The chat will start when you send the first message.
1Kisha, nikaona mlima Siyoni na Mwanakondoo amesimama juu yake; pamoja naye walikuwa watu 144,000 ambao juu ya paji za nyuso zao walikuwa wameandikwa jina la Mwanakondoo na jina la Baba yake.[#14:1 Jina lingine la Yerusalemu.; #14:1 Taz 7:4 maelezo.]
2Basi, nikasikia sauti kutoka mbinguni, sauti iliyokuwa kama ya maji mengi na kama ya ngurumo kubwa. Sauti niliyosikia ilikuwa kama sauti ya wachezaji muziki wakipiga vinubi vyao.
3Walikuwa wanaimba wimbo mpya mbele ya kiti cha enzi na mbele ya wale viumbe hai wanne na wale wazee. Hakuna mtu aliyeweza kujifunza wimbo huo isipokuwa hao watu 144,000 waliokombolewa duniani.
4Watu hao ndio wale ambao hawakujichafua na wanawake, nao ni mabikira. Wao humfuata Mwanakondoo kokote aendako. Wamekombolewa kutoka miongoni mwa binadamu wengine, wakawa wa kwanza kutolewa kwa Mungu na kwa Mwanakondoo.[#14:4 Yaani, hawa hawakuabudu au kuandamana na miungu ya uongo, kitendo ambacho katika A.K. kilitajwa mara nyingi kama kufanya uzinzi. Tazama Ufu 2:14 maelezo.; #14:4 Kut 23:19; Yak 1:18. Wazo ni lile la kufikiria mazao ya kwanza kabisa kuvunwa ambayo ni ya maana kubwa kuliko yote kuwa ni mali yake Mungu, nayo ni ya thamani kuu au ya pekee.]
5Hawakupata kamwe kuwa waongo; hawana hatia yoyote.[#14:5 Hawakuabudu au kuiomba miungu ya uongo jambo ambalo mara kwa mara katika A.K. linatajwa kama udanganyifu. Rejea Sef 3:13.]
6Kisha, nikamwona malaika mwingine anaruka juu angani akiwa na Habari Njema ya milele ya Mungu, aitangaze kwa watu waishio duniani, kwa mataifa yote, makabila yote na watu wa lugha zote na rangi zote.[#14:6-20 Sehemu ya picha ya Mwana wa Mtu ambayo inatanguliwa na malaika watatu (14:6-13) na kufuatiliwa na malaika wengine watatu (14:14-20) na wote, yaani pamoja na Mwana wa Mtu, ni saba. Picha zao zinatangaza kutekelezwa kwa hukumu.]
7Naye akasema kwa sauti kubwa, “Mcheni Mungu na kumtukuza! Maana saa imefika ya kutoa hukumu yake. Mwabuduni yeye aliyeumba mbingu na dunia, bahari na chemchemi za maji.”
8Malaika wa pili alimfuata huyo wa kwanza akisema, “Ameanguka! Naam, Babuloni mkuu ameanguka! Babuloni ambaye aliwapa mataifa yote wainywe divai yake — divai kali ya uzinzi wake!”[#14:8 Isa 21:9; rejea Dan 4:30. “Babuloni”: Mji ambao katika A.K. waonekana kama adui wa watu wa Israeli na pengine umekuwa lengo la laana ya Mungu (Isa 13:1—14:23; 47:1-15; Yer 50—51). Nyakati za A.J. jina hilo lilitumiwa pia kama mfano wa Roma, mji mkuu wa ufalme wa Roma (1Pet 5:13 maelezo).; #14:8 Yahusu kuabudu miungu ya uongo, neno uzinzi likitumika hapa kama mfano (Yer 51:7-8; Ufu 17:1; 18:2-3). Taz maelezo ya 2:14.]
9Na malaika wa tatu aliwafuata hao wawili akisema kwa sauti kubwa, “Yeyote anayemwabudu yule mnyama na sanamu yake na kukubali kutiwa alama yake juu ya paji la uso wake au juu ya mkono wake,
10yeye mwenyewe atakunywa divai ya ghadhabu ya Mungu ambayo imemiminwa katika kikombe cha ghadhabu yake bila kuchanganywa na maji. Mtu huyo atateseka ndani ya moto wa madini ya kiberiti mbele ya malaika watakatifu na mbele ya Mwanakondoo.[#14:10 Taz 16:19; rejea Isa 51:17; Yer 25:15.; #14:10 Taz 19:20; 20:10; rejea Mwa 19:24; Zab 11:6; Eze 38:21-22. Taz maelezo ya Ufu 9:17.]
11Moshi wa moto unaowatesa hupanda juu milele na milele. Watu hao waliomwabudu huyo mnyama na sanamu yake na kutiwa alama ya jina lake, hawatakuwa na nafuu yoyote usiku na mchana.”
12Hivyo, ni lazima watu wa Mungu, yaani wale wanaotii amri za Mungu na kumwamini Yesu, wawe na uvumilivu.[#14:12 Taz 13:10 na maelezo yake.]
13Kisha, nikasikia sauti kutoka mbinguni ikisema, “Andika! Heri watu ambao tangu sasa wanakufa wakiwa wameungana na Bwana.” Naye Roho asema, “Naam! Watapumzika kutoka taabu zao; maana matunda ya jasho lao yatawafuata.”[#14:13 Matumizi ya neno “Heri” kwa mara ya pili katika kitabu hiki. Tazama maelezo ya 1:3.]
14Kisha, nikatazama, na kumbe palikuwapo wingu jeupe hapo. Na juu ya wingu hilo alikuwako aliye kama Mwana wa Mtu. Alikuwa amevaa taji ya dhahabu kichwani, na kushika mundu mkali mkononi mwake.[#14:14 Taz Ufu 1:13. Rejea Dan 7:13.]
15Kisha malaika mwingine akatoka hekaluni, na kwa sauti kubwa akamwambia yule aliyekuwa amekaa juu ya wingu, “Tafadhali, tumia mundu wako ukavune mavuno, maana wakati wa mavuno umefika; mavuno ya dunia yameiva.”
16Basi, yule aliyekuwa amekaa juu ya wingu akautupa mundu wake duniani, na mavuno ya dunia yakavunwa.
17Kisha, malaika mwingine akatoka katika hekalu mbinguni akiwa na mundu wenye makali.
18Kisha malaika mwingine msimamizi wa moto, akatoka madhabahuni, akamwambia kwa sauti kubwa yule malaika mwenye mundu wenye makali, “Nawe tia huo mundu wako mkali, ukakate vichala vya mizabibu ya dunia, maana zabibu zake zimeiva!”
19Basi, malaika huyo akautupa mundu wake duniani, akakata zabibu za dunia, akazitia ndani ya chombo kikubwa cha kukamulia zabibu, chombo cha ghadhabu ya Mungu.
20Zabibu zikakamuliwa ndani ya hilo shinikizo lililoko nje ya mji, na damu ikatoka katika shinikizo hilo mtiririko wenye kina kufikia hatamu za farasi na urefu upatao kilomita 300.[#14:20 Ufu 19:15 rejea Isa 63:3; Omb 1:15; Yoe 3:13; Hos 2:19-20. Katika A.J. wazo hili linatumika kueleza uhusiano kati ya Kristo na kanisa.; #14:20 Hapa latumika kwa mfano wa hasira ya Mungu katika 14:14; 16:19; 19:15 na huungana na mabakuli saba ya sura ya 16.]