The chat will start when you send the first message.
1Kisha nikasikia sauti kubwa kutoka hekaluni ikiwaambia wale malaika saba, “Nendeni mkamwage mabakuli hayo saba ya ghadhabu ya Mungu duniani.”
2Basi, malaika wa kwanza akaenda akamwaga bakuli lake juu ya nchi. Mara madonda mabaya na ya kuumiza sana yakawapata wote waliokuwa na alama ya yule mnyama na wale walioiabudu sanamu yake.[#16:2-21 Maangamizi yanayosababishwa na umwagaji wa mabakuli yanafanana na yale yaliyosababishwa na zile tarumbeta, nayo yatukumbusha juu ya mapigo yale ya Misri. Maangamizi yaliyosababishwa na zile tarumbeta yaliwapa watu fursa ya kutubu kabla ya maangamizi kamili ya mwisho.]
3Kisha malaika wa pili akamwaga bakuli lake baharini. Nayo bahari ikawa damu tupu kama damu ya mtu aliyekufa, na viumbe vyote hai baharini vikafa.
4Malaika wa tatu akamwaga bakuli lake katika mito na chemchemi za maji, navyo vikageuka damu.
5Nikamsikia malaika msimamizi wa maji akisema,
“Ewe mtakatifu, uliyeko na uliyekuwako!
Wewe umetenda sawa kuhukumu mambo hayo.
6Maana waliimwaga damu ya watu wa Mungu na manabii,
nawe umewapa damu wainywe;
wamestahili hivyo!”
7Kisha, nikasikia sauti madhabahuni ikisema, “Naam, Bwana Mungu Mwenye Nguvu! Hukumu zako ni za kweli na haki!”
8Kisha malaika wa nne akamwaga bakuli lake juu ya jua. Jua likapewa nguvu ya kuwachoma watu kwa moto wake.
9Basi, watu wakaunguzwa vibaya sana; wakamtukana Mungu aliye na uwezo juu ya mabaa hayo. Lakini hawakutubu na kumtukuza Mungu.
10Kisha, malaika wa tano akamwaga bakuli lake juu ya makao makuu ya yule mnyama. Giza likauvamia utawala wake, watu wakauma ndimi zao kwa sababu ya maumivu,
11wakamtukana Mungu wa mbinguni kwa sababu ya maumivu yao na madonda yao. Lakini hawakutubu matendo yao mabaya.
12Kisha, malaika wa sita akamwaga bakuli lake juu ya mto mkubwa uitwao Eufrate. Maji yake yakakauka, na hivyo njia ikawekwa kwa ajili ya wafalme kutoka mashariki.
13Kisha, nikaona pepo wabaya watatu walio kama vyura, wakitoka kinywani mwa yule joka, kinywani mwa yule mnyama na kinywani mwa yule nabii wa uongo.[#16:13 Kutajwa kwa mojawapo ya mabaa au mapigo ya kule Misri (Kut 7:25—8:10).; #16:13 Joka na mnyama ni wale waliotajwa katika Ufu 12 na 13:1-10. Nabii wa uongo: Tazama 13:11-12.]
14Hawa ndio roho za pepo wafanyao miujiza. Ndio wanaokwenda kwa wafalme wa ulimwengu wote na kuwakusanya pamoja kwa ajili ya vita ya ile siku kubwa ya Mungu Mwenye Nguvu.
15“Sikiliza! Mimi naja kama mwizi! Heri mtu akeshaye na kuvaa nguo zake ili asije akaenda uchi huko na huko na kuaibika hadharani.”[#16:15 Ufu 3:3. Rejea Mat 24:42-44 Luka 12:39-40; na pia 1Thes 5:2-3. Simulizi linakatizwa kidogo ili kutoa ujumbe wa Yesu.]
16Basi, roho hao wakawakusanya hao wafalme mahali paitwapo kwa Kiebrania Harmagedoni.[#16:16 Ni hapa tu katika Biblia yote jina hili linatajwa. Kiebrania maana yake ni mlima (au sehemu za mlima) wa Megido. Jina hilo lagusia mapigano ya mwisho ambayo yatafanyika bondeni Megido, bonde ambalo laitwa pia Yezreeli ambalo kulifanyika mapigano mengi (Rejea Amu 5:19; 6:33—7:22; 2Fal 9:27; 23:29-30; Zek 12:11).]
17Kisha, malaika wa saba akamwaga bakuli lake hewani. Sauti kubwa ikasikika kutoka kwenye kiti cha enzi, hekaluni, ikisema, “Imetendeka!”
18Kukatokea umeme, kelele, ngurumo na tetemeko kubwa la ardhi ambalo halijapata kutokea tangu Mungu alipomuumba mtu.[#16:18 Hayo ni matukio ambayo yalitangulia na kufuata pia tarumbeta ya saba (Ufu 11:13,19).]
19Mji ule mkuu ukapasuliwa sehemu tatu, nayo miji ya mataifa ikateketea. Babuloni, mji mkuu, haukusahauliwa na Mungu. Aliunywesha kikombe cha divai ya ghadhabu ya hasira yake.[#16:19 Yaani, Babuloni. Wengine wanafikiri ni Roma, mji mkuu wa himaya ya Waroma unaotajwa kwa mfano kwa jina Babuloni (taz Ufu 14:8).; #16:19 Ufu 14:10; rejea Isa 51:17; Yer 25:15.]
20Visiwa vyote vikatoweka, nayo milima haikuonekena tena.
21Mvua ya mawe makubwa yenye uzito wa kama kilo hamsini kila moja, ikawanyeshea watu. Nao wakamtukana Mungu kwa sababu ya mapigo ya mvua hiyo ya mawe. Naam, pigo la mvua hiyo ya mawe lilikuwa kubwa mno.[#16:21 Neno kwa neno: talanta moja.]