The chat will start when you send the first message.
1Sisi tulio imara katika imani tunapaswa kuwasaidia wale walio dhaifu wayakabili matatizo yao. Tusijipendelee sisi wenyewe tu.[#15:1 Naye Paulo anajihesabu kati ya waamini wanaomwamini Kristo bila kuwa na mashaka.; #15:1 Yaani kutowakwaza kama aliyoeleza katika sura iliyotangulia.]
2Kila mmoja wetu anapaswa kumpendeza jirani yake kwa wema ili huyo apate kujijenga katika imani.[#15:2 Ni maelezo ya 13:8-10.; #15:2 Yaani yule ambaye imani yake ni dhaifu aweza kuwa na ushupavu wa kutoyumbayumba kiimani wala asikwazike kwa haraka.]
3Maana Kristo hakujipendelea mwenyewe; ila alikuwa kama yasemavyo Maandiko: “Kashfa zote walizokutolea wewe zimenipata mimi.”[#15:3 Paulo amekwisha washauri wapendane na wasiishi kwa ajili yao wenyewe, kwa hiyo, ndiyo sababu anaanza na neno ni kana kwamba anataka waige mfano wake Yesu Kristo Mwokozi wao aliyewaita wamfuate.]
4Maana, yote yaliyoandikwa yameandikwa kwa ajili ya kutufundisha sisi ili kutokana na saburi na faraja tupewayo na hayo Maandiko Matakatifu tupate kuwa na matumaini.[#15:4 Hapa Paulo anamaanisha maandiko ya Agano la Kale.; #15:4 Baada ya kutaja mambo mawili: na ambayo alikwisha taja katika 5:2-5; 8:20,25; 12:12. Paulo anakaza hivyo anapowaandikia Wakolosai (Kol 1:11) na kwa Wathesalonike (1Thes 1:3-4; ling 1Tim 6:11; 2Tim 3:11; Tito 2:2; Ebr 10:36; Yak 1:4; 2Pet 1:6).]
5Mungu aliye msingi wa saburi na faraja yote, awajalieni nyinyi kuwa na msimamo mmoja kufuatana na mfano wake Kristo Yesu,[#15:5 Hapo Paulo anawaeleza Waroma chanzo cha hayo mambo mawili saburi na . Anataka kuwashauri kuwa waendelee kumwamini Mungu katika Kristo, ili waweze kuwa na matumaini na Mungu mwenyewe. Hoja yake ni kwamba kwa nguvu zao hawawezi kujivunia na (taz pia 15:13).; #15:5 Wapatane katika mambo ambayo yaweza kuvuruga umoja wao au wito wao kwa kuishi kwa amani.; #15:5 Anakumbusha habari za maisha ya Mwokozi wao bila kutaja kwa kirefu au kueleza kinaganaga jinsi Yesu Kristo alivyokuja ulimwenguni akavumilia taabu tangu kuzaliwa mpaka alipofufuka.]
6ili nyinyi nyote, kwa nia moja na sauti moja, mumtukuze Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo.[#15:6 Elekezo kwao wasomaji kuwa wakipata na kwa basi, wamsifu asili ya hayo.; #15:6 Ni mkazo huohuo uliomo katika aya 5. Hapo awali amekwisha sisitiza kuwa watumie vipaji vyao kujenga mwili wa Kristo, sasa anarudia kusisitiza kuwa wafanye vivyo hivyo kwa ushirikiano, utengano waweza kuharibu uhusiano kati yao wakakosa kumsifu Mungu wao. Naye Yesu alikwisha waombea waumini wake wawe na umoja (Yoh 17:21-22). Mkazo wa Paulo kuhusu umoja kati ya waumini ni kama wahenga walivyosema, katika methali ya Kiswahili, “Umoja ni nguvu utengano ni udhaifu.”]
