The chat will start when you send the first message.
1Daudi akawaita maafisa wote wa Israeli wakusanyike huko Yerusalemu: yaani maafisa walio juu ya makabila, majemadari wa vikosi katika utumishi wa mfalme, majemadari wa maelfu na majemadari wa mamia, maafisa wanaosimamia mali yote na mifugo ya mfalme na wanawe, wakiwemo maafisa wa jumba la kifalme, mashujaa na wapiganaji hodari wote.
2Mfalme Daudi akainuka na kusema: “Nisikilizeni ndugu zangu, nanyi watu wangu. Nilikuwa na nia ya kujenga nyumba ili iwe mahali pa kukaa Sanduku la Agano la Bwana , kwa ajili ya kuwa mahali pa kuwekea miguu ya Mungu wetu, nami nikafanya maandalizi ya kuijenga.
3Lakini Mungu akaniambia, ‘Wewe hutajenga nyumba kwa Jina langu, kwa sababu wewe umekuwa mtu wa vita na umemwaga damu.’
4“Hata hivyo, Bwana , Mungu wa Israeli, alinichagua mimi kutoka jamaa zangu wote niwe mfalme juu ya Israeli milele. Alimchagua Yuda kuwa kiongozi, na kutoka nyumba ya Yuda akaichagua jamaa yangu, na kutoka wana wa baba yangu ikampendeza kunifanya niwe mfalme juu ya Israeli yote.
5Miongoni mwa wanangu wote, naye Bwana amenipa wengi, amemchagua Sulemani mwanangu ili kukikalia kiti cha utawala cha ufalme wa Bwana juu ya Israeli.
6Aliniambia, ‘Sulemani mwanao ndiye atakayejenga nyumba yangu na nyua zangu, kwa maana nimemchagua yeye kuwa mwanangu, nami nitakuwa baba yake.
7Nitauimarisha ufalme wake milele kama akiendelea kuzishika amri zangu na sheria zangu, kama afanyavyo hivi leo.’
8“Hivyo basi ninawaagiza mbele za Israeli yote na kusanyiko hili la Bwana , naye Mungu wetu akiwa anasikia: Kuweni na bidii kuzifuata amri za Bwana Mungu wenu, ili mpate kumiliki nchi hii nzuri, na kuwaachia wana wenu kuwa urithi milele.
9“Nawe Sulemani mwanangu, mjue Mungu wa baba yako, ukamtumikie kwa kujitoa kwa moyo wote na kwa nia ya kumkubali, kwa maana Bwana huuchunguza kila moyo na kujua kila kusudi la kila fikira. Ukimtafuta, ataonekana kwako; bali ukimwacha, yeye atakukataa milele.
10Angalia basi, kwa maana Bwana amekuchagua wewe ili ujenge Hekalu kuwa mahali patakatifu. Uwe hodari ukafanye kazi hiyo.”
11Ndipo Daudi akampa Sulemani mwanawe kielelezo kwa ajili ya ukumbi wa Hekalu, nyumba zake, vyumba vyake vya hazina, ghorofa zake, vyumba vyake vya ndani na mahali pa kufanyia upatanisho.
12Akampa vielelezo vya yote ambayo Roho alikuwa ameviweka moyoni mwake kwa ajili ya kumbi za Hekalu la Bwana na vyumba vyote vilivyolizunguka, kwa ajili ya hazina za Hekalu la Mungu na kwa hazina za vitu vilivyowekwa wakfu.
13Mfalme pia akampa Sulemani maelekezo kwa ajili ya migawanyo ya huduma za makuhani na Walawi, pia kwa ajili ya kazi zote za huduma katika Hekalu la Bwana . Akampa pia maelezo kuhusu vifaa vyote vya kutumika katika huduma ya Hekalu.
14Akamwagizia uzito wa dhahabu kwa ajili ya vitu vyote vya dhahabu vya kutumika katika huduma mbalimbali, uzito wa fedha kwa ajili ya vitu vyote vya fedha vya kutumika katika huduma mbalimbali.
15Uzito wa dhahabu kwa ajili ya vinara vya dhahabu na taa zake, kukiwa na uzito kwa ajili ya kila kinara na taa zake, pamoja na uzito wa fedha kwa ajili ya kila kinara cha fedha na taa zake, kulingana na matumizi ya kila kinara;
16uzito wa dhahabu kwa ajili ya meza ya mikate iliyowekwa wakfu, uzito wa fedha kwa ajili ya meza ya fedha;
17uzito wa dhahabu safi kwa ajili ya nyuma, mabakuli ya kunyunyizia na vikombe, masinia; uzito wa dhahabu kwa ajili ya kila bakuli la dhahabu; uzito wa fedha kwa ajili ya kila bakuli la fedha;
18na uzito wa dhahabu safi kwa ajili ya madhabahu ya kufukizia uvumba. Pia alimpa kielelezo kwa ajili ya gari la vita, yaani wale makerubi wa dhahabu waliokunjua mabawa yao na kutia kivuli juu ya Sanduku la Agano la Bwana .
19Daudi akasema, “Hii yote, ninayo kwa maandishi kutoka mkononi mwa Bwana ulio juu yangu, naye amenipa ufahamu kwa ajili ya habari zote za kielelezo hiki.”
20Daudi pia akamwambia Sulemani mwanawe, “Uwe hodari na moyo mkuu, ukafanye kazi hii. Usiogope wala usifadhaike, kwa maana Bwana Mungu, aliye Mungu wangu, yu pamoja nawe. Hatakuacha wala hatakupungukia, hadi kazi hii yote kwa ajili ya utumishi wa Hekalu la Bwana itakapokamilika.
21Migawanyo ya makuhani na Walawi iko tayari kwa ajili ya kazi yote katika Hekalu la Mungu, naye kila mtu mwenye moyo wa kujitolea, aliye na ustadi katika aina yoyote ya ufundi, atakusaidia katika kazi yote. Maafisa na watu wote watatii kila agizo lako.”