Wimbo Ulio Bora 6

Wimbo Ulio Bora 6

1Ewe mwanamke uliye mzuri sana;

amekwenda wapi huyo mpenzi wako?

Ameelekea wapi mpenzi wako

ili tupate kushirikiana nawe katika kumtafuta?

2Mpenzi wangu amekwenda bustanini mwake,

mahali ambapo rihani hustawi.

Yeye analisha kondoo wake

na kukusanya yungiyungi.

3Mimi ni wake mpenzi wangu, naye ni wangu;

yeye huwalisha kondoo wake penye yungiyungi.

Shairi la tano

4Mpenzi wangu, wewe u mzuri kama Tirza,[#6:4 Huu ulikuwa mji mkuu wa kwanza wa utawala wa kaskazini chini ya Yeroboamu (931-910 K.K.).]

wapendeza kama Yerusalemu,

unatisha kama jeshi lenye bendera.

5Hebu tazama kando tafadhali;

ukinitazama nahangaika.

Nywele zako ni kama kundi la mbuzi,

wateremkao chini ya milima ya Gileadi.

6Meno yako kama kundi la kondoo majike

wanaoteremka baada ya kuogeshwa.

Kila mmoja amezaa mapacha,

na hakuna yeyote aliyefiwa.

7Mashavu yako ni kama nusu mbili za komamanga,

nyuma ya shela lako.

8Wapo malkia sitini, masuria themanini,[#6:8 Labda yahusu wake wengi wa Solomoni na masuria wake, ingawaje idadi hii ni ndogo kuliko ile ya 1Fal 11:3.]

na wasichana wasiohesabika!

9Hua wangu, mzuri wangu, ni mmoja tu,

na ni kipenzi cha mama yake;

yeye ni wa pekee kwa mama yake.

Wasichana humtazama na kumwita heri,

nao malkia na masuria huziimba sifa zake.

10Nani huyu atazamaye kama pambazuko?

Mzuri kama mwezi, mwangavu kama jua,

na anatisha kama jeshi lenye bendera.

11Nimeingia katika bustani ya milozi

kutazama machipuko ya bondeni,

kuona kama mizabibu imechanua,

na mikomamanga imechanua maua.

12Bila kutazamia, mpenzi wangu,

akanitia katika gari la mkuu.

13Rudi, rudi ewe msichana wa Mshulami.[#6:13 Kiebrania ni “Shulammite” na huenda lilitumika hapa kukumbusha juu ya Solomoni, au hata uzuri wa yule Abishagi kutoka Shunemu (1Fal 1:3-4).]

Rudi, rudi tupate kukutazama.

Mbona mwataka kunitazama miye Mshulami

kana kwamba mnatazama ngoma

kati ya majeshi mawili?

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania