Hekima ya Solomoni 7

Hekima ya Solomoni 7

Mfalme ni sawa na watu wengine

1Mimi ni binadamu ambaye hufa, sawa na wengine,

mzawa wa yule mtu wa kwanza aliyeumbwa kutoka kwa udongo.

Nilitengenezwa nikawa mwili tumboni mwa mama yangu

2kwa muda upatao miezi tisa,

baada ya kuwekwa pamoja kwa mbegu ya mtu

na kwa furaha ya ndoa.

3Nami nilipozaliwa, nilianza kupumua hewa ya kawaida

nilitua juu ya ardhi yenye asili moja nami,

na sauti ya kwanza niliyotoa ilikuwa kilio kama wengine.

4Nilivikwa nguo za kitoto, nikatunzwa kwa uangalifu.

5Hakuna mfalme yeyote aliyeanza kuishi kwa namna nyingine;

6maana wote huingia duniani kwa njia moja na hutoka humo kwa njia moja.

Solomoni anathamini Hekima

7Basi, niliomba, nami nikapewa maarifa;[#7:7 1Fal 3:5-15; Hek 9:1-18.]

nilimwomba Mungu, nayo roho ya Hekima ikanijia.

8Nilimthamini Hekima kuliko viti vya enzi na mamlaka,

nikaona utajiri si kitu ukilinganishwa naye.

9Sikumfananisha na johari yenye thamani kubwa,

maana dhahabu yote duniani ni kama mchanga,

na fedha ni kama udongo tu mbele yake.

10Nilimpenda Hekima kuliko afya na urembo,

nilimpendelea kuliko mwanga wa jua,

maana mwangaza wake haufifii kamwe.

11Mema yote yalinijia pamoja na Hekima;

mikononi mwake nilipata mali isiyohesabika.

12Niliyafurahia hayo yote maana aliniletea Hekima;

lakini sikujua kwamba Hekima ndiye mama wa hayo yote.

13Nilijifunza bila hila na kufunza bila lalamiko;

utajiri wake sikuwaficha watu.

14Hekima ni hazina isiyomalizika kwa watu;

wanaopata Hekima hujipatia urafiki na Mungu;

yeye huthibitisha yote wanayojifunza kutoka kwake.

15Namwomba Mungu anijalie kunena kadiri atakavyo,

na mawazo yangu yastahili yale niliyojifunza.

Mungu mwenyewe ndiye kiongozi wa Hekima;

yeye huwakosoa wale walio na busara.

16Sisi tumo mikononi mwake, pamoja na maneno yetu;

naam, sisi, maarifa yetu na ufundi wetu.

17Yeye ndiye aliyenijalia ujuzi sahihi wa nguvu za maumbile:

ulimwengu ulitengenezwa kwa kitu gani,

na maunganisho ya maumbile yake,

18mianzo ya nyakati, miisho yake na katikati yake,

zamu za vituo vya jua na mabadiliko ya majira,

19mfululizo wa miaka, na makundi ya nyota.

20Amenifundisha juu ya asili ya viumbe hai,

hisia za wanyama wa porini,

nguvu za roho,

uwezo wa akili ya binadamu,

mimea mbalimbali na matumizi ya mizizi yake.

21Nilijifunza mambo yaliyofichika na yaliyo dhahiri,

maana Hekima, mratibu wa mambo yote, alinifundisha.

Maumbile Yya Hekima

22Katika Hekima kuna roho ya maarifa na utakatifu;

roho ya pekee inayojidhihirisha kwa namna nyingi,

nyepesi sana na yenye kumudu kwa urahisi;

dhahiri, safi, wazi, na isiyoweza kuharibiwa;

yenye kupenda wema, hodari na isiyoshindwa na chochote;

23yenye ukarimu na yenye kupenda watu;

roho thabiti, yenye kuaminika na isiyo na wasiwasi;

yenye nguvu na uwezo wa kuona yote;

yenye kupenya kila chenye akili, kilicho safi

na chenye werevu wa hali ya juu.

24Hekima huenda kwa urahisi kuliko mwendo wowote;

ni safi hivyo kwamba hupenya na kuenea ndani ya kila kitu.

25Hekima ni pumzi ya nguvu ya Mungu,

mmiminiko safi wa utukufu wa Mungu Mwenye Nguvu;

hivyo, chochote kilicho najisi hakiwezi kumwingia.

26Hekima ni mng'ao wa mwanga wa milele,

kioo safi cha matendo ya Mungu

na mfano wa wema wake.

27Ingawa Hekima ni mmoja aweza kutenda chochote,

habadiliki, ingawa hufanya upya kila kitu.

Katika vizazi vyote huingia rohoni mwa watu watakatifu

na kuwafanya marafiki wa Mungu na manabii.

28Maana Mungu humpenda tu mtu akaaye na Hekima.

29Hekima ni mzuri kuliko jua

na apita makundi yote ya nyota;

ni bora kuliko mwanga wa mchana,

30maana baada ya mchana huja usiku,

lakini uovu hauwezi kumshinda Hekima.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania