The chat will start when you send the first message.
1Baada ya muda mrefu, katika mwaka wa tatu, neno la Bwana likamjia Eliya kusema, “Nenda ukajioneshe kwa Ahabu nami nitaleta mvua juu ya nchi.”
2Kwa hiyo Eliya akaenda kujionesha kwa Ahabu.
Wakati huo njaa ilikuwa kali sana katika Samaria,
3naye Ahabu alikuwa amemwita Obadia aliyekuwa msimamizi wa jumba la mfalme. (Obadia alimcha Bwana sana.
4Yezebeli alipokuwa akiwaua manabii wa Bwana , Obadia alikuwa amewachukua manabii mia moja na kuwaficha katika mapango mawili, hamsini kwenye kila moja, na akawa akiwapa chakula na maji.)
5Ahabu alikuwa amemwambia Obadia, “Nenda katika nchi yote kwenye vijito vyote na mabonde. Huenda tunaweza kupata majani ya kuwalisha farasi na nyumbu ili wapate kuishi, tusilazimike kumuua hata mmoja wa wanyama wetu.”
6Kwa hiyo wakagawanya nchi waliyokusudia kutafuta majani, Ahabu akaenda upande mmoja na Obadia upande mwingine.
7Obadia alipokuwa akitembea njiani, Eliya akakutana naye. Obadia akamtambua, akasujudu, uso wake ukigusa chini, na kusema, “Je, hivi kweli ni wewe, bwana wangu Eliya?”
8Eliya akamjibu, “Ndiyo, nenda ukamwambie bwana wako, ‘Eliya yuko hapa.’ ”
9Obadia akamuuliza, “Ni kosa gani nimefanya, hata ukaamua kumkabidhi mtumishi wako mkononi mwa Ahabu ili aniue?
10Hakika kama Bwana Mungu wako aishivyo, hakuna taifa hata moja au ufalme ambapo bwana wangu hajamtuma mtu kukutafuta. Kila wakati taifa au ufalme walipodai kwamba haupo huko, aliwafanya waape kwamba hawakuweza kukupata.
11Lakini sasa unaniambia niende kwa bwana wangu na kusema, ‘Eliya yuko hapa.’
12Sijui ni wapi Roho wa Bwana ataamua kukupeleka wakati nitakapokuacha. Nikienda kumwambia Ahabu na asikupate, ataniua; lakini mimi mtumishi wako nimekuwa nikimwabudu Bwana tangu ujana wangu.
13Je, hukusikia, bwana wangu, nilifanya nini Yezebeli alipokuwa akiua manabii wa Bwana ? Niliwaficha manabii wa Bwana mia moja katika mapango mawili, hamsini katika kila moja, na nikawapatia chakula na maji.
14Nawe sasa unaniambia niende kwa bwana wangu na kumwambia, ‘Eliya yuko hapa.’ Yeye ataniua!”
15Eliya akasema, “Kama Bwana wa majeshi aishivyo, yeye ninayemtumikia, hakika nitajionesha kwa Ahabu leo.”
16Basi Obadia akaenda kukutana na Ahabu na kumwambia; naye Ahabu akaenda kukutana na Eliya.
17Ahabu alipomwona Eliya, akamwambia, “Je, ni wewe, mtaabishaji wa Israeli?”
18Eliya akamjibu, “Mimi sijaitaabisha Israeli. Lakini wewe na jamaa ya baba yako ndio mnaofanya hivyo. Mmeziacha amri za Bwana na mkafuata Mabaali.
19Sasa waite watu kutoka Israeli yote tukutane nao juu ya Mlima Karmeli. Nawe uwalete hao manabii wa Baali mia nne na hamsini na hao manabii mia nne wa Ashera, walao chakula mezani mwa Yezebeli.”
20Ndipo Ahabu akatuma ujumbe katika Israeli yote na kuwakusanya manabii hao juu ya Mlima Karmeli.
21Eliya akasimama mbele ya watu na kusema, “Mtayumbayumba katikati ya mawazo mawili hadi lini? Ikiwa Bwana ndiye Mungu, mfuateni yeye; lakini ikiwa Baali ni Mungu, basi mfuateni yeye.”
Lakini watu hawakusema kitu.
22Kisha Eliya akawaambia, “Ni mimi peke yangu nabii wa Bwana aliyebaki, lakini Baali ana manabii mia nne na hamsini.
23Leteni mafahali wawili. Wao na wajichagulie mmoja, wamkate vipande vipande na wamweke juu ya kuni, lakini wasimwashie moto. Nitamwandaa huyo fahali mwingine na kumweka juu ya kuni, lakini sitamwashia moto.
24Kisha mliitie jina la mungu wenu, nami nitaliitia jina la Bwana Mungu yule ambaye atajibu kwa moto, huyo ndiye Mungu.”
Kisha watu wote wakasema, “Hilo unalosema ni jema.”
