Hekima ya Solomoni 4

Hekima ya Solomoni 4

1Afadhali kukosa watoto na kuwa mnyofu,

maana unyofu wako utakumbukwa milele,

na unatambuliwa na Mungu na wanaadamu.

2Unyofu wako utawapa watu fursa ya kuuiga,

na usipokuwapo watu watasikitika kuukosa.

Siku zote unapita umevikwa taji ya ushindi,

mshindi katika mashindano ya tuzo zisizo na dosari.

3Lakini wazawa wengi wa wasiomcha Mungu hawafai kitu,

watoto wao haramu hawawezi kutoa mizizi

wala kuwa na msingi imara.

4Na hata wakitoa matawi ni ya muda tu,

bila mizizi imara watatikiswa na upepo

na kwa nguvu za dhoruba watang'olewa.

5Matawi yao yatavunjika kabla ya kukomaa,

matunda yao hayatafaa chochote,

hayataiva yaliwe, ni bure kabisa.

6Watoto waliozaliwa haramu

watashuhudia juu ya uovu wa wazazi wao wakati wa hukumu.

7Lakini mtu mwema, hata akifa kijana, atapata pumziko.

8Uzee unaheshimika sio tu kwa urefu wa maisha,

wala haupimwi kwa wingi wa miaka.

9Hekima na maisha mema ni ishara ya kukomaa;

hivyo huja pamoja na uzee.

10Palikuwa na mtu aliyempendeza Mungu naye Mungu akampenda,

wakati alipokuwa anaishi kati ya wenye dhambi, Mungu alimchukua,

11akamhamisha ili uovu usibadili busara yake

udanganyifu usiweze kuipotosha roho yake.

12Mvuto wa uovu huzuia wema usionekane;

hata mtu asiweze kuona jambo jema mbele yake;

upepo wa tamaa waweza kumpotosha mtu mnyofu.

13Huyo alifikia ukamilifu kwa muda mfupi tu,

akawa ametimiza miaka mingi.

14Maisha yake yalimpendeza Bwana,

naye akaharakisha kumtoa kati ya uovu.

Watu waliona jambo hilo lakini hawakuelewa;

hawakuweza kutambua jambo hili moja:

15Kwamba Mungu ni mwema na mwenye huruma kwa watu wake;

huwalinda hao aliowateua kuwa wake.

16Mtu mwema ambaye amekwisha kufa

atawahukumu wasiomcha Mungu walio hai.

Kijana aliyefikia hali ya ukamilifu upesi,

atamwaibisha mzee mkongwe aliye dhalimu.

17Watu waovu watamwona mwenye busara anakufa

lakini hawataelewa matakwa ya Bwana juu yake,

wala kwa sababu gani alimweka salama.

18Watadhihaki kifo cha mtu mwema

lakini Bwana atawacheka.

Wao watakapokufa hawatazikwa kwa heshima;

na hata wafu watawapuuza milele.

19Bwana atawatupa chini na kuwanyamazisha;

atawatikisa mpaka misingi yao,

watakuwa magofu matupu na ukiwa

wataaibika kwa uchungu.

Hakuna mtu atakayewakumbuka tena.

Tofauti ya wema na waovu wakati wa hukumu

20Waovu wataingia hukumuni kwa hofu na woga dhambi zao zitakapohesabiwa,

matendo yao maovu yatawahukumu mbele ya macho yao.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania