The chat will start when you send the first message.
1Kisha, nikamwona malaika mmoja anashuka kutoka mbinguni akiwa na ufunguo wa kuzimu na mnyororo mkubwa mkononi mwake.[#20:1 Taz Ufu 9:1 maelezo.]
2Akalikamata lile joka — nyoka wa kale, yaani Ibilisi au Shetani — akalifunga kwa muda wa miaka 1,000.[#20:2 Taz 12:9; rejea Mwa 3:1-5.; #20:2 Muda ambao hautajwi mahali pengine. Umefafanuliwa kwa namna kadha wa kadha; labda wasomaji wa kwanza wa kitabu hiki waliona katika tarakimu hiyo kama vile katika nyingine, kuwa mfano wa kitu fulani; hapa yahusu muhula maalumu mkamilifu (10x10x10) ambao unaonesha ushindi kamili wa Mungu dhidi ya Shetani.]
3Malaika akalitupa kuzimu, akaufunga mlango wa kuingilia huko na kuutia mhuri ili lisiweze tena kuyapotosha mataifa mpaka hapo miaka 1,000 itakapotimia. Lakini baada ya miaka hiyo ni lazima lifunguliwe tena, lakini kwa muda mfupi tu.
4Kisha nikaona viti vya enzi na watu walioketi juu yake; watu hao walipewa mamlaka ya hukumu. Niliona pia roho za wale waliokuwa wamenyongwa kwa sababu ya kumshuhudia Yesu na kwa sababu ya neno la Mungu. Hawa hawakumwabudu yule mnyama na sanamu yake, wala hawakupigwa alama yake juu ya paji za nyuso zao, au juu ya mikono yao. Walipata tena uhai, wakatawala pamoja na Kristo kwa miaka 1,000.[#20:4 Rejea Dan 7:9,22,27; Mat 19:28; Luka 22:30. Yahusu utawala wa mashahidi hao pamoja na Kristo (taz Ufu 6:9-10).]
5(Wale wengine waliokufa hawakupata uhai mpaka miaka 1,000 itimie). Huu ndio ufufuo wa kwanza.
6Wameneemeka sana, tena heri yao wote wanaoshiriki ufufuo huu wa kwanza. Kifo cha pili hakitakuwa na nguvu juu yao; watakuwa makuhani wa Mungu na wa Kristo, na watatawala pamoja naye kwa miaka 1,000.[#20:6 Mara ya sita katika kitabu hiki. Taz maelezo ya 1:3.; #20:6 Tazama Ufu 2:11. Kifo cha kwanza ni kifo cha mwili, na cha pili ni kifo cha kiroho cha milele.; #20:6 Ufu 1:6; 5:10; rejea 1Pet 2:5,9.]
7Wakati miaka 1,000 itakapotimia, Shetani atafunguliwa kutoka gerezani mwake.
8Basi, atatoka nje, ataanza kuyapotosha mataifa yote yaliyotawanyika kila mahali duniani, yaani Gogu na Magogu. Shetani atawakusanya pamoja kwa ajili ya vita; nao watakuwa wengi kama mchanga wa pwani.[#20:8 Maneno haya mawili yametolewa kwa Eze 38—39; hapa yahusu majina ya mataifa adui kwa jumla.]
9Walipita katika nchi yote, wakaizunguka kambi ya watakatifu na mji wa Mungu aupendao. Lakini moto ulishuka kutoka mbinguni, ukawaangamiza.
10Naye Ibilisi aliyekuwa anawapotosha, akatupwa ndani ya ziwa linalowaka madini ya kiberiti, walimo yule mnyama na yule nabii wa uongo, nao watateswa mchana na usiku, milele na milele.[#20:10 Taz Ufu 9:17 maelezo; rejea 21:8 na pia Mat 25:41.]
11Kisha, nikaona kiti cha enzi kikubwa cheupe, na yule aketiye juu yake. Dunia na mbingu vikatoweka mbele ya macho yake, na havikuonekana tena.
12Kisha nikawaona watu wakubwa na wadogo, wamesimama mbele ya kiti cha enzi, na vitabu vikafunguliwa. Halafu kitabu kingine, yaani kitabu cha uhai, kikafunguliwa pia. Wafu wakahukumiwa kadiri ya matendo yao, kama ilivyoandikwa ndani ya vitabu hivyo.[#20:12 Aya 15; taz Ufu 3:5 maelezo.]
13Bahari ikawatoa nje wafu waliokuwa ndani yake; Kifo na Kuzimu vikawatoa nje wafu waliokuwa ndani yao. Kila mmoja akahukumiwa kufuatana na matendo yake.
14Kisha Kifo na Kuzimu vikatupwa ndani ya ziwa la moto. Ziwa hili la moto ndicho kifo cha pili.[#20:14 Rejea I Kor 15:26.; #20:14 Taz 2:11; rejea Ufu 21:8 na pia Mat 10:28; 25:41.]
15Mtu yeyote ambaye jina lake halikupatikana limeandikwa katika kitabu cha uhai, alitupwa katika ziwa la moto.