1 Wafalme 14

1 Wafalme 14

Unabii wa Ahiya dhidi ya Yeroboamu

1Wakati ule, Abiya mwana wa Yeroboamu akaugua,

2naye Yeroboamu akamwambia mke wake, “Nenda ukajibadilishe, ili watu wasijue kwamba wewe ni mke wa Yeroboamu. Kisha uende Shilo. Nabii Ahiya, yule aliyeniambia kuwa nitakuwa mfalme wa watu hawa, yuko huko.

3Chukua mikate kumi, maandazi kadhaa na gudulia la asali na umwendee. Atakuambia kitakachotokea kwa kijana.”

4Basi mke wa Yeroboamu akafanya kama mumewe alivyosema, akaenda kwenye nyumba ya Ahiya huko Shilo.

Wakati huu Ahiya alikuwa kipofu naye alishindwa kuona kwa sababu ya umri wake.

5Lakini Bwana alikuwa amemwambia Ahiya, “Mke wa Yeroboamu anakuja kukuuliza kuhusu mwanawe, kwa kuwa ni mgonjwa, nawe utamjibu hivi na hivi. Atakapowasili, atajifanya kuwa ni mtu mwingine.”

6Hivyo, Ahiya aliposikia kishindo cha hatua zake mlangoni, akasema, “Karibu ndani, mke wa Yeroboamu. Kwa nini unajifanya kuwa si wewe? Nimetumwa kwako kukupa habari mbaya.

7Nenda, ukamwambie Yeroboamu kwamba hivi ndivyo asemavyo Bwana , Mungu wa Israeli: ‘Nilikuinua miongoni mwa watu na kukufanya mtawala wa watu wangu Israeli.

8Nikararua ufalme kutoka kwa nyumba ya Daudi na kukupa wewe, lakini hukuwa kama mtumishi wangu Daudi, ambaye aliyashika maagizo yangu na kunifuata kwa moyo wake wote, akifanya tu lile lililokuwa sawa machoni pangu.

9Umefanya maovu mengi kuliko wote waliokutangulia. Umejitengenezea miungu mingine, sanamu za chuma, umenighadhibisha na kunigeuka.

10“ ‘Kwa sababu hii, nitaleta maafa juu ya nyumba ya Yeroboamu. Nitakatilia mbali kutoka kwa Yeroboamu kila mzaliwa wa mwisho wa kiume katika Israeli, mtumwa au mtu huru. Nitachoma nyumba ya Yeroboamu hadi iteketee yote kama mtu anavyochoma kinyesi.

11Mbwa watawala walio wa nyumba ya Yeroboamu watakaofia ndani ya mji, na ndege wa angani watawala wale watakaofia mashambani. Bwana amenena!’

12“Lakini wewe, rudi nyumbani. Utakapofika mji wako, kijana atakufa.

13Israeli yote itamwombolezea na kumzika. Ni yeye pekee wa nyumba ya Yeroboamu atakayezikwa, kwa sababu ni yeye tu ndani ya nyumba ya Yeroboamu ambaye Bwana , Mungu wa Israeli, ameona kitu chema kwake.

14“Bwana atajiinulia mwenyewe mfalme juu ya Israeli ambaye ataikatilia mbali jamaa ya Yeroboamu. Siku hiyo itakuwa lini? Hata sasa yameanza kutokea.

15Naye Bwana ataipiga Israeli, hata iwe kama mwanzi unaoyumbayumba kwenye maji. Ataingʼoa Israeli kutoka nchi hii nzuri aliyowapa baba zao na kuwatawanya ngʼambo ya Mto, kwa sababu wamemghadhibisha Bwana kwa kutengeneza nguzo za Ashera.[#14:15 yaani Mto Frati]

16Naye atawaacha Israeli kwa sababu ya dhambi Yeroboamu alizozitenda na kuisababisha Israeli kuzitenda.”

17Kisha, mke wa Yeroboamu akainuka, akaondoka kwenda Tirsa. Mara alipokanyaga kizingiti cha mlango, kijana akafa.

18Wakamzika na Israeli yote ikamwombolezea, kama Bwana alivyokuwa amesema kupitia kwa mtumishi wake, nabii Ahiya.

19Matukio mengine ya utawala wa Yeroboamu, vita vyake na jinsi alivyotawala, vimeandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli.

20Yeroboamu akawatawala kwa miaka ishirini na mbili, kisha akalala na baba zake. Naye Nadabu mwanawe akawa mfalme baada yake.

Rehoboamu mfalme wa Yuda

(2Nya 11:5–12:15)

21Rehoboamu mwana wa Sulemani alikuwa mfalme wa Yuda. Alikuwa na umri wa miaka arobaini na moja alipoanza kuwa mfalme, naye akatawala miaka kumi na saba huko Yerusalemu, mji ambao Bwana alikuwa ameuchagua miongoni mwa makabila yote ya Israeli ili apate kuliweka humo Jina lake. Mama yake aliitwa Naama, na alikuwa Mwamoni.

22Yuda wakatenda maovu machoni pa Bwana . Kwa dhambi walizotenda wakachochea hasira yake yenye wivu kuliko baba zao walivyofanya.

23Pia wakajijengea mahali pa juu pa kuabudia, mawe ya kuabudiwa, na nguzo za Ashera juu ya kila kilima kilichoinuka na kila mti uliotanda.

24Kulikuwa na hata mahanithi wa mahali pa ibada za sanamu katika nchi. Watu wakajiingiza katika kutenda machukizo ya mataifa ambayo Bwana aliyafukuza mbele ya Waisraeli.

25Katika mwaka wa tano wa utawala wa Mfalme Rehoboamu, Shishaki mfalme wa Misri akashambulia Yerusalemu.

26Akachukua hazina za Hekalu la Bwana na hazina za jumba la kifalme. Akachukua kila kitu, pamoja na zile ngao zote za dhahabu ambazo Sulemani alikuwa amezitengeneza.

27Kwa hiyo Mfalme Rehoboamu akatengeneza ngao za shaba badala ya zile za dhahabu na kuzikabidhi kwa majemadari wa ulinzi wa zamu kwenye ingilio la jumba la mfalme.

28Kila wakati mfalme alipoenda katika Hekalu la Bwana , walinzi walizichukua hizo ngao, na baadaye walizirudisha kwenye chumba cha ulinzi.

29Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Rehoboamu na yote aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda?

30Kulikuwa na vita vinavyoendelea kati ya Rehoboamu na Yeroboamu.

31Naye Rehoboamu akalala na baba zake, na akazikwa pamoja nao katika Mji wa Daudi. Mama yake aliitwa Naama; alikuwa Mwamoni. Naye Abiya mwanawe akawa mfalme baada yake.[#14:31 au Abiyamu]

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.