7Basi, karibishaneni kwa ajili ya utukufu wa Mungu kama naye Kristo alivyowakaribisheni.[#15:7 Mkazo anaorudia mara kwa mara. Wanaokaribishana wasukumwa na upendo (taz pia 12:13; 14:1), wafanya hivyo kwa kumwigiza Mwokozi wao (taz 15:7). Paulo aongeza mkazo wake juu ya mafundisho ya Yesu Kristo (taz Mat 25:31-46).; #15:7 Yaani alipowaita wamfuate na pia alivyowapa matumaini ya kuwa naye mbinguni (taz k.m. Mat 11:28-30; 25:34-40,46b; Yoh 11:25; 17:24; ling Ufu 2:10b; 3:11-12).]
8Maana, nawaambieni Kristo aliwatumikia Wayahudi apate kuonesha uaminifu wa Mungu, na zile ahadi Mungu alizowapa babu zetu zipate kutimia;[#15:8 Tafsiri nyingine Hoja ya Paulo ni kwamba Yesu Kristo kama Myahudi mzawa wa Abrahamu aliishi kama hao Wayahudi kwa sababu ya lengo la Mungu la kuokoa ulimwengu kwa njia yake. Naye Yesu alimtii Mungu, ambaye kila mara alimtaja kuwa Baba yake (taz k.m. Yoh 15:5-17,23-27; 16:1—17:26; 18:11).; #15:8 Ahadi kwa Abrahamu, Isaka na Yakobo hasa kuwa kutokana na Abrahamu kutakuweko taifa kubwa na mtawala atazaliwa kati ya wazawa wake Abrahamu ambaye hata manabii walitabiri juu yake (taz k.m. Mwa 12:1-3; Isa 7:14; 9:6-7; 11:1-5; Mika 5:2; ling Isa 61:1-3).]
9ili nao watu wa mataifa mengine wapate kumtukuza Mungu kwa sababu ya huruma yake. Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu:[#15:9 Ndivyo Mungu alivyomwahidi Abrahamu kuwa mataifa ya ulimwengu yatabarikiwa kwa njia yake. Ni wazi kuwa yakibarikiwa yatapaswa kusifu baraka za Mwenyezi-Mungu.; #15:9 Mungu alilichagua taifa la Israeli na kulihurumia mara nyingi walipomkosea, ni kwa ajili ya agano lake kwao ili waendelee kuwa taifa lake teule na ili mataifa mengine yapate pia kubarikiwa.]
“Kwa hiyo nitakusifu miongoni mwa watu wa mataifa.
Nitaziimba sifa za jina lako.”
10Tena Maandiko yasema:
“Furahini, enyi watu wa mataifa;
furahini pamoja na watu wake.”
11Na tena:
“Enyi mataifa yote, msifuni Bwana;
enyi watu wote, msifuni.”
12Tena Isaya asema:
“Atatokea chipukizi katika ukoo wa Yese,
naye atawatawala watu wa mataifa;
nao watamtumainia.”
13Basi, Mungu aliye msingi wa matumaini, awajazeni furaha yote na amani kutokana na imani yenu; tumaini lenu lipate kuongezeka kwa nguvu ya Roho Mtakatifu.[#15:13 Taz maelezo ya aya ya 5. Maneno yanasisitizwa sana na Paulo katika barua zake. Mkazo wake kuwa Mungu ni asili au wa matumaini unaonesha jinsi anavyowashauri wasitegemee kuzaliwa kwao kuwa ni Wayahudi au wale wa mataifa mengine kuona kuwa kwa sababu Kristo amewaokoa nao wanaweza kujipatia matumaini.; #15:13 Kwa kuwa mtu hawawezi kujipatia wajue kuwa mwenye kuwawezesha ni Mungu kwa njia ya Roho Mtakatifu. Kwa maneno mengine ni kwamba bila Roho Mtakatifu hakuna tumaini kamili. Hapa Paulo anakumbusha aliyokwisha sema kuhusu Roho Mtakatifu hapo awali katika barua hii, k.m. katika 8:9.]
