19:10; 22:6-10,18-19 na pia tazama 1Kor 14:1 maelezo.; #1:3 Wakati ambapo mambo yanayotajwa yatatimia.]

Salamu kwa makanisa saba

4Mimi Yohane nayaandikia makanisa saba yaliyoko Asia. Nawatakieni neema na amani kutoka kwake yeye aliyeko, aliyekuwako na anayekuja; na kutoka kwa roho saba walio mbele ya kiti chake cha enzi,[#1:4 Rom 1:7; 1Kor 1:3; Gal 1:3.; #1:4 Tazama pia 1:8; 11:17; 16:5. Msemo huu wahusu jina au kitambulisho cha Mungu kulingana na Kut 3:14-15.; #1:4 Rejea Ufu 3:1; 4:5; 5:6. Yahusu, au malaika, au namna mbalimbali za kujionesha kwa Mungu. Tarakimu “saba” hutumika mara nyingi katika kitabu cha Ufunuo kama “ishara” ya ukamilifu au upeo.; #1:4-5a Kitabu cha Ufunuo kinaanza kwa mtindo wa kawaida wa barua za nyakati hizo kikimtambulisha mwandishi na waandikiwa pamoja na salamu. Waandikiwa ni jumuiya za makanisa saba ya Asia Ndogo, eneo ambalo sasa ni Uturuki. Idadi saba yamkini inatumiwa hapa kama mfano wa makanisa yote. Aidha katika kuwatakia salamu Yohane anatamka utatu wa Uungu: Baba “aliyeko, aliyekuwako na anayekuja”, Roho: “roho saba walio mbele ya kiti chake cha enzi”; Mwana: Yesu Kristo.]

5na kutoka kwa Yesu Kristo, shahidi mwaminifu, wa kwanza kufufuliwa kutoka kwa wafu, na ambaye ni mtawala wa wafalme wa dunia.[#1:5 Tazama 1:2, 9; 6:9; 12:11; 17:6. Angalia pia Isa 55:4; 1Tim 6:13.; #1:5 Mate 26:23; Kol 1:18.; #1:5 Zab 89:27; taz pia Rom 14:9.]

Yeye anatupenda, na kwa damu yake ametufungua kutoka vifungo vya dhambi zetu,

6akatufanya sisi kuwa ufalme wa makuhani, tumtumikie Mungu, Baba yake. Kwake Yesu Kristo uwe utukufu na nguvu, milele na milele! Amina.[#1:6 Tazama Kut 19:6 ambapo maneno hayo yanahusu taifa la Israeli na sasa yanatumiwa kuhusu taifa jipya la Mungu, yaani kanisa.; #1:6 Neno la Kiebrania ambalo lilitumika kuthibitisha kilichosemwa na hapa latumika vivyo hivyo. Katika 3:14 linatumiwa kama jina la Kristo. Tazama pia 5:14; 7:12; 19:4; 2Kor 1:20.]

7Tazama! Anakuja na mawingu![#1:7 Maelezo ya aya hii yanatumia maneno yaliyotumiwa katika Dan 7:13 na Zek 12:10. Maneno hayo ya A.K. yanatumika pia katika Mat 24:30; Marko 13:26; Luka 21:27; Yoh 19:34-37.]

Kila mtu atamwona, na hata wale waliomtoboa.

Makabila yote duniani yataomboleza juu yake.

Naam! Amina.

8“Mimi ni Alfa na Omega,” asema Bwana Mungu Mwenye Nguvu, aliyeko, aliyekuwako na anayekuja.[#1:8 Tazama Ufu 1:4 maelezo. Alfa na Omega: Herufi ya kwanza na ya mwisho katika alfabeti za Kigiriki. Jina hilo linamaanisha kwa mfano uwezo mkuu wa Mungu katika kila kitu (21:6; 22:13); ni sawa na maana ya: Wa kwanza na wa mwisho (1:17; 2:8; 22:13); na Mwanzo na Mwisho (21:6; 22:13). Jina hilo la sifa anapewa Mungu hapa na Kristo katika 1:17; 2:8; 22:13.; #1:8 Taz maelezo ya 1:4.]

