The chat will start when you send the first message.
1Baada ya hayo nikasikia kitu kama sauti kubwa ya umati wa watu wengi mbinguni ikisema, “Asifiwe Mungu! Ukombozi, utukufu na nguvu ni mali yake Mungu wetu![#19:1 Ufu 7:9-10. Mwito huu wa kumsifu Mungu (Haleluya) ulikuwa mojawapo ya viitikio vya ibada ambavyo vinatumiwa pia katika Zaburi (rejea Zab 104:35; n.k.) Aidha mwito huo ulikuwa tamko la furaha la kumsifu Mungu.]
2Maana hukumu yake ni ya kweli na ya haki. Amemhukumu yule mzinzi mkuu ambaye alikuwa ameipotosha dunia kwa uzinzi wake. Amemwadhibu kwa sababu ya kumwaga damu ya watumishi wake!”
3Wakasema, “Asifiwe Mungu! Moshi wa moto unaoteketeza mji huo utapanda juu milele na milele!”
4Na wale wazee ishirini na wanne, na wale viumbe hai wanne, wakajitupa chini, wakamwabudu Mungu aliyeketi juu ya kiti cha enzi wakisema, “Amina! Asifiwe Mungu!”[#19:4 Ufu 4:3-6, 9-10. Kuhusu “Amina”: taz 1:6 maelezo.]
5Kisha, kukatokea sauti kwenye kiti cha enzi: “Msifuni Mungu enyi watumishi wake wote, nyote mnaomcha, wadogo kwa wakubwa.”
6Kisha nikasikia kitu kama sauti ya umati mkubwa wa watu na sauti ya maji mengi na ya ngurumo kubwa, ikisema, “Asifiwe Mungu! Maana Bwana Mungu wetu Mwenye Nguvu ametawala!
7Tufurahi na kushangilia; tumtukuze, kwani wakati wa harusi ya Mwanakondoo umefika, na bibi arusi yuko tayari.[#19:7 Iliaminika kwamba karamu au sikukuu ya furaha (aya 9) ingezindua utawala wa Masiha: taz Mat 8:11; 22:2-9; 25:10; Luka 13:29; 14:15-17. Hapa bibi harusi ni Kanisa na harusi hiyo ni muungano mkamilifu kati ya Kristo na Kanisa.; #19:7-8 Agano la Kale mara kwa mara hutumia lugha ya mfano ambayo Israeli ni kama mchumba wa Mwenyezi-Mungu (Isa 54:5-6; 62:5; Yer 2:2; Eze 16); katika A.J. wazo hili linatumika kueleza uhusiano uliopo kati ya Kristo na Kanisa: 2Kor 11:2; Efe 5:23-32; na katika Ufu 21:9-10 mchumba wa Mwanakondoo ni Yerusalemu Mpya.]
8Amepewa uwezo wa kujivalia nguo ya kitani safi, iliyotakata na yenye kung'aa!” (Nguo hiyo ya kitani safi ni matendo mema ya watakatifu).[#19:8 Rejea Isa 52:1; Zek 3:4-5.]
9Kisha malaika akaniambia, “Andika haya: Heri wale walioalikwa kwenye karamu ya harusi ya Mwanakondoo!” Tena akaniambia, “Hayo ni maneno ya kweli ya Mungu.”[#19:9 Mara ya nne (taz Ufu 1:3).]
10Basi, mimi nikaanguka kifudifudi mbele ya miguu yake, nikataka kumwabudu. Lakini yeye akaniambia, “Acha! Mimi ni mtumishi tu kama wewe na ndugu zako; sote tunamshuhudia Yesu. Mwabudu Mungu! Maana ushuhuda wa Yesu ndio unaowaangazia manabii.”[#19:10 Au: Ni ushuhuda anaotoa Yesu, au ni ujumbe unaotolewa juu yake Yesu. Taz 1:2 maelezo.]
11Kisha, nikaona mbingu zimefunguliwa; na huko alikuwako farasi mmoja mweupe, na mpandafarasi wake aliitwa “Mwaminifu” na “Kweli”. Huyo huhukumu na kupigana kwa ajili ya haki.[#19:11 Taz Eze 1:1 na Ufu 4:1.; #19:11 Haya ni majina ya sifa ya Kristo (taz 3:14; rejea Yoh 1:17). Taz pia 3:14 maelezo.; #19:11 Zab 96:13; Isa 9:6-7; 11:1-5.]
12Macho yake ni kama mwali wa moto, na alikuwa amevaa taji nyingi kichwani. Alikuwa ameandikwa jina ambalo hakuna mtu alijuaye isipokuwa tu yeye mwenyewe.
13Alikuwa amevaa vazi lililokuwa limelowekwa katika damu. Na jina lake huyo ni “Neno la Mungu”.[#19:13 Kulingana na wengi wa wafafanuzi wa Maandiko Matakatifu yahusu damu ya wale ambao ni adui waliouawa na Kristo.; #19:13 Rejea Yoh 1:1,14.]
14Majeshi ya mbinguni yalimfuata yakiwa yamepanda farasi weupe na yamevaa mavazi ya kitani, meupe na safi.
15Upanga mkali hutoka kinywani mwake, na kwa upanga huo atawashinda watu wa mataifa. Yeye ndiye atakayetawala kwa fimbo ya chuma na kuikamua divai katika chombo cha kukamulia zabibu za ghadhabu kuu ya Mungu Mwenye Nguvu.[#19:15 Ufu 1:16. “Upanga mkali hutoka kinywani mwake”: Mfano wa neno la mfalme mshindi (aya 13; rejea Isa 49:2; Ebr 4:12).; #19:15 Taz 2:27-28; 12:5; rejea Zab 2:9. Katika mataifa mbalimbali huko Mashariki ya Kati mfalme alipotawazwa alipewa fimbo ya chuma alama ya kuonesha kuwa ana uweza wa kuwaponda adui zake.; #19:15 Taz 14:19-20; rejea Isa 63:3; Omb 1:5; Yoeli 3:13.]
16Juu ya vazi lake, na juu ya paja lake, alikuwa ameandikwa jina: “Mfalme wa wafalme na Bwana wa mabwana.”[#19:16 Ufu 17:14; rejea Kumb 10:17; Zab 136:2,3.]
17Kisha, nikamwona malaika mmoja amesimama katika jua. Akapaza sauti na kuwaambia ndege wote waliokuwa wanaruka juu angani, “Njoni! Kusanyikeni pamoja kwa karamu kuu ya Mungu.
18Njoni mkaitafune miili ya wafalme, ya majemadari, ya watu wenye nguvu, ya farasi na wapandafarasi wao; njoni mkaitafune miili ya watu wote: walio huru na watumwa, wadogo na wakubwa.”
19Kisha, nikaona yule mnyama pamoja na mfalme wa dunia na askari wao wamekusanyika pamoja kusudi wapigane na yule aliyekuwa ameketi juu ya farasi pamoja na jeshi lake.
20Lakini huyo mnyama akachukuliwa mateka pamoja na nabii wa uongo aliyekuwa akifanya miujiza mbele yake. (Kwa miujiza hiyo, alikuwa amewapotosha wale waliokuwa na chapa ya huyo mnyama, na ambao walikuwa wameiabudu sanamu yake). Huyo mnyama pamoja na huyo nabii walitupwa wote wawili, wakiwa wazimawazima, ndani ya ziwa linalowaka moto wa madini ya kiberiti.[#19:20 Rejea 13:11-17.; #19:20 Au: “Ziwa liwakalo moto mkali wa kiberiti”. Ni sawa na kuzimu (20:1-3). Rejea Ufu 20:10; 21:8; tazama Ufu 9:17 maelezo.]
21Majeshi yao yaliuawa kwa upanga uliotoka kinywani mwa yule anayepanda farasi. Ndege wote wakajishibisha kwa nyama zao.