25Eliya akawaambia manabii wa Baali, “Chagueni mmoja kati ya hawa mafahali na mwe wa kwanza kumwandaa, kwa kuwa ninyi mko wengi sana. Liitieni jina la mungu wenu, lakini msiwashe moto.”
26Kwa hiyo wakamchukua yule fahali waliyepewa, nao wakamwandaa.
Kisha wakaliitia jina la Baali kutoka asubuhi hadi adhuhuri, wakapiga kelele, “Ee Baali, utujibu!” Lakini hapakuwa na jibu; hakuna aliyejibu. Nao wakacheza kuizunguka madhabahu waliyoijenga.
27Wakati wa adhuhuri, Eliya akaanza kuwadhihaki, akisema, “Pigeni kelele zaidi! Hakika yeye ni mungu! Labda amezama katika mawazo mazito, au ana shughuli nyingi, au amesafiri. Labda amelala usingizi mzito, naye ni lazima aamshwe.”
28Kwa hiyo wakapiga kelele zaidi na kama ilivyokuwa desturi yao wakajichanja kwa visu na vyembe, hadi damu ikachuruzika.
29Adhuhuri ikapita, nao wakaendelea na utabiri wao wa kiwazimu hadi wakati wa dhabihu ya jioni. Lakini hapakuwa na itikio, hakuna aliyejibu, na hakuna aliyezingatia.
30Kisha Eliya akawaambia watu wote, “Sogeeni karibu nami.” Wakamkaribia, naye akaikarabati madhabahu ya Bwana , iliyokuwa imeharibiwa.
31Eliya akachukua mawe kumi na mbili, moja kwa ajili ya kila kabila la wana wa Yakobo, ambaye neno la Bwana lilimjia, kusema, “Jina lako litakuwa Israeli.”
32Kwa mawe hayo, akajenga madhabahu katika jina la Bwana , na akachimba handaki kuizunguka, ukubwa wa kutosha vipimo viwili vya mbegu.
33Akapanga kuni, akamkata yule fahali vipande vipande na kuvipanga juu ya kuni. Kisha akawaambia, “Jazeni mapipa manne maji na kuyamwaga juu ya sadaka ya kuteketezwa na juu ya kuni.”
34Akawaambia, “Fanyeni hivyo tena.” Nao wakafanya hivyo tena.
Akaagiza, “Fanyeni kwa mara ya tatu.” Nao wakafanya hivyo kwa mara ya tatu.
35Maji yakatiririka kuizunguka madhabahu na hata kujaza lile handaki.
36Wakati wa kutoa dhabihu ya jioni, nabii Eliya akasogea mbele na kuomba, akisema: “Ee Bwana , Mungu wa Abrahamu, na Isaka na Israeli, ijulikane leo kwamba wewe ndiwe Mungu katika Israeli, na kwamba mimi ni mtumishi wako na nimefanya mambo haya yote kama ulivyoagiza.
37Unijibu, Ee Bwana ! Unijibu ili watu hawa wajue kuwa wewe, Ee Bwana , ndiwe Mungu, na kwamba unaigeuza mioyo yao ikurudie tena.”
38Kisha moto wa Bwana ukashuka na kuiteketeza ile dhabihu, zile kuni, yale mawe, ule udongo, na pia kuramba yale maji yaliyokuwa ndani ya handaki.
39Watu wote walipoona hili, wakaanguka kifudifudi na kulia, “Bwana : yeye ndiye Mungu! Bwana : yeye ndiye Mungu!”
40Kisha Eliya akawaamuru, “Wakamateni hao manabii wa Baali. Msimwache hata mmoja atoroke!” Wakawakamata, naye Eliya akawaleta Bonde la Kishoni na kuwachinja huko.
41Eliya akamwambia Ahabu, “Nenda, ukale na kunywa, kwa kuwa kuna sauti ya mvua kubwa.”
42Hivyo Ahabu akaondoka ili kula na kunywa. Lakini Eliya akapanda kileleni mwa Karmeli, akainama hadi chini, na kuweka kichwa chake katikati ya magoti.
43Akamwambia mtumishi wake, “Nenda ukatazame kuelekea bahari.” Akaenda na kutazama.
Akasema, “Hakuna kitu chochote huko.”
Mara saba Eliya akasema, “Nenda tena.”
44Mara ya saba, mtumishi akaleta taarifa, “Wingu dogo kama mkono wa mwanadamu linainuka kutoka baharini.”
Hivyo Eliya akasema, “Nenda ukamwambie Ahabu, ‘Tandika gari lako la vita, ushuke kabla mvua haijakuzuia.’ ”
45Wakati ule ule anga likawa jeusi kwa mawingu, upepo ukainuka na mvua kubwa ikanyesha, naye Ahabu akaenda zake Yezreeli.
46Nguvu za Bwana zikamjia Eliya, naye akajikaza viuno, akakimbia mbele ya Ahabu njia yote hadi ingilio la Yezreeli.