The chat will start when you send the first message.
1Mimi ni ua la Sharoni,
ni yungiyungi ya bondeni.
2Kama yungiyungi kati ya michongoma,
ndivyo alivyo mpenzi wangu kati ya wasichana.
3Kama mtofaa kati ya miti ya msituni,[#2:3 Hili ni jina la tunda mwitu lakini ni lipi hasa haijulikani. Matunda ya mtofaa yalifikiriwa kuwa na kitu cha kuhimiza mapenzi.]
ndivyo alivyo mpenzi wangu kati ya wavulana.
Nafurahia kuketi chini ya kivuli chake,
na tunda lake tamu sana kwangu.
4Alinichukua hadi ukumbi wa karamu,[#2:4 Neno kwa neno: “nyumba ya divai” divai ikiwa ni mfano wa furaha ya mapenzi.]
akatweka bendera ya mapenzi juu yangu.
5Nishibishe na zabibu kavu,
niburudishe kwa matofaa,
maana naugua kwa mapenzi!
6Mkono wake wa kushoto chini ya kichwa changu,
mkono wake wa kulia wanikumbatia.
7Nawasihi enyi wanawake wa Yerusalemu,
kama walivyo paa au swala wa porini,
msiyachochee wala kuyaamsha mapenzi,
hadi hapo wakati wake utakapofika.
8Hiyo ni sauti ya mpenzi wangu,
yuaja mbio,
anaruka milima,
vilima anavipita kasi!
9Mpenzi wangu ni kama paa,
ni kama swala mchanga.
Amesimama karibu na ukuta wetu,
achungulia dirishani,
atazama kimiani.
10Mpenzi wangu aniambia:
“Inuka basi, ewe mpenzi wangu, unipendezaye,
njoo twende zetu.
11Tazama, majira ya baridi yamepita,[#2:11 Msimu wa baridi katika Mashariki ya Kati ulikuwa wakati wa mvua. Mwishoni mwa msimu huo huanza wakati wa joto na majani na maua kuchanua; ni wakati ambapo hua waliokuwa wamehama wakati wa baridi wanarudi tena.]
nazo mvua zimekwisha koma;
12maua yamechanua kila mahali.
Wakati wa kuimba umefika;
sauti ya hua yasikika mashambani mwetu.
13Mitini imeanza kuzaa;
na mizabibu imechanua;
inatoa harufu nzuri.
Njoo, basi, ewe mpenzi wangu unipendezaye,
njoo twende.
14Ee hua wangu, uliyejificha miambani.
Hebu niuone uso wako,
hebu niisikie sauti yako,
maana sauti yako yapendeza na uso wako wavutia.
15“Tukamatieni mbweha,[#2:15 Matumizi ya mbweha hapa si dhahiri. Huenda ni mfano wa vijana wanaume ambao wanachukuliwa kuwa tishio kwa bustani ya mizabibu ambayo hapa ni mfano wa vijana wanawake.]
wale mbweha wadogowadogo,
wanaoiharibu mizabibu yetu inayochanua.”
16Mpenzi wangu ni wangu, nami ni wake.
Yeye hulisha kondoo wake penye yungiyungi,
17hadi hapo jua linapochomoza
na vivuli kutoweka.
Rudi kama paa mpenzi wangu,
kama swala mdogo juu ya milima ya Betheri.