The chat will start when you send the first message.
1Baada ya hayo nilitazama nikaona mlango umefunguliwa mbinguni. Na ile sauti niliyoisikia pale awali ambayo ilikuwa kama sauti ya tarumbeta, ikasema, “Njoo hapa juu, nami nitakuonesha mambo yatakayotukia baadaye.”[#4:1 Picha yampa mwandishi fursa ya kuingia mbinguni kuona maono ya mambo ambayo budi yatukie punde. Picha za maono haya zimeelezwa kwa wingi kutoka kwa Eze 1 na 3; tazama pia Isa 6.; #4:1—8:1 Sura 4 na 5 zinatumika hapa kujenga na kutayarisha maono ya ile mihuri saba - 6:1—8:1. Sura ya nne aghalabu yahusu ibada kwa Mungu na ya tano ibada kwa Kristo.]
2Mara nikakumbwa na Roho. Kumbe, huko mbinguni kuna kiti cha enzi na juu yake ameketi mmoja.[#4:2 Taz maelezo ya 1:10.]
3Huyo aliyeketi juu yake alikuwa kama almasi na jiwe zuri jekundu. Upinde wa mvua ulikuwa unang'aa kama zumaridi na ulikizunguka kiti cha enzi pande zote.[#4:3 Mara nyingi mwandishi anaeleza uzuri wa watu au vitu kwa kulinganisha na mawe ya thamani. Neno almasi hapa ni Yaspi Kigiriki na mara nyingi katika lugha yetu si rahisi kupata majina halisi yanayopatana na mawe hayo. Hapa mwandishi anasema juu ya Mungu, bila kumtaja moja kwa moja ili kumweka katika hali yake ya kupita fikra za binadamu. Taz Eze 1:26-28; 10:1.; #4:3 Neno kwa neno: Karnelia.; #4:3 Jiwe la thamani, kwa kawaida ni la rangi ya kijani.]
4Kulikuwa na duara la viti ishirini na vinne kukizunguka kiti cha enzi, na juu ya viti hivyo wazee ishirini na wanne walikuwa wameketi wamevaa mavazi meupe na taji za dhahabu vichwani.[#4:4 Mwandishi anapendelea sana kutumia tarakimu zenye mifano ya vitu vingine kama vile tarakimu 12 n.k (taz 7:4-8). Hawa wazee ishirini na wanne wamekaa kana kwamba ni mahakama ya mbinguni, nao wanasimama mahali pa watu wote wa Mungu. Baadhi hufikiri kuwa ni malaika.]
5Umeme, sauti na ngurumo, vilikuwa vinatoka kwenye hicho kiti cha enzi. Taa saba za moto zilikuwa zinawaka mbele ya hicho kiti cha enzi. Taa hizo ni roho saba za Mungu.[#4:5 Picha ya mfano wa kutokea au kuweko kwake Mungu. Ufu8:5; 11:19; 16:18. Tazama pia kutokea kwake Mungu katika Kut 19:16; Eze 1:4.]
6Mbele ya kiti cha enzi kulikuwa na kitu kama bahari ya kioo, angavu kama jiwe ling'aalo sana.
Katika pande zote za hicho kiti cha enzi na kukizunguka, kulikuwa na viumbe hai wanne. Viumbe hao walikuwa wamejaa macho mbele na nyuma.
7Kiumbe wa kwanza alikuwa kama simba, wa pili kama ng'ombe, wa tatu alikuwa na sura ya mtu, na wa nne alikuwa kama tai anayeruka.
8Viumbe hao wanne walikuwa na mabawa sita kila mmoja, na walikuwa wamejaa macho, ndani na nje. Usiku na mchana, bila kupumzika, huimba:
“Mtakatifu, mtakatifu, mtakatifu,
Bwana, Mungu Mwenye Nguvu,
aliyekuwako, aliyeko na anayekuja!”
9Kila mara viumbe hao wanne walipomtukuza na kumheshimu na kumshukuru huyo aliyeketi juu ya kiti cha enzi ambaye anaishi milele na milele,
10wale wazee ishirini na wanne hujiangusha mbele ya huyo aliyeketi juu ya kiti cha enzi na kumwabudu huyo ambaye anaishi milele na milele; na huziweka taji zao mbele ya kiti cha enzi wakisema:
11“Wastahili ee Bwana na Mungu wetu,
kupokea utukufu na heshima na nguvu.
Maana wewe uliumba vitu vyote,
na kwa matakwa yako viliumbwa na vipo.”