14Ndugu zangu, mimi binafsi nina hakika kwamba nyinyi pia mmejaa wema, elimu yote, na mnaweza kushauriana nyinyi kwa nyinyi.[#15:14 Paulo anasifu aliowaandikia ili asiwakatishe tamaa, kwani barua yote si juu ya kuwasifu, amewapa maongozi pia kuhusu wito wao na jukumu walilonalo kwa kuishi pamoja.]
15Lakini nimewaandikia hapa na pale katika barua hii bila woga, nipate kuwakumbusheni juu ya mambo fulani. Nimefanya hivyo kwa sababu ya neema aliyonijalia Mungu[#15:15-21 Sababu ya kuwaandikia Waroma.; #15:15 Paulo amewaandikia mambo mengi hii ni pamoja na kuhusu imani, kutahiriwa, ubatizo, kutobaguana, kushirikiana, kupendana, n.k.]
16ya kuwa mtumishi wa Yesu Kristo kwa watu wa mataifa. Ni jukumu langu la kikuhani kuihubiri Habari Njema ya Mungu ili watu wa mataifa mengine wapate kuwa tambiko inayokubaliwa na Mungu, tambiko iliyotakaswa na Roho Mtakatifu.[#15:16 Aeleza kuhusu wito wake, huduma hii anaitaja mara kadhaa katika barua zake (taz 11:13; 15:18; Fil 2:17; Gal 1:16; Efe 3:8; ling Gal 2:7; Mate 9:15; 13:2; 15:12; 22:21).; #15:16 Si kama makuhani wa Agano la Kale walivyohudumu katika hekalu, bali yeye ni mwenye kupita mipaka ya nchi yake kuhudumu kati ya watu wa mataifa.; #15:16 Huduma ya Paulo anajieleza kama inavyosemwa kuhusu Yesu Kristo. Habari Njema ni kuhusu wokovu kwa watu wote. Wayahudi na wasio Wayahudi. Makuhani wa Agano la Kale hawakushughulika sana na kazi ya kuhubiri kwa hiyo hapa twaona wazo la maana kuwa wanaomfuata Yesu aliye kuhani wapaswa nao kuhubiri Injili, ni wajibu wao pia.; #15:16 Badala ya watu kutoa ng'ombe, mbuzi, kondoo, n.k. kama sadaka yao, jinsi walivyozoea tangu babu zao, wao wawe sadaka; wenye kupokelewa na Mungu kama watoto wapendwa na hapo Paulo anaeleza kuwa mwenye kufanya hivyo ndani yao ni Roho Mtakatifu, jambo ambalo amekwisha litaja mara kadhaa katika barua hii (taz 8:1-17,26-27; 15:13). Kwa upande mwingine ni kama Paulo anawataka kuwa tambiko, kwani yeye ni kuhani hapo anapowahubiria wakamrudia Mungu wao.]
17Kwa hiyo, nikiwa nimeungana na Kristo Yesu, naweza kujivunia huduma yangu kwa ajili ya Mungu.[#15:17 Hapa Paulo anawaeleza, ingawa si kwa kirefu, kuwa amekubaliwa na Kristo. Hapo bila shaka anawakumbusha alivyokwisha sema kuhusu umuhimu wa ubatizo na nia ya kwamba ubatizo wake ulikuwa wa maana; alipobatizwa amekuwa wake Kristo kama wengine walivyo wake Kristo walipobatizwa (taz 6:3-8).]
18Sithubutu kusema kitu kingine chochote isipokuwa tu kile ambacho Kristo Yesu amekifanya kwa kunitumia mimi ili watu wa mataifa wapate kutii. Amefanya hivyo kwa maneno na vitendo,[#15:18 Ndiyo sababu ya Paulo kufanya huduma (ling 6:16; 16:19; 2Kor 9:13).; #15:18 Jinsi alivyomtumia Paulo kati ya mataifa.]
19kwa nguvu ya miujiza na maajabu, na kwa nguvu ya Roho wa Mungu. Basi, kwa kusafiri kila mahali, tangu kule Yerusalemu mpaka Iluriko, nimeihubiri kikamilifu Habari Njema ya Kristo.[#15:19-21 Namna Kristo alivyomtumia Paulo. Ni maelezo zaidi ya aya ya 18.; #15:19 Ni maelezo kuhusu safari yake ya kwenda mahali Injili ilipoanzia (ling Mate 1:8; Mat 28:18-20). ni katika mkoa wa Roma huko kaskazini ya Makedonia panapojulikana leo kama Albania na Yugoslavia. Bahati mbaya hatupati maelezo ya kazi aliyofanya huko hasemi lolote katika barua yake wala Luka katika Matendo ya Mitume hakueleza chochote kuhusu kukaa kwake huko wala hataji kama alifika huko.]
20Nia yangu imekuwa daima kuihubiri Habari Njema popote pale ambapo jina la Kristo halijapata kusikika, nisije nikajenga juu ya msingi wa mtu mwingine.
21Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu:
“Watu wote ambao hawakuambiwa habari zake wataona;
nao wale ambao hawajapata kusikia, wataelewa.”
22Kwa sababu hiyo nilizuiwa mara nyingi kuja kwenu.[#15:22 Kwa ajili ya kazi ya mahali pengi alikopitia toka Yerusalemu mpaka Iluriko. Amekwisha taja vivyo hivyo alipoanza kuandika barua hii (taz Rom 1:10-15).]
23Lakini maadamu sasa nimemaliza kazi yangu pande hizi, na kwa kuwa kwa miaka mingi nimekuwa na nia kubwa ya kuja kwenu,
24natumaini kufanya hivyo sasa. Ningependa kuwaoneni nikiwa safarini kwenda Spania na kupata msaada wenu kwa safari hiyo baada ya kufurahia kuwa kwa muda pamoja nanyi.[#15:24 Kwenda huko kwa mara ya kwanza (taz pia aya ya 28).; #15:24 Paulo alitumaini kuwa Kanisa la Roma litajishughulisha na huduma ya misioni likimtumia Paulo.]
25Lakini, kwa sasa nakwenda kuwahudumia watu wa Mungu kule Yerusalemu.[#15:25 Tafsiri nyingine ni: Paulo anawataja hao waliomwamini Kristo walioko Yerusalemu. Sababu ya kurudi Yerusalemu inatajwa katika aya ya 26-28.]
26Maana makanisa ya Makedonia na Akaya yemeamua kutoa mchango wao kuwasaidia watu wa Mungu walio maskini huko Yerusalemu.[#15:26 Tayari wakati huo waumini waliokuwa Makedonia na Akaya walikwisha tambulika kuwa kundi linalojitegemea na hata kusaidia wengine.; #15:26 Hapa Paulo hataji aina za mchango bila shaka kwa kuwa ni ule uliotolewa kwa Wakristo anaowataja kuwa wa huko Yerusalemu, huenda ni pesa na vitu vingine walivyokosa kwa maisha yao ya kawaida. Paulo alishauri mara kwa mara Wakristo watoe chochote walichonacho kwa uhuru, upendo ukarimu, n.k. (taz pia 1Kor 16:1-4; 2Kor 8—9), ni namna ya kuonesha upendo wao kwa wengine.]
27Wao wenyewe wameamua kufanya hivyo; lakini, kwa kweli, hilo ni jukumu lao kwa hao. Maana, ikiwa watu wa mataifa mengine wameshiriki baraka za kiroho za Wayahudi, wanapaswa nao pia kuwahudumia Wayahudi katika mahitaji yao ya kidunia.[#15:27 Wapaswa kuwajibika kuwatunza hao Habari Njema ilipoanzia.; #15:27 Kunakotajwa hapa ni kule kupata wokovu ulioahidiwa Wayahudi - kuja kwa Kristo Mkombozi; na ye yote mwenye kuamini apate uzima wa milele.]
