Ufunuo 17

Ufunuo 17

Mzinzi mkuu

1Mmoja wa wale malaika saba waliokuwa na bakuli akaja, akaniambia, “Njoo, nami nitakuonesha adhabu aliyopewa yule mzinzi mkuu, mji ule uliojengwa juu ya maji mengi.[#17:1—21:1 Sehemu hii ya sita kwa mfululizo wa maono tunasimuliwa hukumu ya Mungu dhidi ya Babuloni mfano wa himaya ya Waroma, dhidi ya adui Shetani.; #17:1 Tazama Ufu 2:14. Yahusu “Babuloni” yaani “Roma”.; #17:1 Tazama aya 15; picha hiyo imetolewa kutoka Yer 51:13, nayo yaafiki mji wa Babuloni na sio mji wa Roma hasa. Babuloni ulikuwa umejengwa mahali ambapo matawi mawili ya mto Eufrate yalikutana.]

2Wafalme wa dunia wamefanya uzinzi pamoja naye; na wakazi wa dunia wamelewa divai ya uzinzi wake.”[#17:2 Yer 51:7; taz Ufu 14:8.]

3Kisha, nikakumbwa na Roho mpaka jangwani. Huko nikamwona mwanamke ameketi juu ya mnyama mwekundu. Mnyama huyo alikuwa ameandikwa kila mahali majina ya makufuru; alikuwa na vichwa saba na pembe kumi.[#17:3 Tazama Ufu 1:10; 4:2; 21:10; Yohane anaeleza hali ya kupoteza kujisikia hata mtu anaona vitu visivyo kawaida, (taz pia Eze 37:1; 2Kor 12:1-3).; #17:3 Ni yuleyule wa Ufu 13:1 pamoja na vichwa vyake saba na pembe kumi, picha ambayo huenda ni mfano wa himaya ya Waroma na ibada yake ya miungu ya uongo. Mwanamke hapa ni mji wa Roma. Majina ya kufuru yaweza kuwa majina ya sifa waliyopewa wafalme wa Roma.]

4Mwanamke huyo alikuwa amevaa vazi la rangi ya zambarau na nyekundu; alikuwa amejipamba kwa dhahabu, mawe ya thamani na lulu. Mkononi mwake alishika kikombe cha dhahabu ambacho kilikuwa kimejaa machukizo na mambo machafu yanayoonesha uzinzi wake.

5Alikuwa ameandikwa juu ya paji la uso wake jina la fumbo “Babuloni mkuu, mama wa wazinzi na wa mambo yote ya kuchukiza sana duniani.”

6Nikamwona huyo mwanamke amelewa damu ya watu wa Mungu, na damu ya watu waliouawa kwa sababu ya kumshuhudia Yesu.[#17:6 Baadhi ya wakuu wa Roma walisababisha vifo vya Wakristo wengi.]

Nilipomwona nilishangaa mno.

7Lakini malaika akaniambia, “Kwa nini unashangaa? Mimi nitakuambia maana iliyofichika ya mwanamke huyu na mnyama huyo amchukuaye ambaye ana vichwa saba na pembe kumi.

8Huyo mnyama uliyemwona, alikuwa hai hapo awali lakini sasa amekufa. Hata hivyo, karibu sana atapanda kutoka shimoni kuzimu, lakini ataangamizwa. Wanaoishi duniani watashangaa; naam, watu wote ambao majina yao hayakupata kuandikwa katika kitabu cha uhai tangu mwanzo wa ulimwengu, watashangaa kumwona huyo mnyama ambaye hapo awali aliishi, kisha akafa na sasa anatokea tena![#17:8 Ufu 3:5; rejea Ufu 13:8.]

9“Hapa panahitaji akili na hekima! Hivyo vichwa saba ni vilima saba ambavyo huyo mwanamke anaketi juu yake. Vichwa hivyo pia ni wafalme saba.[#17:9 Mji wa Roma ulikuwa unajulikana kama uliojengwa juu ya vilima saba (taz pia 17:18).; #17:9 Inaaminiwa kwa jumla kwamba hao saba ni wafalme wa kweli wa Roma ambao walitawala mmoja baada ya mwingine lakini hakuna maafikiano walikuwa akina nani.]

10Kati ya hao wafalme saba, watano wamekwisha angamia, mmoja anatawala bado na yule mwingine bado hajafika; na atakapofika atabaki kwa muda mfupi.

11Huyo mnyama ambaye alikuwa anaishi hapo awali lakini sasa haishi tena ni mfalme wa nane, naye pia ni miongoni mwa hao saba, na anakwenda zake kuharibiwa.[#17:9-11 Si rahisi kufafanua lugha hii ya mfano. Labda vichwa, wafalme saba vinawakilisha wafalme wakuu wa himaya ya Roma, hata hivyo haijulikani hao walikuwa akina nani.]

12“Zile pembe kumi ulizoziona ni wafalme ambao bado hawajaanza kutawala. Lakini watapewa mamlaka ya kutawala kwa muda wa saa moja pamoja na yule mnyama.[#17:12 Rejea Dan 7:7,23-24. Muda huo mfupi (saa moja) unaonesha kutoweka ghafla kwa nguvu zote zinazopingana na Mwanakondoo (aya 14).]

13Shabaha ya hawa kumi ni moja, na watampa yule mnyama nguvu na mamlaka yao yote.

14Watapigana na Mwanakondoo, lakini Mwanakondoo pamoja na wale aliowaita na kuwachagua ambao ni waaminifu, atawashinda kwa sababu yeye ni Bwana wa mabwana na Mfalme wa wafalme.”[#17:14 Kwa mara ya kwanza Yesu anapewa cheo kama kile cha Mungu Baba taz Kumb 10:17; Zab 136:2,3; Ling Kut 15:3,11; Zab 47:2; 82; Dan 2:47; 1Tim 6:15.]

15Malaika akaniambia pia, “Yale maji uliyoyaona pale alipokaa yule mzinzi: ni makundi ya watu wa kila taifa, rangi na lugha.[#17:15 Kwa picha hii, taz 17:1.]

16Pembe zile kumi ulizoziona na yule mnyama watamchukia huyo mzinzi. Watachukua kila kitu alicho nacho na kumwacha uchi; watakula nyama yake na kumteketeza kwa moto.

17Maana Mungu ametia mioyoni mwao nia ya kutekeleza shabaha yake, yaani wakubaliane wao kwa wao na kumpa huyo mnyama mamlaka yao ya kutawala, mpaka hapo yale aliyosema Mungu yatakapotimia.

18“Na yule mwanamke uliyemwona ndio ule mji mkuu ulio na mamlaka juu ya wafalme wa dunia.”[#17:18 Maelezo haya yanaafiki himaya ya Roma ambayo iligeuka kuwa mfano kamili wa nguvu za kibinadamu zilizo adui ya Mungu (taz Ufu 14:8).]

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania