Ufunuo 22

Ufunuo 22

1Kisha malaika akanionesha mto wa maji ya uhai maangavu kama kioo, yakitoka kwenye kiti cha enzi cha Mungu na Mwanakondoo.[#22:1 Eze 47:1; Zek 14:8; rejea Mwa 2:10; Zab 46:4. Rejea pia Yoh 4:10,14. Katika maono ya Ezekieli mto huo ulitoka hekaluni. Lakini hapa unatoka kwenye kiti cha enzi cha Mungu na Mwanakondoo (taz 21:22). Taz Yoh 7:37-38.]

2Mto huo ulitiririka kupitia katikati ya barabara kuu ya mji. Kandokando ya mto huo kulikuwa na mti wa uhai unaozaa matunda mara kumi na mbili kwa mwaka, yaani kila mwezi; na majani yake ni dawa ya kuwaponya watu wa mataifa.[#22:2 Mwa 2:9; Ufu 2:7.]

3Hapana kitu chochote kilicholaaniwa kitakachokuwa katika mji huo.[#22:3 Mwa 3:17,22-24. Kwa sababu ya laana ya Mwanzo, watu walikatazwa na kuzuiliwa kuufikia mti wa uhai; katika Yerusalemu mpya, lakini, inawezekana sasa kuufikia. Rejea Zek 14:11 (Kigiriki cha Septuajinta - LXX) na Rom 8:20-21.]

Kiti cha enzi cha Mungu na cha Mwanakondoo kitakuwa katika mji huo, na watumishi wake watamwabudu.

4Watauona uso wake, na jina lake litaandikwa juu ya paji za nyuso zao.[#22:4 Jambo hili halikupata kamwe kutukia; Zab 17:15; Mat 5:8; 1Yoh 3:2.]

5Usiku hautakuwako tena, wala hawatahitaji mwanga wa taa au wa jua, maana Bwana Mungu atawaangazia, nao watatawala milele na milele.

Kuja kwa Yesu

6Kisha malaika akaniambia, “Maneno haya ni ya kweli na ya kuaminika. Bwana Mungu ambaye huwapa manabii Roho wake, alimtuma malaika wake awaoneshe watumishi wake mambo ambayo lazima yatukie punde.[#22:6-21 Kitabu kinamalizia na mfululizo wa maneno ya kutia moyo na matamshi mengine; mengine yamesemwa na malaika (aya 6, 9-11) mengine na Yesu mwenyewe (12-13,16, 20) na mengine ni dhahiri yanasemwa na mwandishi mwenyewe.]

7“Sikiliza! Naja upesi. Heri yake anayeyazingatia maneno ya unabii yaliyo katika kitabu hiki.”[#22:7 “Sikiliza! Naja upesi” (hapa na 22:12, 20; rejea Ufu 2:16; 3:11). “Heri” mara ya sita linatumiwa katika aya 7 (taz Ufu 1:3). Maneno haya yaweza kuwa yamesemwa na Yesu au na mwandishi.]

8Mimi Yohane, niliyaona na kusikia mambo haya. Nilipokwisha sikia na kuona, nikajitupa chini mbele ya miguu ya huyo malaika aliyenionesha mambo hayo, nikataka kumwabudu.

9Lakini yeye akaniambia, “Acha! Mimi ni mtumishi tu kama wewe na ndugu zako manabii na wote wanaoyatii maagizo yaliyomo katika kitabu hiki. Mwabudu Mungu!”

10Tena akaniambia, “Usiyafiche kama siri maneno ya unabii yaliyomo katika kitabu hiki, maana wakati wa kutimizwa kwake umekaribia.[#22:10 Neno kwa neno: Usiyafunge kwa mhuri; tofauti na Dan 8:26; 12:4,9.]

11Kwa sasa anayetenda mabaya na aendelee kutenda mabaya, na aliye mchafu aendelee kuwa mchafu. Mwenye kutenda mema na azidi kutenda mema, na aliye mtakatifu na azidi kuwa mtakatifu.”

12“Sikiliza!” Asema Yesu, “Naja upesi pamoja na tuzo nitakalompa kila mmoja kufuatana na matendo yake.[#22:12-13 Maneno ya Yesu.]

13Mimi ni Alfa na Omega, wa kwanza na wa mwisho, mwanzo na mwisho.”

14Heri yao wale wanaoosha mavazi yao, wapate kuwa na haki ya kula tunda la mti wa uhai, na haki ya kuingia mjini kwa kupitia milango yake.[#22:14]

15Lakini mbwa, wachawi, wazinzi, wauaji, waabudu sanamu na wote wanaopenda kusema uongo, watakaa nje ya mji.

16“Mimi, Yesu, nimemtuma malaika wangu awathibitishieni mambo haya katika makanisa. Mimi ni mzawa wa ukoo wa Daudi. Mimi ni nyota angavu ya asubuhi!”

17Roho na Bibi arusi waseme, “Njoo!” Kila mtu asikiaye hili, na aseme, “Njoo!” Aliye na kiu na aje; anayependa, na achukue maji ya uhai bila malipo.

Hatima

18Mimi Yohane nawapa onyo wote wanaosikia maneno ya unabii yaliyomo katika kitabu hiki: mtu yeyote akiongeza chochote katika mambo haya, Mungu atamwongezea mabaa yaliyoandikwa katika kitabu hiki.[#22:18-19 Yaani Ufunuo.]

19Na mtu yeyote akipunguza chochote katika maneno ya unabii yaliyomo katika kitabu hiki, Mungu atamnyang'anya sehemu yake katika ule mti wa uhai, na sehemu yake katika mji mtakatifu, ambavyo vimeelezwa katika kitabu hiki.

20Naye anayetoa ushahidi wake juu ya mambo haya asema: “Kweli naja upesi.”

Amina. Njoo Bwana Yesu!

21Nawatakieni nyote neema ya Bwana Yesu. Amina.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania