Sira 34

Sira 34

Ndoto hazina maana

1Mtu mjinga huwa na matumaini ya bure na ya uongo;

ndoto humpa mpumbavu mabawa ya kuruka.

2Kama mtu anayejaribu kushika kivuli na kufukuza upepo

ndivyo alivyo mtu anayeamini ndoto.

3Ndoto ni kama kioo,

sura inayoukabili uso.

4Ni kitu gani kiwezacho kutakaswa na uchafu?

Je, ukweli waweza kupatikana kwa uongo?

5Kupiga bao, ramli na ndoto ni upuuzi;

akili huwa na mawazo kama ya mama anayejifungua.

6Usizitie maanani ndoto

isipokuwa kama zimetoka kwa Mungu Mkuu.

7Maana ndoto zimewadanganya wengi,

na wale wanaozitumaini wameaibishwa.

8Sheria ni kamilifu bila udanganyifu huo,

nayo hekima ni kamilifu kwa mtu mwaminifu:

Kusafiri

9Mtu aliyesafiri sana anajua mengi,

na mtu mzoefu wa mengi anajua anachoongea.

10Mtu ambaye hajakumbana na matatizo hajui mengi,

11lakini aliyesafiri sana amejipatia maarifa.

12Katika safari zangu nimeona mengi;

ninajua mengi kuliko niwezavyo kuyaeleza.

13Mara nyingi nimekuwa katika hatari ya kifo,

lakini nimechopoka kwa sababu ya maarifa haya.

Kumcha Bwana

14Wamchao Bwana wataishi,

15maana tumaini lao liko kwake yeye anayewaokoa.

16Amchaye Bwana hatakuwa na woga,

hawezi kuogopa kwani Bwana ndiye tumaini lake.

17Heri mtu ambaye anamcha Bwana!

18Maana anamtazamia yeye amtegemeze.

19Bwana huwaangalia kwa wema wale wampendao.

Yeye ni ngao imara na tegemeo lao thabiti;

yeye ni kinga yao mbali na upepo mkali,

ni kivuli chao wakati wa jua kali;

yeye huwalinda wasijikwae,

huwasaidia wasianguke.

20Bwana huijaza mioyo furaha,

na huyatia macho mwanga.

Yeye huwapa watu afya, uhai na baraka

Tambiko

21Mtu akitoa sadaka kitu kilichopatikana kwa udanganyifu

tambiko yake hiyo ina dosari.

Zawadi za wasiotii sheria hazikubaliki.

22Mungu Mkuu hakubali sadaka za wasiomcha,

wala wingi wa sadaka hauwezi kuleta upatanisho.

23Mtu atoaye sadaka kitu alichomnyang'anya maskini,

ni sawa na mtu anayemuua mtoto mbele ya baba yake.

24Chakula cha maskini ni uhai wake;

yeyote anayempora maskini chakula ni muuaji.

25Kumnyang'anya jirani chakula chake ni kumuua;

na kumnyang'anya mwajiriwa mshahara wake ni kuua.

26Mtu mmoja akijenga na mwingine akibomoa,

je, wamefanikiwa chochote ila kutoa jasho?

27Mmoja akimwomba Mungu na mwingine akilaani,

je, Bwana ataisikiliza sauti ya nani?

28Mtu akitawadha baada ya kushika maiti, akaishika tena,

je, amepata faida gani kwa kutawadha kwake?

29Hivyo mtu akifunga kwa ajili ya dhambi zake,

kisha akaenda kufanya mambo yaleyale,

ni nani atakayesikiliza sala yake?

Tena amepata faida gani kwa kujinyenyekesha?

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania