Ufunuo 21

Ufunuo 21

Mbingu mpya na dunia mpya

1Kisha, nikaona mbingu mpya na dunia mpya. Mbingu ile ya kwanza na dunia ile ya kwanza vilikuwa vimetoweka, nayo bahari pia haikuwako tena.[#21:1 Maono haya yanamalizia sehemu iliyosimulia juu ya hukumu ya Mungu (17:1—21:1) na inatayarisha sehemu ifuatayo ambayo ni ya mwisho (21:2—22:5). Mbingu mpya na dunia mpya: Isa 65:17; 66:22; 2Pet 3:13; rejea Mwa 1:1.]

2Nikaona mji mtakatifu, Yerusalemu mpya, ukishuka kutoka kwa Mungu mbinguni. Ulikuwa umetayarishwa vizuri kama bibi arusi aliyepambwa tayari kukutana na mumewe.[#21:2—22:5 Kitabu cha Ufunuo kinamalizia kwa Maono ya Yerusalemu mpya inayokuja kutoka mbinguni. Picha tunayopewa ya mji huo inachanganywa na maelezo au picha za bibi harusi kueleza uhusiano kamili kati ya Mungu na Mwanakondoo pamoja na watu wake. Angalia jinsi Yerusalemu Mpya ilivyo kinyume cha mji wa Babuloni (sura za 17 na 18).; #21:2 Isa 52:1.; #21:2 Taz 3:12; rejea Gal 4:26; Fil 3:20; Ebr 12:22.]

3Kisha nikasikia sauti kubwa kutoka katika kiti cha enzi ikisema, “Tazama! Maskani ya Mungu kati ya watu. Atakaa kati yao, nao watakuwa watu wake, naye atakuwa Mungu wao.[#21:3 Kwa mara ya mwisho agano la Mungu la milele na masharti yake na watu wake linarudiwa rasmi (taz Kut 19:4-6; Lawi 26:12; Yer 31:31-34; Eze 37:27; 2Kor 6:16; Ebr 8:8-12).]

4Yeye atayafuta machozi yao yote; maana kifo hakitakuwako tena, wala uchungu, wala kilio, wala maumivu; maana ile hali ya kale imepita!”

5Kisha yule aliyeketi juu ya kiti cha enzi akasema, “Tazama, nafanya yote mapya.” Tena akaniambia, “Andika jambo hili, maana maneno haya ni ya kuaminika na ya kweli!”

6Kisha akaniambia, “Yametimia! Mimi ni Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho. Aliye na kiu nitampa kinywaji cha bure kutoka katika chemchemi ya maji ya uhai.[#21:6 Taz 1:8.]

7Mshindi yeyote atapokea hicho, nami nitakuwa Mungu wake, naye atakuwa mwanangu.[#21:7 Neno ambalo lilitumika kumalizia kila moja ya barua kwa makanisa saba katika Ufu 2—3, na ambalo lamalizia pia hapa kitabu chote.]

8Lakini watu waoga, wasioamini, wapotovu, wauaji, wazinzi, wachawi, waabudu sanamu, na waongo wote, mahali pao patakuwa ndani ya lile ziwa linalowaka moto na madini ya kiberiti; hicho ndicho kifo cha pili.”[#21:8 Taz Rom 1:32 maelezo.]

Yerusalemu mpya

9Kisha mmoja wa wale malaika saba waliokuwa na yale mabakuli saba yaliyokuwa yamejaa mabaa saba ya mwisho, akaja na kuniambia, “Njoo! Nami nitakuonesha bibi arusi, mkewe Mwanakondoo!”[#21:9 Huyu ni Yerusalemu mpya na sio kama Ufu 19:7-8 ambapo ni watu wa Mungu.]

10Basi, Roho akanikumba, naye malaika akanipeleka juu ya mlima mrefu sana. Akanionesha mji mtakatifu, ukishuka kutoka kwa Mungu mbinguni,

11uking'aa kwa utukufu wa Mungu. Mwangaza wake ulikuwa kama wa jiwe la thamani kubwa kama yaspi, angavu kama kioo.

12Ulikuwa na ukuta mrefu na mkubwa, wenye milango kumi na miwili, na kila mmoja ulilindwa na malaika. Juu ya kila mlango paliandikwa mojawapo ya majina ya makabila kumi na mawili ya Israeli.

13Kila upande ulikuwa na milango mitatu: upande wa mashariki milango mitatu, kaskazini milango mitatu, kusini milango mitatu na magharibi milango mitatu.

14Kuta za mji huo zilikuwa zimejengwa juu ya mawe ya msingi kumi na mawili, na juu ya kila jiwe palikuwa pameandikwa mojawapo ya majina ya wale mitume kumi na wawili wa Mwanakondoo.[#21:14 Efe 2:20.]

15Basi, yule malaika aliyekuwa anasema nami alikuwa na kijiti cha dhahabu cha kupimia, kwa ajili ya kuupima huo mji, milango yake na kuta zake.[#21:15 Rejea Eze 40:3. Katika muundo na vipimo vya huo mji kuna vitu vingi ambavyo vina shabaha ya kusisitiza kwa mfano ukamilifu na usafi wa Yerusalemu mpya. Vipimo vyake vimezidishwa mara kumi na mbili (aya 12-14,16-17,19-21; taz Ufu 4:4).]

16Mji wenyewe ulikuwa wa mraba, upana na urefu wake sawa. Basi, malaika akaupima mji huo kwa kijiti chake: ulikuwa na urefu, upana na kimo cha kama kilomita 2,400.[#21:16 Au neno kwa neno: Stadia elfu mbili. Mji ulikuwa na msingi wake mraba, mfano wa ukamilifu.]

17Kisha akaupima ukuta wake pia; nao ulikuwa mita 60 kwa kipimo cha macho cha kibinadamu ambacho malaika alitumia.[#21:17 Yahusu kusikia ujumbe wa kitabu hiki cha Ufunuo kisomwapo.]

18Ukuta huo ulikuwa umejengwa kwa mawe mekundu ya thamani, na mji wenyewe ulikuwa umejengwa kwa dhahabu safi, angavu kama kioo.

19Mawe ya msingi wa ukuta huo yalikuwa yamepambwa kwa kila aina ya mawe ya thamani. Jiwe la kwanza la msingi lilikuwa jiwe la thamani jekundu, la pili johari ya rangi ya samawati, la tatu kalkedoni, la nne zumaridi,[#21:19-20 Rejea Isa 54:11-12. Mawe ya thamani kumi na mawili yanaafikiana kijumla na mawe yaliyovaliwa na kuhani kifuani (Kut 28:17-26; 39:10-13).]

20la tano sardoniki, la sita akiki, la saba krisolito, la nane zabarajadi, la tisa topazi, la kumi krisopraso, la kumi na moja yasintho, na la kumi na mbili amethisto.

21Na ile milango kumi na miwili ilikuwa lulu kumi na mbili; kila mlango ulikuwa umetengenezwa kwa lulu moja. Barabara kuu ya mji ilikuwa imetengenezwa kwa dhahabu safi, angavu kama kioo.

22Sikuona hekalu katika mji huo, maana Bwana Mungu Mwenye Nguvu na yule Mwanakondoo ndio hekalu lake.[#21:22 Eze 11:16. Katika Israeli ishara au alama ya kwamba Mungu alikuwako kati yao ilikuwa kuweko kwa hekalu. Katika Yerusalemu mpya hamna hekalu, kwani Mungu mwenyewe yupo, kadhalika naye Mwanakondoo, nao waumini wana fursa ya kwenda moja kwa moja kwa Mungu na kwa Mwanakondoo. Aidha hata lile hekalu la mbinguni (7:15) hapa limepitwa na wakati. Tazama Yoh 1:51 na rejea Yoh 2:19-21.]

23Mji huo hauhitaji jua wala mwezi kuuangazia, maana utukufu wa Mungu huuangazia, na taa yake ni yule Mwanakondoo.

24Watu wa mataifa watatembea katika mwanga wake na wafalme wa dunia watauletea utajiri wao.

25Milango ya mji huo itakuwa wazi mchana wote; maana hakutakuwa na usiku humo.

26Fahari na utajiri wa watu wa mataifa utaletwa humo ndani.

27Lakini hakuna chochote kilicho najisi kitakachoingia humo; wala mtu yeyote atendaye mambo ya kuchukiza au ya uongo hataingia humo. Ni wale tu walioandikwa katika kitabu cha uhai cha Mwanakondoo ndio watakaoingia ndani.[#21:27 Taz Ufu 3:5; 13:8; 17:8; rejea 20:12,15.]

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania