The chat will start when you send the first message.
1Kisha nikapewa mwanzi uliokuwa kama kijiti cha kupimia, nikaambiwa, “Inuka, ukalipime hekalu la Mungu, madhabahu ya kufukizia ubani na kawahesabu watu wanaoabudu ndani ya hekalu.[#11:1-2 Rejea Eze 40:3; Zek 2:1-2. Hekalu la Yerusalemu liliharibiwa kabisa mnamo mwaka 70 B.K. na jeshi la Waroma.]
2Lakini uache ukumbi ulio nje ya hekalu; usiupime, maana huo umekabidhiwa watu wa mataifa mengine, ambao wataukanyaga mji mtakatifu kwa muda wa miezi arubaini na miwili.[#11:2 Yerusalemu. Rejea Isa 63:18; Dan 8:13; Luka 21:24.; #11:2 Ufu 13:5; Idadi hiyo ni siku 1260 (aya 3; Ufu 12:6) au miaka mitatu na nusu (Ufu 12:14) ambayo ni nusu ya miaka saba. Hapa kama vile kuhusu tarakimu saba idadi hiyo yatumika kuonesha ukamilifu wa kitu hali nusu yake ni kinyume chake, yaani idadi isiyo timilifu. Taz Ufu 1:4 na rejea Dan 7:25; 12:7.]
3Nami nitawatuma mashahidi wangu wawili ili watoe unabii kwa muda huo wa siku 1,260, wakiwa wamevaa mavazi ya gunia.”[#11:3 Mashahidi hao wawili hawatambulishwi; lakini maelezo yake yanamwafiki Zerubabeli na kuhani Yoshua (Zek 3:1—4:14) na kiasi fulani Elia na Mose (Taz 11:6).; #11:3 Mfano wa wito wao kwa watu waongoke.]
4Hao mashahidi wawili ni miti miwili ya mizeituni na taa mbili zinazosimama mbele ya Bwana wa dunia.
5Kama mtu akijaribu kuwadhuru, moto hutoka kinywani mwao na kuwaangamiza maadui zao; na kila mtu atakayejaribu kuwadhuru atakufa namna hiyo.
6Hao wanayo mamlaka ya kufunga anga, mvua isinyeshe wakati wanapotoa unabii. Tena wanayo mamlaka ya kuzigeuza chemchemi zote za maji ziwe damu, na ya kusababisha maafa ya kila namna duniani kila mara wanapopenda.[#11:6 Kama wakati wa Elia (1Fal 17:1) ambapo ukame ulidumu muda huohuo (taz pia Luka 4:25; Yak 5:17).; #11:6 Kama wakati wa Mose (Kut 7:17-24).]
7Lakini wakisha maliza kutoa unabii huo, mnyama atokaye shimoni kuzimu atapigana nao, atawashinda na kuwaua.
8Maiti zao zitabaki katika barabara za mji mkuu ambapo Bwana wao alisulubiwa. Jina la kupanga la mji huo ni Sodoma au Misri.[#11:8 Ni Yerusalemu ambao hapa unaonekana kama mji uliomwasi Mungu. Mji huo kwa hivyo unatajwa sana kama Sodoma na pia Misri. Rejea Isa 1:10; 3:9.]
9Watu wa kila kabila, lugha, taifa na rangi wataziangalia maiti hizo kwa muda wa siku tatu na nusu, na hawataruhusu zizikwe.
10Watu waishio duniani watafurahia kifo cha hao wawili. Watafanya sherehe na kupelekeana zawadi, maana manabii hawa wawili walikuwa wamewasumbua mno watu wa dunia.
11Lakini baada ya zile siku tatu na nusu pumzi ya uhai kutoka kwa Mungu iliwaingia, nao wakasimama; wote waliowaona wakaingiwa na hofu kuu.
12Kisha, hao manabii wawili wakasikia sauti kubwa kutoka mbinguni ikiwaambia, “Njoni hapa juu!” Nao wakapanda juu mbinguni katika wingu, maadui zao wakiwa wanawatazama.
13Wakati huohuo, kukatokea tetemeko kubwa la ardhi, sehemu moja ya kumi ya ardhi ikaharibiwa. Watu 7,000 wakauawa kwa tetemeko hilo la ardhi. Watu waliosalia wakaogopa sana, wakamtukuza Mungu wa mbinguni.[#11:13 Ufu 14:7; 15:4.]
14Maafa ya pili yamepita; lakini tazama! Maafa ya tatu yanafuata hima.[#11:14 Ufu 9:12; Taz maelezo ya 8:13.]
15Kisha, malaika wa saba akapiga tarumbeta yake. Na sauti kuu zikasikika mbinguni zikisema, “Sasa ufalme wa ulimwengu ni wa Bwana wetu na Kristo wake. Naye atatawala milele na milele!”[#11:15-18 Sehemu hii ya tatu inamalizika kwa utenzi au wimbo wa ushindi kwa kuanzishwa kwa utawala wa milele wa Mungu na wa Kristo.]
16Kisha, wale wazee ishirini na wanne walioketi mbele ya Mungu katika viti vyao vya enzi, wakaanguka kifudifudi, wakamwabudu Mungu,[#11:16 Rejea Ufu 4:9-11 ambapo kuna mpango au muundo wa maelezo unaofanana na ule wa 11:16-18.]
17wakisema:
“Tunakushukuru ee Bwana Mungu Mwenye Nguvu,
uliyeko na uliyekuwako!
Maana umetumia nguvu yako kuu, ukaanza kutawala!
18Watu wa mataifa waliwaka hasira,
lakini ghadhabu yako imefika,
naam wakati wa kuwahukumu wafu.
Ndio wakati wa kuwatuza watumishi wako manabii,
watakatifu na wote wanaolitukuza jina lako, wakubwa kwa wadogo.
Ni wakati wa kuwaangamiza waangamizi wa dunia.”
19Kisha hekalu la Mungu mbinguni likafunguliwa, na sanduku la agano lake likaonekana hekaluni mwake. Kukatokea umeme, sauti, ngurumo, tetemeko la ardhi, na mvua kubwa ya mawe.[#11:19 Au: Mkataba. Latumika kuonesha kuweko kwake Mungu kati ya watu wake (Kut 25:10-22; rejea Ufu 21:3,22).]