The chat will start when you send the first message.
1Kisha nikaona kitabu katika mkono wa kulia wa huyo aliyeketi juu ya kiti cha enzi, nacho kilikuwa kimeandikwa ndani na nje na kufungwa kwa mihuri saba.[#5:1-4 Vitabu vya kale vilikuwa vya namna ya msokoto wa karatasi au ngozi iliyotengenezwa kwa namna fulani. Wafafanuzi wengi wa Biblia wanafikiri kitabu hicho ni mfano wa mipango yote ya Mungu kuhusu binadamu kama inavyoelezwa katika hayo matukio yanayofuata kufunguliwa kwa kila mhuri. Kuvunja hiyo mihuri ni kufanya mipango hiyo ya Mungu ifanyike.; #5:1 Taz Eze 2:9-3:3 na pia Isa 29:11 na Zek 5:1-4.]
2Tena nikamwona malaika mwenye nguvu akitangaza kwa sauti kubwa: “Nani anayestahili kuvunja hiyo mihuri na kukifungua kitabu hicho?”
3Lakini hakupatikana mtu yeyote mbinguni, wala duniani, wala chini kuzimu, aliyeweza kukifungua hicho kitabu au kukitazama ndani.
4Basi, mimi nikalia sana kwa sababu hakupatikana mtu aliyestahili kukifungua, au kukitazama ndani.
5Kisha mmoja wa wale wazee akaniambia, “Usilie! Tazama! Simba wa kabila la Yuda, chipukizi wa Daudi, ameshinda. Yeye anaweza kuivunja mihuri yake saba na kukifungua hicho kitabu.”[#5:5 Maneno ya kimfano yaliyotolewa kutoka Mwa 49:9-10 sehemu ambayo kadiri ya mapokeo yahusu Masiha. Katika maandishi ya Wayahudi ya wakati huo simba alitumika kama mfano wa Masiha, mshindi wa uovu.; #5:5 Maneno yanayorejea Isa 11:1,10; Ling Ufu 22:16. Kigiriki kina “mzizi wa Daudi” maneno ambayo ni jina la sifa la Masiha.; #5:5 “Yeye” ni yule “Mwanakondoo” wa aya 6. Yeye ndiye awezaye kujulisha matakwa ya Mungu kuhusu historia ya binadamu na kuyafanya matakwa yake Mungu yafikie lengo lake kamili (5:6). Mwanakondoo: Angalia Isa 53:7,10-12 na pia Yoh 1:29. Katika Ufunuo si jambo geni kukuta matumizi ya mfano fulani kwa kurejea mambo au maana zinazopingana au zilizo kinyume cha mambo, simba - Mwanakondoo. Mwanakondoo aliyechinjwa ni mfano wa Kristo ambaye alishinda kutoka mateso yake na kifo. Ling Luka 24:26; Mate 8:32-35; 1Pet 1:18-19.]
6Kisha nikaona pale katikati ya kiti cha enzi Mwanakondoo amesimama, akizungukwa kila upande na wale viumbe hai wanne, na wale wazee. Huyo Mwanakondoo alionekana kana kwamba amechinjwa. Alikuwa na pembe saba na macho saba ambayo ni roho saba za Mungu zilizokuwa zimepelekwa kila mahali duniani.[#5:6 Pembe ni ishara au mfano wa nguvu na uwezo (Kumb 33:17 na makala ya Kiebrania ya Zab 18:2; 112:9. Pembe saba zinamaanisha uwezo au nguvu kamili za Kristo Mwanakondoo (ling Mat 28:18; 1Kor 1:24). Kuhusu picha ya macho saba ambayo yanatajwa hapa kama roho saba za Mungu, aghalabu maneno hayo yanasisitiza uwezo wa Mungu wa kuona na kujua kila kitu (taz 1:4).]
7Mwanakondoo akaenda, akakitwaa hicho kitabu kutoka mkono wa kulia wa yule aliyeketi juu ya kiti cha enzi.
8Mara tu alipokwisha twaa hicho kitabu, wale viumbe hai wanne pamoja na wale wazee ishirini na wanne walianguka kifudifudi mbele ya Mwanakondoo. Kila mmoja alikuwa na kinubi na bakuli za dhahabu zilizojaa ubani, ambao ni sala za watu wa Mungu.[#5:8 Kitu kinachotoa harufu nzuri kinapochomwa na mara kwa mara kinamaanisha sala za watu wa Mungu.]
9Basi, wakaimba wimbo huu mpya:
“Wewe wastahili kukitwaa hicho kitabu
na kuivunja mihuri yake.
Kwa sababu wewe umechinjwa,
na kwa damu yako umemnunulia Mungu wetu
watu kutoka kila kabila, lugha, jamaa na taifa.
10Umewafanya ufalme wa makuhani wamtumikie Mungu wetu,[#5:10 Ufu 20:6; 22:5.]
nao watatawala duniani.”
11Kisha nikatazama, nikasikia sauti ya malaika wengi sana, idadi isiyohesabika, maelfu na maelfu. Walikuwa wamekaa kuzunguka kiti cha enzi, wale viumbe hai wanne na wale wazee;
12wakasema kwa sauti kuu:
“Mwanakondoo aliyechinjwa anastahili kupokea
uwezo, utajiri, hekima, nguvu, utukufu na sifa.”
13Nikasikia viumbe vyote mbinguni, duniani, chini ya dunia na baharini — viumbe vyote ulimwenguni — vikisema:
“Kwake yeye aketiye katika kiti cha enzi,
na kwa Mwanakondoo,
iwe sifa na heshima na utukufu na enzi,
milele na milele.”
14Na wale viumbe hai wanne wakasema, “Amina!” Na wale wazee wakaanguka kifudifudi, wakaabudu.[#5:14 Taz Ufu 1:6 maelezo.]