28Nitakapokwisha tekeleza kazi hiyo na kuwakabidhi mchango huo uliokusanywa kwa ajili yao, nitawatembeleeni nyinyi nikiwa safarini kwenda Spania.[#15:28 Yaelekea Paulo hakuwa na shabaha ya kukaa Yerusalemu. Ni dokezo kuwa yeye ametumwa kuwahudumia watu wa mataifa, ingawa hata kule kuwapelekea Wakristo wa Yerusalemu mchango ni kuwahudumia pia, lakini si kukaa na kuhubiri huku na kule. Pia ni wazi kuwa kulikuwepo mitume na wengi waliokuwa Wakristo tayari kwa miaka kadhaa; wahubiri walikuweko, kwa hiyo kutokuwako kwa Paulo si pigo kubwa.]
29Najua ya kuwa nikija kwenu nitawaletea wingi wa baraka za Kristo.[#15:29 Tumaini la Paulo kuwa kuhubiri Habari Njema kwaleta baraka.]
30Basi, ndugu zangu, nawasihi kwa Bwana wetu Yesu Kristo na kwa upendo uletwao na Roho, mniunge mkono kwa kuniombea kwa Mungu.[#15:30-32 Mkazo kuhusu umuhimu wa kuomba. Paulo naye alihitaji nguvu ya Roho Mtakatifu.]
31Ombeni nipate kutoka salama miongoni mwa wale wasioamini walioko Uyahudi, nayo huduma yangu huko Yerusalemu ipate kukubaliwa na watu wa Mungu walioko huko.[#15:31 Yaelekea Paulo alikuwa na wasiwasi kuhusu hao wapinzani wa Injili ambao yeye anawafahamu vizuri shabaha zao, kwani alikuwa mmoja wao. Kulikuwako waliokuwa tayari kumpinga hii ni wazi kama anavyojieleza mwenyewe taz Mate 20:22-23; 21:7—28:31.; #15:31 Hatujui kwa uwazi anamaanisha nini, kama ni kuhubiri huko; lakini haielekei kama huo ulikuwa wajibu wake huko, labda ni namna ya kugawa mchango aliokuwa akiwapelekea. Kazi ambayo ilipaswa kufanywa vizuri wenye kupokea waridhike na kuufurahia na wenye kutuma wapate ripoti nzuri.]
32Hivyo, Mungu akipenda, nitaweza kuja kwenu na moyo wa furaha, nikapumzike pamoja nanyi.[#15:32 Mara tatu katika sura hii anataja juu ya safari yake ya kuelekea Roma, na mara anapoitaja anadokeza kuwa atafurahi pamoja nao (taz 22,24,29).]
33Mungu aliye chanzo cha amani na awe nanyi nyote! Amina![#15:33 Mwisho hapa wa barua yake Paulo. Mungu chanzo cha amani: tafsiri nyingine: . Hapa Paulo anakiri kuwa amani, asili yake ni Mungu tu, si kwa nguvu za kibinadamu; ndiyo sababu hata kwenda kwake Yerusalemu kulihitaji maombi ili asipatwe na fujo au mikasa ya aina yoyote. Mkazo huu kuwa ni unarudiwa mara kwa mara katika barua zake Paulo (taz 5:1; 16:20; 1Kor 7:15; 2Kor 13:11; Fil 4:7,9; 1Thes 5:23, 2Thes 3:16); na kule kutakia wengine amani ni kama ilikuwa tabia yake Paulo (taz pia Rom 12:18; 14:19; 15:13; 1Kor 1:3; 2Kor 1:2; Gal 1:3; Efe 1:2; Fil 1:2; Kol 1:2; 1Thes 1:1; 2Thes 1:2; Tito 1:4; File 3; Gal 6:16; Efe 6:23; 2Tim 2:22; 1Thes 5:13; 2Thes 3:16; 1Tim 2:2; 2Tim 2:22).]