The chat will start when you send the first message.
1Kisha, ishara kubwa ikaonekana mbinguni: mwanamke aliyevikwa jua na mwezi chini ya miguu yake na taji ya nyota kumi na mbili juu ya kichwa chake![#12:1-2 Kadiri ya ufafanuzi wa jumla mama huyo ni mfano wa watu wake Mungu, kwanza watu wa Israeli kulingana na vile walivyokuwa au walivyochukuliwa kuwa waaminifu kwa Mungu, na ambao wanateseka maumivu ya kujaliwa mtoto (rejea Mika 5:3) mpaka Masiha ambaye waliahidiwa amezaliwa; ufafanuzi mwingine unaliafiki kanisa ambalo ni watu wanaomwamini Yesu (aya 17; rejea Gal 4:26).]
2Alikuwa mjamzito, naye akapaza sauti kwa maumivu na uchungu wa kujifungua mtoto.
3Kisha, ishara nyingine ikatokea mbinguni: joka kubwa jekundu na lenye pembe kumi na vichwa saba; na kila kichwa kilikuwa na taji.[#12:3 Mnyama wa hadithi za jadi za kale ambaye anatumika kwa mfano wa shetani (aya 9). Picha hii yatokea katika Dan 7:7. Vichwa saba na pembe kumi vinatajwa katika 13:1 na 17:3. Pembe ni mfano wa nguvu. Katika 12:9 Hilo joka linabainishwa kuwa ni Ibilisi au Shetani.]
4Joka hilo liliburuta kwa mkia wake theluthi moja ya nyota za anga na kuzitupa duniani. Nalo lilisimama mbele ya huyo mama aliyekuwa karibu kujifungua mtoto, tayari kabisa kummeza mtoto, mara tu atakapozaliwa.
5Kisha, mama huyo akajifungua mtoto wa kiume ambaye atayatawala mataifa yote kwa fimbo ya chuma. Lakini mtoto akanyakuliwa na kupelekwa kwa Mungu na kwenye kiti chake cha enzi.[#12:5 Ufu 19:15. Rejea Zab 2:9 ambayo yatumika kumtaja Masiha. Taz Ebr 1:5 maelezo.]
6Huyo mama akakimbilia jangwani ambako Mungu alikuwa amemtayarishia mahali pa usalama ambapo angehifadhiwa kwa muda wa siku 1,260.[#12:6 Muda wa siku 1260, au miaka mitatu na nusu ni sawa na ule uliotajwa katika Ufu 11:2-3 (taz maelezo ya aya 2). Hapa mfano wa mwanamke huyo anayekimbilia usalama jangwani wahusu bila shaka kanisa ambalo linalindwa na kukingwa na Mungu wakati linapoteswa; taz 12:1-2 na 12:17 maelezo.]
7Kisha, kukazuka vita mbinguni: Mikaeli na malaika wake walipigana na hilo joka, nalo likawashambulia pamoja na malaika wake.[#12:7 Dan 10:13,21; 12:1; Yuda 9.]
8Lakini joka hilo na malaika wake walishindwa, na hatimaye hapakuwa tena na nafasi mbinguni kwa ajili yao.
9Basi, joka hilo kuu likatupwa nje. Joka hilo ndiye yule nyoka wa kale ambaye huitwa pia Ibilisi au Shetani ambaye huudanganya ulimwengu wote. Naam, alitupwa duniani, na malaika wake wote pamoja naye.[#12:9 Ufu 20:2; rejea Mwa 3:1-5.]
10Kisha nikasikia sauti kubwa kutoka mbinguni ikisema: “Sasa umefika ukombozi na nguvu na ufalme wa Mungu wetu, na mamlaka ya Kristo wake! Maana yule aliyewashtaki ndugu zetu mbele ya Mungu ametupwa chini. Naam, ametupwa chini huyo anayewashtaki usiku na mchana.[#12:10 Mshtaki ni maana ya neno Shetani, rejea Yobu 1:6; Zek 3:1.]
11Ndugu zetu wamemshinda kwa damu ya Mwanakondoo na kwa neno waliloshuhudia; maana hawakuyathamini maisha yao kuwa kitu sana, wakawa tayari kufa.[#12:11 Tazama Yoh 1:29 maelezo; rejea Ufu 5:9 na pia angalia Rom 3:25 maelezo; 1Pet 1:18. “Damu ya Mwanakondoo”: Yahusu kifo cha Yesu msalabani.]
12Kwa sababu hiyo, furahini enyi mbingu na vyote vilivyomo ndani yenu. Lakini, ole wenu nchi na bahari, maana Ibilisi amewajieni akiwa na ghadhabu kuu, kwa sababu anajua kwamba muda wake uliobakia ni mfupi.”
13Joka lilipotambua kwamba limetupwa chini duniani, likaanza kumwinda yule mama aliyekuwa amejifungua mtoto wa kiume.
14Lakini mama huyo akapewa mabawa mawili ya tai apate kuruka mbali sana na hilo joka, mpaka mahali pake jangwani ambapo angehifadhiwa salama kwa muda wa miaka mitatu na nusu.[#12:14 Yagusia kutoka Misri na safari kwenda nchi ya ahadi kupitia jangwani, ambapo hapa panamaanisha usalama na ulinzi. Picha ya mabawa ya tai inatokea katika Kut 19:4; Kumb 32:11.; #12:14 Taz maelezo ya 12:6.]
15Basi, joka likatapika maji mengi kama mto, yakamfuata huyo mama nyuma ili yamchukue.
16Lakini nchi ikamsaidia huyo mama: ikajifunua kama mdomo na kuyameza maji hayo yaliyotoka kinywani mwa hilo joka.
17Basi, joka hilo likamkasirikia huyo mama, likajiondokea, likaenda kupigana na wazawa wengine wa huyo mama, yaani wote wanaotii amri za Mungu na kumshuhudia Yesu.[#12:17 Wazawa wengine wa huyo mama ni Wakristo ambao wanafuata kwa uaminifu ushuhuda wa Yesu (taz 12:6). Rejea Dan 7:7,21.]
18Basi, likajisimamia ukingoni mwa bahari.[#12:18 Yamkini kungojea mnyama anayesemwa katika sura inayofuata atokee. Makala ya Kiebrania yana “yeye” (kiume) na baadhi ya hati za kale zina “Mimi”.]