Njozi ya Mwana wa Mtu

9Mimi ni Yohane, ndugu yenu, ambaye kwa kuungana na Yesu, nashiriki pamoja nanyi mateso na ufalme wake na uvumilivu thabiti. Mimi nilikuwa katika kisiwa kiitwacho Patmo kwa sababu ya kuhubiri neno la Mungu na kumshuhudia Yesu.[#1:9 Kisiwa kidogo katika bahari ya Ageo, kusini-mashariki mwa Efeso ambamo Waroma waliwaweka baadhi ya wafungwa wao wa kisiasa.]

10Basi, wakati mmoja, siku ya Bwana, nilikumbwa na Roho, nikasikia nyuma yangu sauti kubwa kama sauti ya tarumbeta.[#1:10 Kwa mara ya kwanza hapa msemo huo watumiwa kutaja siku ya kwanza ya Juma ambayo ni Jumapili. Hiyo ilikuwa siku ambayo waamini walikutana kuadhimisha Karamu ya Bwana na siku ile alipofufuka.; #1:10 Msemo huu unamaanisha kwamba Yohane alijikuta katika hali ya maono (4:2; 17:3; 21:10 taz pia Mate 10:10; 11:5; 22:6-7). Roho wa Mungu yamkini ndiye anayesababisha hali hiyo.]

11Nayo ilisema, “Andika katika kitabu yale unayoyaona, ukipeleke kwa makanisa haya saba: Efeso, Smurna, Pergamumu, Thuatira, Sarde, Filadelfia na Laodikea.”

12Basi, nikageuka nimwone huyo aliyesema nami, nikaona vinara vya taa saba vya dhahabu,[#1:12 Hivi vinasimamia au vinamaanisha makanisa saba (1:20).]

13na katikati yake kulikuwa na kitu kama Mwana wa Mtu, naye alikuwa amevaa kanzu ndefu na mkanda wa dhahabu kifuani.[#1:13 14:14; ling Dan 7:13. Pia angalia Mwana wa Mtu katika fahirisi.]

14Nywele zake zilikuwa nyeupe kama pamba nyeupe, kama theluji; macho yake yalimetameta kama moto;[#1:14 Taz Dan 7:9. Katika Dan 7:9 ni Mungu, lakini hapa ni Yesu Kristo.]

15miguu yake kama shaba iliyong'arishwa iliyosafishwa katika tanuri ya moto, na sauti yake ilikuwa kama sauti ya poromoko la maji.

16Katika mkono wake wa kulia alikuwa na nyota saba, na kinywani mwake mlitoka upanga wenye makali kuwili. Uso wake uling'aa kama jua kali kabisa.[#1:16 Zatumiwa kama picha ya makanisa saba. Katika aya ya 20 tunaambiwa moja kwa moja kuwa ni malaika.; #1:16 19:15; taz pia Isa 49:2 na Ebr 4:12. Hapa ni picha au mfano wa hukumu ya Mungu.]

17Basi, nilipomwona tu, nilianguka mbele ya miguu yake kama maiti. Lakini yeye akaweka mkono wake wa kulia juu yangu, akasema, “Usiogope! Mimi ni wa kwanza na wa mwisho.[#1:17 Ufu 1:8; 2:8; 22:13; ling Isa 41:4; 44:6,8; 48:12.]

18Mimi ni yeye aliye hai! Nilikuwa nimekufa, lakini, tazama, sasa ni hai milele na milele. Ninazo funguo za kifo na kuzimu.[#1:18 Picha ya mamlaka na uwezo wa Yesu dhidi ya kifo (ling Yoh 5:21,25-29).]

19Basi, sasa andika mambo haya unayoyaona, mambo yanayotukia sasa na yale yatakayotukia baadaye.

20Siri ya nyota zile saba ulizoziona katika mkono wangu wa kulia na siri ya vile vinara saba vya taa vya dhahabu, ni hii: zile nyota saba ni malaika wa makanisa; na vile vinara saba vya taa vya dhahabu ni makanisa saba.[#1:20 Au: “Fumbo” neno litumikalo katika A.J. kwa mfano Marko 4:11; Rom 11:25; 16:25 katika mazingira ya maandishi ya mambo yanayodhihirishwa kwa ufunuo.; #1:20 Katika lugha ya awali ni mjumbe. Hapa waweza kueleweka kama viumbe wa mbinguni kama wale waliotajwa katika Dan 10:13; 12:1 ambao ni walinzi wa mataifa. Katika Ufu 2—3 wanasimama mahali pa makanisa.]

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania