The chat will start when you send the first message.
1Kisha, nikamwona malaika mwingine mwenye nguvu akishuka kutoka mbinguni. Alikuwa amevikwa wingu na upinde wa mvua kichwani mwake. Uso wake ulikuwa kama jua, na miguu yake ilikuwa kama nguzo za moto.[#10:1—11:14 Muundo wa maandishi ya 10:1-11 unafanana na ule wa Eze 1—3. Sehemu hii na ifuatayo, yaani 11:1-14 inatumika kushikilia sehemu iliyotangulia na inayofuata, yaani kati ya tukio la tarumbeta ya sita na ya saba.]
2Mikononi mwake alishika kitabu kidogo kimefunguliwa. Aliweka mguu wake wa kulia juu ya bahari na wa kushoto juu ya nchi kavu,
3na kuita kwa sauti kubwa kama ya mngurumo wa simba. Alipopaza sauti, ngurumo saba ziliitikia kwa kishindo.[#10:3-4 Hapa yaonekana kwamba Mungu ndiye anayehusika katika maelezo hayo; yaani mwandishi anasema ni malaika kuepa kumtaja Mungu moja kwa moja (Zab 29:3-9). Katika Ufunuo kwa jumla ngurumo huhusu aghalabu hasira ya Mungu (Rejea Ufu 8:5; 11:19; 16:18).]
4Na hizo ngurumo saba ziliposema, mimi nikataka kuandika. Lakini nikasikia sauti kutoka mbinguni: “Maneno ya ngurumo hizo saba ni siri; usiyaandike!”
5Kisha, yule malaika niliyemwona akisimama juu ya bahari na juu ya nchi kavu akainua mkono wake wa kulia juu mbinguni,
6akaapa kwa jina la Mungu aishiye milele na milele, Mungu aliyeumba mbingu na vyote vilivyomo, bahari na vyote vilivyomo, dunia na vyote vilivyomo. Akasema, “Wakati wa kusubiri zaidi umekwisha![#10:6 Au: Wakati umekwisha (Dan 12:6-7).]
7Lakini wakati yule malaika wa saba atakapotoa sauti ya tarumbeta yake, Mungu atakamilisha mpango wake wa siri kama alivyowatangazia watumishi wake manabii.”
8Kisha, ile sauti niliyokuwa nimeisikia kutoka mbinguni pale awali ikasema nami tena: “Nenda ukakichukue kile kitabu kilichofunguliwa, kilicho mkononi mwa malaika asimamaye juu ya bahari na juu ya nchi kavu.”[#10:8-11 Rejea 10:2. Ni kitabu kidogo kilicho mviringo (taz Ufu 5:1); kisa hiki chafanana na yaliyompata Ezekieli (Eze 2:7-34) ila hapa badala ya utamu tunapata uchungu ambao wahusu si tu uchungu wa adhabu bali pia uchungu ambao mjumbe atapaswa kuteseka na kufa kwa ajili ya ushuhuda wake.]
9Basi, nikamwendea huyo malaika, nikamwambia anipe hicho kitabu kidogo. Naye akaniambia, “Kichukue, ukile. Kinywani mwako kitakuwa kitamu kama asali, lakini tumboni kitakuwa kichungu!”
10Basi, nikakichukua kitabu hicho kidogo kutoka mkononi mwa huyo malaika, nikakila. Nacho kilikuwa kitamu kinywani mwangu kama asali, lakini nilipokimeza kikawa kichungu tumboni mwangu.
11Kisha, nikaambiwa, “Inakubidi tena kutoa unabii kuhusu watu wengi, mataifa, watu wa lugha nyingi na wafalme!”