Ufunuo 6

Ufunuo 6

Mwanakondoo anaivunja mihuri

1Kisha, nikamwona Mwanakondoo anavunja mhuri mmojawapo wa ile mihuri saba. Nikasikia mmoja wa wale viumbe hai wanne akisema kwa sauti kama ya ngurumo, “Njoo!”[#6:1—8:1 Sehemu inayoeleza juu ya kufunguliwa mihuri saba ya kile kitabu. Ukuu wa Kristo umekwisha sisitizwa na upeo wa uwezo na ukuu wake utatajwa tena baada ya tarumbeta ya saba (11:15-16) na tena baada ya umwagaji wa bakuli lile la saba (16-17).]

2Mimi nikatazama, na kumbe palikuwa na farasi mmoja mweupe hapo. Na mpandafarasi wake alikuwa na upinde, akapewa na taji. Basi, akatoka kama mshindi, aendelee kushinda.[#6:1-2 Zingatia matumizi ya kimfano kuhusu rangi nyeupe kama ilivyo katika 2:17 na 3:4 na kufanana kwa matumizi hayo na 19:11. Ushindi hapa ni wa Kristo mwenyewe (5:5). Wengine, kwa kufikiria farasi wote saba wanafafanua hapa kwamba wao ni jeshi la kuangamiza.]

3Kisha, Mwanakondoo akavunja mhuri wa pili. Nikamsikia yule kiumbe hai wa pili akisema, “Njoo!”

4Nami nikatazama na kumbe palikuwapo farasi mwingine hapo, mwekundu. Mpandafarasi wake alikabidhiwa jukumu la kuondoa amani duniani, watu wauane, naye akapewa upanga mkubwa.[#6:3-4 Mfano wa vita na mauaji.]

5Kisha Mwanakondoo akavunja mhuri wa tatu. Nikamsikia yule kiumbe hai wa tatu akisema, “Njoo!” Nikatazama na kumbe palikuwapo farasi mmoja hapo, mweusi. Mpandafarasi wake alikuwa na vipimo viwili vya kupimia uzito mkononi mwake.[#6:5-6 Mfano wa njaa inayofuata vita na umwagaji damu vipimo vinavyotajwa ni kwa ajili ya kukazia ukali wa njaa.]

6Nikasikia kitu kama sauti itokayo kwa wale viumbe hai wanne. Nayo ilisema, “Kibaba kimoja cha unga wa ngano kwa kiasi cha fedha denari moja, na vibaba vitatu vya shayiri kwa denari moja. Lakini usiharibu mafuta wala divai!”

7Kisha, Mwanakondoo akavunja mhuri wa nne. Nikamsikia yule kiumbe hai wa nne akisema, “Njoo!”

8Nami nikatazama, na kumbe alikuwapo farasi mmoja hapo, rangi yake kijivu. Na jina la mpandafarasi wake lilikuwa Kifo, na Kuzimu alimfuata nyuma. Hao walipewa mamlaka juu ya robo moja ya dunia, wawaue watu kwa upanga, njaa, tauni na kwa wanyama wakali wa dunia.[#6:7-8 Rangi kijivu mfano wa kifo; ling Eze 14:21.]

9Kisha, Mwanakondoo akavunja mhuri wa tano. Nikaona pale chini ya madhabahu ya kufukizia ubani roho za wale waliouawa kwa sababu ya ujumbe wa Mungu, na kwa sababu ya ushuhuda waliotoa.[#6:9-11 Unapovunjwa panasikika maombolezo au malalamiko ya wale waliouawa kwa sababu ya imani yao na huduma zao za kumshuhudia huyo Mwanakondoo (Zab 79:5-10). Labda yahusu mashahidi wa dini wakati wa enzi ya Domisiano (yapata mwaka 81-96 B.K.).; #6:9 Damu ya kafara ilinyunyizwa pembeni mwa madhabahu. Kwa kuwaweka hao roho hapo mwandishi alitaka kusema kwamba kifo cha hao kilikuwa kama tambiko au kafara iliyokubalika kwa Mungu (ling Fil 2:17; 2Tim 4:6).]

10Basi, wakalia kwa sauti kubwa: “Ee Bwana, uliye mtakatifu na mwaminifu, mpaka lini utakawia kulipiza kisasi kwa wakazi wote wa dunia kwa ajili ya kuuawa kwetu?”

11Wakapewa kila mmoja vazi refu jeupe, wakaambiwa wazidi kusubiri kwa muda mfupi, mpaka itakapotimia idadi ya watumishi wenzao na ndugu ambao watauawa kama wao wenyewe walivyouawa.[#6:11 Taz maelezo ya 3:4.]

12Kisha nikatazama, na wakati Mwanakondoo alipouvunja mhuri wa sita, kukawa na tetemeko kubwa la ardhi; jua likawa jeusi kama gunia la manyoya; mwezi wote ukawa mwekundu kama damu;[#6:12 Kuvunjwa mhuri huo kunaleta maangamizi ya dunia nzima.; #6:12 Ling Isa 13:10; Yoe 2:10; 2:31; 3:15; Mat 24:29 na sambamba zake katika Injili.; #6:12 Taz Yoe 2:31; 3:15.]

13nazo nyota za mbingu zikaanguka juu ya ardhi kama matunda ya mtini yasiyokomaa yaangukavyo wakati mti wake unapotikiswa na upepo mkali.

14Anga likatoweka kama vile karatasi inavyokunjwakunjwa; milima yote na visima vyote vikaondolewa mahali pake.[#6:13-14 Taz Isa 34:4.; #6:14 Taz 16:20]

15Kisha, wafalme wa duniani, wakuu, majemadari, matajiri, wenye nguvu, kila mtumwa na mtu huru, wakajificha mapangoni na kwenye miamba milimani.

16Wakaiambia hiyo milima na hayo majabali, “Tuangukieni, mkatufiche mbali na yeye aketiye juu ya kiti cha enzi, na mbali na ghadhabu ya Mwanakondoo!

17Maana siku maalumu ya ghadhabu yao imefika. Nani awezaye kuikabili?”

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania