The chat will start when you send the first message.
1Ndipo Mfalme Daudi akawaambia kusanyiko lote: “Mwanangu Sulemani, yeye ambaye Mungu amemchagua, ni kijana mdogo na asiye na uzoefu. Kazi hii ni kubwa, kwa sababu Hekalu hili la fahari si kwa ajili ya mwanadamu bali ni kwa ajili ya Bwana Mungu.
2Kwa uwezo wangu wote nimetenga mali kwa ajili ya Hekalu la Mungu wangu: dhahabu kwa kazi za dhahabu, fedha kwa ajili ya fedha, shaba kwa kazi za shaba, chuma kwa kazi za chuma na miti kwa kazi za miti, vivyo hivyo vito vya shohamu kwa ajili ya kutia kwenye vijalizo, almasi, mawe ya rangi mbalimbali, aina zote za vito vya thamani na marumaru; haya yote kwa wingi mno.
3Zaidi ya hayo, kwa kujitolea kwangu kwa ajili ya Hekalu la Mungu wangu, sasa ninatoa hazina zangu mwenyewe za dhahabu na fedha kwa ajili ya Hekalu la Mungu wangu, zaidi ya mali niliyotoa kwa ajili ya Hekalu hili takatifu:
4talanta elfu tatu za dhahabu (dhahabu ya Ofiri), na talanta elfu saba za fedha safi iliyosafishwa, kwa ajili ya kufunika kuta za Hekalu,[#29:4 Talanta 3,000 ni sawa na tani 110.; #29:4 Talanta 7,000 ni sawa na tani 260.]
5kwa kazi ya dhahabu na kazi ya fedha na kwa kazi yote itakayofanywa na mafundi. Basi, ni nani anayependa kujitoa kwa Bwana leo?”
6Ndipo viongozi wa jamaa, maafisa wa makabila ya Israeli, majemadari wa maelfu na majemadari wa mamia, pamoja na maafisa waliokuwa wasimamizi wa kazi za mfalme wakatoa kwa hiari.
7Wakatoa kwa ajili ya kazi ya Hekalu la Mungu talanta elfu tano na darkoni elfu kumi za dhahabu, talanta elfu kumi za fedha, talanta elfu kumi na nane za shaba, na talanta elfu mia moja za chuma.[#29:7 Talanta 5,000 ni sawa na tani 190.; #29:7 Darkoni 10,000 ni sawa na kilo 84.; #29:7 Talanta 10,000 ni sawa na tani 375.; #29:7 Talanta 18,000 ni sawa na tani 675.; #29:7 Talanta 100,000 ni sawa na tani 3,750.]
8Kila mmoja aliyekuwa na vito vya thamani akavitoa katika hazina ya Hekalu la Bwana , chini ya uangalizi wa Yehieli Mgershoni.
9Watu wakafurahi kwa sababu ya itikio la hiari la viongozi wao, kwa kuwa walikuwa wametoa kwa hiari na kwa moyo wote kwa Bwana . Mfalme Daudi pia akafurahi sana.
10Daudi akamhimidi Bwana mbele ya kusanyiko lote, akisema:
“Uhimidiwe wewe, Ee Bwana ,
Mungu wa Israeli baba yetu,
tangu milele hata milele.
11Ukuu na uweza, ni vyako, Ee Bwana ,
na utukufu na enzi na uzuri,
kwa kuwa kila kilichoko mbinguni na duniani
ni chako wewe.
Ee Bwana , ufalme ni wako;
umetukuzwa kuwa mkuu juu ya yote.
12Utajiri na heshima vyatoka kwako;
wewe ndiwe unayetawala vitu vyote.
Mikononi mwako kuna nguvu na uweza
ili kuinua na kuwapa wote nguvu,
13Sasa, Mungu wetu, tunakushukuru
na kulisifu Jina lako tukufu.
14“Lakini mimi ni nani, nao watu wangu ni nani, hata tuweze kukutolea kwa ukarimu namna hii? Vitu vyote vyatoka kwako, nasi tumekutolea tu vile vinavyotoka mkononi mwako.
15Sisi ni wageni na wapitaji machoni pako, kama walivyokuwa baba zetu wote. Siku zetu duniani ni kama kivuli, bila tumaini.
16Ee Bwana Mungu wetu, kwa wingi wote huu ambao tumekutolea kwa kujenga Hekalu kwa ajili ya Jina lako Takatifu, vimetoka mkononi mwako, navyo vyote ni mali yako.
17Ninajua, Mungu wangu, kwamba wewe huujaribu moyo na unapendezwa na unyofu. Vitu hivi vyote nimetoa kwa hiari na kwa moyo mnyofu. Nami sasa nimeona kwa furaha jinsi watu wako walio hapa kwa hiari yao walivyokutolea wewe.
18Ee Bwana , Mungu wa baba zetu Abrahamu, Isaka na Israeli, weka shauku hii ndani ya mioyo ya watu wako daima na uifanye mioyo yao iwe na uaminifu kwako.
19Nawe umpe mwanangu Sulemani kujitolea kwako kwa moyo wote ili kuzishika amri zako, masharti yako, maagizo yako na kufanya kila kitu ili kujenga Hekalu hili la fahari ambalo kwa ajili yake nimetoa.”
20Ndipo Daudi akawaambia kusanyiko lote, “Mhimidini Bwana Mungu wenu.” Hivyo wote wakamhimidi Bwana , Mungu wa baba zao. Wakasujudu, na nyuso zao zikagusa chini mbele za Bwana na mfalme.
21Siku ya pili yake, wakamtolea Bwana dhabihu na sadaka za kuteketezwa: mafahali elfu moja, kondoo dume elfu moja, na wana-kondoo dume elfu moja, pamoja na sadaka za vinywaji, na sadaka nyingine nyingi sana kwa ajili ya Israeli yote.
22Wakala na kunywa kwa furaha kubwa mbele za Bwana siku ile.
Wakamtawaza Sulemani mwana wa Daudi mara ya pili kuwa mfalme, wakampaka mafuta mbele za Bwana ili awe mfalme na Sadoki kuwa kuhani.
23Sulemani akaketi kwenye kiti cha enzi cha Bwana kuwa mfalme mahali pa Daudi baba yake. Akafanikiwa sana, na Waisraeli wote wakamtii.
24Maafisa wote na mashujaa, pamoja na wana wote wa Daudi, wakaahidi kumtii Mfalme Sulemani.
25Bwana akamtukuza sana Sulemani mbele ya Waisraeli wote na kumvika fahari ya kifalme ambayo hakuna mfalme yeyote wa Israeli kabla yake aliwahi kuwa nayo.
26Daudi mwana wa Yese alikuwa mfalme wa Israeli yote.
27Alitawala Israeli kwa miaka arobaini: huko Hebroni alitawala miaka saba, na katika Yerusalemu akatawala miaka thelathini na tatu.
28Daudi akafa akiwa mzee mwenye umri mwema, akiwa ameshiba siku, utajiri na heshima. Naye Sulemani mwanawe akawa mfalme baada yake.
29Kuhusu matukio ya utawala wa Mfalme Daudi, kuanzia mwanzo hadi mwisho, yameandikwa katika kumbukumbu za mwonaji Samweli, na kumbukumbu za nabii Nathani na kumbukumbu za mwonaji Gadi,
30pamoja na habari zote za utawala wake, nguvu zake na matukio yaliyompata yeye, na Israeli, na falme za nchi nyingine zote.