Hekima ya Solomoni 9

Hekima ya Solomoni 9

Sala ya kuomba Hekima

1“Ee Mungu wa wazee wetu, Bwana mwenye huruma!

Kwa neno lako uliumba vitu vyote.

2Kwa Hekima yako ulimuumba mtu

avitawale viumbe ulivyoumba,

3aumiliki ulimwengu kwa utakatifu na uadilifu,

na kutekeleza haki kwa moyo mnyofu.

4Nakuomba unipe Hekima anayekaa kando ya kiti chako cha enzi;

wala usinikatae mimi miongoni mwa watumishi wako.

5Mimi ni mtumishi wako, mtoto wa mjakazi wako,

mtu dhaifu asiye wa siku nyingi,

wala sina nguvu ya kuelewa hukumu na sheria.

6Hata kama mtu yeyote akiwa mkamilifu kiasi gani,

bila Hekima atokaye kwako atakuwa bure tu.

7Ulinichagua mimi kuwa mfalme wa watu wako,

hakimu wa wanao wa kiume na wa kike.

8Uliniagiza nijenge hekalu juu ya mlima wako mtakatifu,

na madhabahu katika mji uliochagua kuwa makao yako,

mfano wa hema takatifu uliyoifanya tangu awali.

9Hekima yupo pamoja nawe; naye ajua matendo yako;

alikuwa pamoja nawe wakati ulipoumba ulimwengu.

Hekima anajua yanayokupendeza,

na yaliyo sawa kulingana na amri zako.

10Umpeleke, basi, kutoka mbingu tukufu,

kutoka kiti chako cha enzi kitukufu,

ili akae nami na kufanya kazi pamoja nami,

nipate kujifunza yale yanayokupendeza.

11Maana Hekima anajua na anaelewa mambo yote,

naye ataniongoza kwa busara katika matendo yangu;

kwa utukufu wake atanilinda.

12Hapo matendo yangu yatakubalika.

Nitawahukumu watu wako kwa haki

na kustahili kuwa katika kiti cha enzi cha baba yangu.

13“Nani awezaye kuijua nia ya Mungu?

Au nani awezaye kufahamu matakwa yake?

14Akili ya binadamu haifai kitu

na elimu yetu huelekea kupotosha,

15kwa maana miili yetu yenye kufa hugandamiza roho zetu.

Mwili uliotengenezwa kwa udongo, ni mzigo kwa akili timamu.

16Twabahatisha tu kupambanua juu ya mambo ya duniani;

na yale yaliyo karibu nasi ni jasho kuyafahamu.

Nani basi, atakayefaulu kujifunza yaliyoko mbinguni?

17Hakuna aliyeweza kujifunza mashauri yako, ee Mungu, isipokuwa kwanza umempa Hekima

na kumpelekea roho yako kutoka juu.

18Ndivyo njia za watu duniani zilivyowekwa sawa,

wakajifunza yanayokupendeza

na kuokolewa na Hekima.”

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania