The chat will start when you send the first message.
1Neno la Mwenyezi-Mungu lililomjia Sefania mwana wa Kushi, mwana wa Gedalia, mwana wa Amenia, mwana wa Hezekia, wakati wa utawala wa mfalme Yosia mwana wa Amoni, mfalme wa Yuda:[#1:1 Nasaba ya nabii Sefania ni ndefu kuliko nasaba nyingine za manabii. Kutaja ukoo wake hadi kizazi cha 4 aghalabu kunaonesha kwamba yeye alikuwa mtu maarufu. Jina la babu yake “Kushi” ni jina pia la nchi kwenye eneo la Afrika kaskazini ambapo sasa ni nchi za Misri Ethiopia, Eritrea na Sudani.]
2Mwenyezi-Mungu asema:
“Nitavifagilia mbali viumbe vyote duniani:
3wanadamu, wanyama, ndege wa angani
na samaki wa baharini;
vyote nitaviangamiza.
Waovu nitawaangamiza kabisa;
wanadamu nitawafagilia mbali duniani.
4Nitaunyosha mkono wangu dhidi ya nchi ya Yuda,[#1:4 Huu ni msemo unaotumika mara kwa mara katika Biblia kwa maana ya “nitaadhibu” (taz Isa 5:25; 23:11; Yer 6:12; 15:6; Eze 6:14; 14;9,13).]
kadhalika na wakazi wote wa mji wa Yerusalemu.
Nitaangamiza mabaki yote ya Baali kutoka nchi hii,
na hakuna atakayetambua jina lao.
5Nitawaangamiza wote wanaosujudu juu ya paa,
wakiabudu jeshi la mbinguni.
Nitawaangamiza wale wanaoniabudu
na kuapa kwa jina langu,
hali wanaapa pia kwa jina la mungu Milkomu.
6Nitawaangamiza wote walioniacha mimi Mwenyezi-Mungu
wote walioacha kunitafuta na kuniuliza shauri.”
7Nyamazeni mbele ya Bwana Mwenyezi-Mungu,[#1:7 Rejea Hab 2:20; Zek 2:13.]
kwani siku ya Mwenyezi-Mungu iko karibu.
Mwenyezi-Mungu ameandaa tambiko,
nao aliowaalika amewateua.
8Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Katika siku ile ya karamu yangu,
nitawaadhibu viongozi wa watu hao,
kadhalika na wana wa mfalme
pamoja na wote wanaoiga desturi za kigeni.
9Siku hiyo nitawaadhibu wote:
wanaoruka kizingiti cha nyumba kama wapagani,
wanaojaza nyumba ya bwana wao vitu vya dhuluma na wizi.
10“Siku hiyo, nasema mimi Mwenyezi-Mungu,
Kutasikika kilio kutoka Lango la Samaki,
maombolezo kutoka Mtaa wa Pili,
na mlio mkubwa kutoka milimani.
11Lieni enyi wakazi wa Makteshi![#1:11 Eneo kusini mwa Yerusalemu lakini haijulikani hasa ni wapi.]
Wafanyabiashara wote wameangamia,
wote wapimao fedha wamefutiliwa mbali.
12Wakati huo nitaupekua mji wa Yerusalemu kwa taa,[#1:12 Baadhi ya wafafanuzi wa Maandiko Matakatifu wanafikiri kwamba nabii Sefania alipotamka ujumbe huu alifanya hivyo akiwa na taa mkononi.]
nitawaadhibu wanaoishi wametulia kama machicha ya divai,
wote ambao husema mioyoni mwao:
‘Mwenyezi-Mungu hatafanya kitu: chema au kibaya.’
13Utajiri wao utanyakuliwa,
na nyumba zao zitaachwa tupu!
Watajijengea nyumba, lakini hawataishi humo.
Watapanda mizabibu, lakini hawatakunywa divai yake.”
14Ile siku kubwa ya Mwenyezi-Mungu imekaribia,[#1:14-18 Isa 13:6; Eze 30:2-3; Yoe 1:15.]
iko karibu na inakuja mbio.
Mlio wa siku ya Mwenyezi-Mungu ni wa uchungu;
hapo, shujaa atalia kwa sauti.
15Siku hiyo itakuwa siku ya ghadhabu,
ni siku ya dhiki na uchungu,
siku ya giza na huzuni;
siku ya uharibifu na maangamizi,
siku ya mawingu na giza nene.
16Siku hiyo ni ya mlio wa tarumbeta ya vita,
dhidi ya miji yenye ngome na kuta ndefu.
17Kwa kuwa watu wamemkosea Mwenyezi-Mungu,
yeye atawaletea dhiki kubwa,
hivyo kwamba watatembea kama vipofu.
Damu yao itamwagwa kama vumbi,
na miili yao kama mavi.
18Fedha yao wala dhahabu yao havitaweza kuwaokoa
katika siku hiyo ya ghadhabu ya Mwenyezi-Mungu.
Kwa moto wa wivu wake
dunia yote itateketezwa.
Kwa ukamilifu na kwa namna ya kutisha
atawafanya wakazi wote duniani watoweke.