Hekima ya Solomoni 6

Hekima ya Solomoni 6

Jukumu la watawala

1Sikilizeni basi, enyi wafalme, mkaelewe;

jifunzeni, enyi waamuzi popote duniani.

2Tegeni sikio nyinyi mnaotawala watu wengi,

na kujisifia wingi wa mataifa.

3Mamlaka hayo mlipewa na Bwana;

na utawala mliupata kwa Mungu Mkuu.

Atazipima kazi zenu na kuchunguza mipango yenu.

4Maana, kama watumishi katika utawala wake, hamtawali kwa uadilifu,

kama hamshiki sheria,

wala kufuata mwongozo wa Mungu,

5yeye atawajia ghafla na kuwapeni adhabu kali,

maana adhabu kali huwapata aghalabu wenye madaraka.

6Watu wa kawaida wanaweza kusamehewa kutokana na huruma;

lakini wenye madaraka watakabiliwa na uchunguzi mkali.

7Maana Bwana wa wote hamwogopi mtu yeyote,

ukuu wa mtu hauwezi kumfanya apendelee;

Yeye mwenyewe aliwafanya wote, wakubwa na wadogo

na huangalia mahitaji ya wote kwa usawa.

8Lakini wenye madaraka watakabiliwa na uchunguzi mkali.

9Basi, maneno yangu yawahusu nyinyi wafalme,

ili mjifunze kuwa na hekima, msije mkakosa.

10Maana wanaozingatia mambo matakatifu

watakubaliwa kuwa watakatifu.

Waliofunzwa hayo watapata humo cha kujitetea hukumuni.

11Basi, muwe na hamu ya mafundisho yangu;

yatamani yawaongoze nanyi mtapata nidhamu.

Thamani ya Hekima

12Hekima huangaza wala hafifii.

Wanaompenda Hekima humwona kwa urahisi,

wanaomtafuta Hekima humpata.

13Hekima hutangulia kujionesha kwa wale wanaomtaka.

14Ukiamka mapema asubuhi kumtafuta, hutataabika;

utamkuta anakungojea mlangoni pake.

15Kumsikiliza Hekima kwa makini ni kupata maarifa kamili.

Ukimtafuta usiku na mchana hutapata masumbuko.

16Hekima daima huwatafuta wale wanaomstahili;

njiani hujidhihirisha kwao kwa upendo,

yu pamoja nao katika kila wazo.

17Mwanzo wa Hekima ni hamu kubwa ya kufunzwa;[#6:17 Taz 2Pet 1:5-7 maelezo.]

kujali mafundisho ni kumpenda Hekima,

18kumpenda ni kushika sheria zake;[#6:18 Sira 2:15-16; Yoh 14:15.]

kushika sheria zake ni uhakika wa kutokufa.

19na kutokufa kwamleta mtu karibu na Mungu.

20Hivyo hamu ya kumpata Hekima huongoza kwenye ufalme.

21Basi, enyi watawala wa watu,

kama mwafurahia viti vyenu vya enzi

na alama za mamlaka juu ya watu,

mheshimuni Hekima mpate kutawala milele.

Nia ya kuwashirikisha wengine Hekima

22Nitawaambieni Hekima ni nani na chanzo chake.

Sitawaficheni siri yoyote ile;

nitawaambieni historia yake yote tangu mwanzo wake,

na kudhihirisha wazi habari zake

bila kuacha ukweli wowote ule.

23Wivu ule mbaya kamwe hautakuwa mwenzangu,

maana Hekima hapatani na hali ya wivu.

24Wingi wa wenye Hekima ni wokovu kwa ulimwengu,

mfalme mwenye busara ni uthabiti wa watu wake.

25Kwa hiyo basi, mfunzwe na maneno yangu,

nanyi mtapata faida.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania