The chat will start when you send the first message.
1Tazameni ni pendo kuu namna gani alilotupatia Baba, kwamba sisi tuitwe wana wa Mungu! Na ndivyo tulivyo. Kwa sababu hii ulimwengu haututambui, kwa kuwa haukumtambua yeye.
2Wapendwa, sasa tu wana wa Mungu, lakini bado haijadhihirika tutakavyokuwa, lakini twajua kwamba yeye atakapodhihirishwa, tutafanana naye, kwa maana tutamwona kama alivyo.
3Kila mmoja mwenye matumaini haya ndani yake hujitakasa, kama vile yeye alivyo mtakatifu.
4Kila mtu atendaye dhambi afanya uasi, kwa kuwa dhambi ni uasi.
5Lakini mwajua ya kuwa yeye alidhihirishwa ili aziondoe dhambi, wala ndani yake hamna dhambi.
6Kila mtu akaaye ndani yake hatendi dhambi. Kila mtu atendaye dhambi hakumwona yeye wala hakumtambua.
7Watoto wapendwa, mtu yeyote asiwadanganye. Kila mtu atendaye haki ana haki, kama yeye alivyo na haki.
8Yeye atendaye dhambi ni wa ibilisi, kwa sababu ibilisi amekuwa akitenda dhambi tangu mwanzo. Kwa kusudi hili Mwana wa Mungu alidhihirishwa, ili aziangamize kazi za ibilisi.
9Yeyote aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, kwa sababu uzao wa Mungu wakaa ndani yake, wala hawezi kutenda dhambi kwa sababu amezaliwa na Mungu.
10Kwa jinsi hii tunaweza kujua dhahiri watoto wa Mungu na pia watoto wa ibilisi. Yeyote asiyetenda haki hatokani na Mungu, wala yeye asiyempenda ndugu yake.
11Hili ndilo neno mlilolisikia tangu mwanzo: Kwamba imetupasa tupendane sisi kwa sisi.
12Msiwe kama Kaini aliyekuwa wa yule mwovu akamuua ndugu yake. Basi kwa nini alimuua? Ni kwa sababu matendo yake Kaini yalikuwa mabaya na ya ndugu yake yalikuwa ya haki.
13Ndugu zangu, ninyi msistaajabu kama ulimwengu ukiwachukia.
14Sisi tunajua kwamba tumepita mautini kuingia uzimani, kwa sababu tunawapenda ndugu. Kila asiyempenda ndugu yake akaa mautini.
15Yeyote amchukiaye ndugu yake ni muuaji, nanyi mwajua kwamba muuaji hana uzima wa milele ndani yake.
16Kwa namna hii twaweza kulijua pendo la Mungu: Kwa sababu Yesu Kristo aliutoa uhai wake kwa ajili yetu. Nasi imetupasa kuutoa uhai kwa ajili ya hao ndugu.
17Ikiwa mtu anavyo vitu vya ulimwengu huu na akamwona ndugu yake ni mhitaji lakini asimhurumie, upendo wa Mungu wakaaje ndani ya mtu huyo?
18Watoto wapendwa, tusipende kwa maneno au kwa ulimi bali kwa tendo na kweli.
19Basi hivi ndivyo tutakavyoweza kujua ya kuwa sisi tu wa kweli na hivyo twaithibitisha mioyo yetu mbele za Mungu
20kila mara mioyo yetu inapotuhukumu. Kwa maana Mungu ni mkuu kuliko mioyo yetu, naye anajua kila kitu.
21Wapendwa, kama mioyo yetu haituhukumu, tunao ujasiri mbele za Mungu,
22lolote tuombalo, twalipokea kutoka kwake, kwa sababu tumezitii amri zake na kutenda yale yanayompendeza.
23Hii ndiyo amri yake: kwamba tuliamini Jina la Mwanawe, Yesu Kristo, na kupendana sisi kwa sisi kama yeye alivyotuamuru.
24Wale wote wanaozishika amri zake hukaa ndani yake na yeye ndani yao. Hivi ndivyo tunavyojua kwamba anakaa ndani yetu. Nasi twajua hili kupitia kwa Roho yule aliyetupatia.