The chat will start when you send the first message.
1Lakini, mwanga mkubwa uliwaangazia watu wako watakatifu.
Maadui zao walisikia sauti zao lakini hawakuweza kuwaona;
waliona watu wako wana bahati kwa vile hawakuteseka.
2Hao maadui angalau walishukuru
kwamba watu wale ambao waliwatesa hapo awali hawakuwalipiza kisasi,
na hivyo wakawasihi wajiendee zao.
3Kisha ukawapatia watu wako mnara wa mwanga wa moto
uwaongoze katika njia ambayo hawakuijua,
mwangaza mtulivu katika safari hiyo tukufu.
4Lakini maadui zao wakanyimwa mwanga huo,
wakastahili kufungwa gizani hao waliokuwa wamewafunga watu wako,
ambao kwa njia yao ulimwengu ungepewa mwanga wa milele wa sheria yako.
5Wakati maadui hao walipoamua kuwaua watoto wachanga wa watu wako,
na yule mtoto mchanga alipoachwa na kuokolewa baadaye,
wewe uliwaadhibu kwa kuua idadi kubwa ya watoto wao,
na kuwaangamiza wote katika mafuriko makubwa.
6Lakini wazee wetu walijulishwa juu ya usiku huo
ili wakiwa wanajua wapate moyo na kufurahia ahadi walizopewa.
7Watu wako walitazamia kuokolewa kwa waadilifu
na kuangamizwa kwa maadui zao.
8Kwa kitendo hichohicho cha kuwaadhibu maadui zetu
ulitujalia heshima tukufu ya kutuita kwako.
9Kwa siri, watu hao wema wa taifa adilifu walitolea tambiko
na kwa moyo mmoja wakatekeleza sheria ya Mungu
watu watakatifu washiriki pamoja: baraka na hatari,
wakawa tayari wanaimba sifa za wazee wao.
10Lakini sauti za maadui zao zilisikika kila mahali
wakiomboleza vifo vya watoto wao.
11Watumwa walipata adhabu ileile waliyopata mabwana zao;
watu wa kawaida wakapata hasara sawasawa na mfalme.
12Wote pamoja walikufa kwa njia ileile;
maiti zilikuwa nyingi mno
na waliobaki hai hawakutosha kuzizika.
Kwa pigo moja tu, watoto wao waliowapenda mno walikufa.
13Watu hao hawakujali onyo lolote ila walitegemea uchawi wao.
Lakini watoto wao wa kwanza walipoangamizwa,
walitambua kwamba watu hao walikuwa watoto wa Mungu.
14Kulipokuwa shwari kabisa, kila mahali,
na usiku ukiwa umefikia nusu ya safari yake,
15Neno wako wa nguvu kuu akashuka kutoka mbinguni,
naam, kutoka kwenye kiti chako cha enzi,
akiwa kama mtu shujaa wa vita,
aliishukia nchi iliyohukumiwa kuangamizwa,
16ameshika upanga mkali wa kutekeleza amri yako thabiti.
Alisimama na vitu vyote vikakumbwa na kifo,
aligusa mbingu kwa kichwa chake
akiwa amesimama juu ya nchi.
17Mara, watu wale wakapatwa na maono ya kutisha
na ndoto za kuogopesha zikawavamia.
18Walilala kila mahali nchini wamezirai
huku wakionesha sababu ya kifo chao.
19Ndoto zao za kutisha ziliwadhihirishia jambo hilo,
ili wasije wakafa kabla ya kujua sababu ya mateso yao.
20Waadilifu pia iliwabidi kuonja kifo;
ugonjwa mbaya uliwavamia wengi kule jangwani,
lakini hasira yako haikudumu muda mrefu.
21Mtu mmoja asiye na hatia aliharakisha kuwaombea.
Yeye, kama vile kasisi, alifanya maombi na kufukiza ubani wa upatanisho,
na hivyo akaonesha kwamba alikuwa mtumishi wako.
Hizo zikiwa silaha zake,
aliikabili hasira yako na kuyakomesha yale maafa.
22Aliyashinda yale maafa si kwa nguvu za kibinadamu
wala kwa silaha za vita,
ila kwa sala aliikomesha ile adhabu
akikumbusha ahadi na maagano uliyowapa wazee wetu.
23Maiti zilipokuwa zimerundikana,
yeye aliingilia kati na akaikinga hasira yako,
akaizuia isiwapate wale waliokuwa bado hai.
24Alikuwa amevaa vazi refu lililochorwa alama za ulimwengu,
na kifuani alivaa sifa za wazee wetu zimechorwa katika safu nne za vito,
na kichwani kilemba kilichopambwa kuonesha enzi yako.
25Mharibifu aliyaogopa hayo, akakata tamaa.
Uliwaonjesha tu hasira yako lakini hiyo ilitosha.