The chat will start when you send the first message.
1Kisha nikaona ishara nyingine mbinguni, kubwa na ya kushangaza. Palikuwa hapo malaika saba wenye mabaa saba ya mwisho. Kwa mabaa hayo saba, ghadhabu ya Mungu imekamilishwa.
2Kisha nikaona kitu kama bahari ya kioo, imechanganywa na moto. Nikawaona pia wale watu waliomshinda yule mnyama na sanamu yake na ambaye jina lake lilitajwa kwa ile tarakimu. Watu hao walikuwa wamesimama kando ya hiyo bahari ya kioo, wakiwa na vinubi walivyopewa na Mungu.[#15:2 Rejea Ufu 4:6. Wengi wanafikiri “bahari” hiyo ni mfano wa “mpaka” uliowekwa na Mungu kuwalinda watu wa Mungu mbali na maadui zake (Kut14).; #15:2—16:21 Sehemu hii ya tano inatupatia maono ya malaika saba ambao wanaimwagia dunia mabakuli yaliyojaa ghadhabu ya Mungu (rejea Ufu 14:19).]
3Walikuwa wakiimba wimbo wa Mose, mtumishi wa Mungu na wa Mwanakondoo:[#15:2-4 Rejea Ufu 14:3; Kut 15:1-8. Mwandishi anataja bahari hapa kukumbusha ushindi wa Mungu dhidi ya Wamisri katika bahari ya Shamu (Kut 14). Sura hii na hiyo ifuatayo zinataja tena visa vinavyofanana sana na matukio yaliyowapata Wamisri.]
“Bwana Mungu Mwenye Nguvu,
matendo yako ni makuu na ya ajabu mno!
Ewe Mfalme wa mataifa,
njia zako ni za haki na za kweli!
4Bwana, ni nani asiyekucha wewe?
Nani asiyelitukuza jina lako?
Wewe peke yako ni Mtakatifu.
Mataifa yote yatakujia na kukuabudu
maana matendo yako ya haki yamedhihirishwa.”
5Baada ya hayo nikaona hekalu limefunguliwa mbinguni, na ndani yake hema ya kuwapo kwa Mungu.[#15:5 Neno kwa neno: “Hekalu la hema ya ushuhuda” Ufu 11:19; rejea Kut 38:21. Hes 9:15; 18:2. Laitwa pia Hema ya Mkutano; matumizi ambayo yakumbusha kukaa kwa Waisraeli kule jangwani.]
6Basi, wale malaika saba wenye mabaa saba wakatoka humo hekaluni, wakiwa wamevaa nguo za kitani safi zenye kung'aa na kanda za dhahabu vifuani mwao.
7Kisha, mmojawapo wa wale viumbe wanne akawapa hao malaika saba mabakuli ya dhahabu yaliyojaa ghadhabu ya Mungu, aishiye milele na milele.
8Hekalu likajaa moshi uliosababishwa na utukufu na nguvu ya Mungu, na hakuna mtu aliyeweza kuingia hekaluni mpaka mwisho wa mabaa saba ya wale malaika saba.