1 Samweli 30

1 Samweli 30

Daudi aangamiza Waamaleki

1Daudi na watu wake wakafika Siklagi siku ya tatu. Basi Waamaleki walikuwa wamevamia Negebu na Siklagi. Wakawa wameshambulia mji wa Siklagi na kuuteketeza kwa moto,

2nao wakawa wamewachukua mateka wanawake pamoja na wote waliokuwamo humo, vijana na wazee. Hawakumuua yeyote, bali waliwachukua wakaenda zao.

3Daudi na watu wake walipofika Siklagi, wakakuta mji umeangamizwa kwa moto na wake zao pamoja na wana wao wa kiume na wa kike wamechukuliwa mateka.

4Hivyo Daudi na watu wake wakapaza sauti na kulia hadi wakaishiwa na nguvu za kulia.

5Wake wawili wa Daudi walikuwa wametekwa: yaani Ahinoamu wa Yezreeli, na Abigaili, mjane wa Nabali wa Karmeli.

6Daudi alihuzunika sana kwa sababu watu walikuwa wakisemezana kuhusu kumpiga kwa mawe. Kila mmoja alikuwa na uchungu rohoni kwa sababu ya wanawe wa kiume na wa kike. Lakini Daudi akajitia nguvu katika Bwana , Mungu wake.

7Kisha Daudi akamwambia kuhani Abiathari mwana wa Ahimeleki, “Niletee kizibau.” Abiathari akamletea,

8naye Daudi akamuuliza Bwana , “Je, nifuatie kundi hili la wavamizi? Je, nitawapata?”

Bwana akajibu, “Wafuatie. Hakika utawapata na utafanikiwa kuwaokoa.”

9Daudi pamoja na watu wake mia sita wakafika kwenye Bonde la Besori, ambapo wengine waliachwa nyuma,

10kwa kuwa watu mia mbili walikuwa wamechoka sana kuweza kuvuka hilo bonde. Lakini Daudi pamoja na watu mia nne wakaendelea kufuatia.

11Wakamkuta Mmisri katika shamba fulani, nao wakamleta kwa Daudi. Wakampa huyo Mmisri maji ya kunywa na chakula;

12kipande cha andazi la tini na andazi la zabibu zilizokaushwa. Akala naye akapata nguvu, kwa kuwa hakuwa amekula chakula chochote wala kunywa maji kwa siku tatu usiku na mchana.

13Daudi akamuuliza, “Wewe ni wa nani, na umetoka wapi?”

Akajibu, “Mimi ni Mmisri, mtumwa wa Mwamaleki. Bwana wangu alinitelekeza nilipougua siku tatu zilizopita.

14Tulivamia Negebu ya Wakerethi, na nchi ya Yuda, na Negebu ya Kalebu. Nasi tulichoma moto Siklagi.”

15Daudi akamuuliza, “Je, unaweza kuniongoza kufikia kundi hili la uvamizi?”

Akajibu, “Niapie mbele ya Mungu kwamba hutaniua wala kunikabidhi mikononi mwa bwana wangu, nami nitakupeleka hadi waliko.”

16Akamwongoza Daudi hadi mahali walipokuwa, nao walikuwa wametawanyika eneo lote, wakila, wakinywa na wakifanya karamu kwa sababu ya nyara nyingi walizochukua kutoka nchi ya Wafilisti na kutoka Yuda.

17Daudi akapigana nao kuanzia machweo ya jua hadi kesho yake jioni, na hakuna yeyote miongoni mwao aliyetoroka, isipokuwa vijana mia nne waliopanda ngamia na kutoroka.

18Daudi akarudisha kila kitu ambacho Waamaleki walikuwa wamechukua, pamoja na wake zake wawili.

19Hakuna chochote kilichopotea: kijana au mzee, mvulana au msichana, nyara au kitu kingine chochote walichokuwa wamechukua. Daudi akarudisha kila kitu.

20Akachukua makundi yote ya kondoo, mbuzi na ngʼombe, nao watu wake wakawaswaga wanyama hao mbele ya mifugo wengine, wakisema, “Hizi ni nyara za Daudi.”

21Kisha Daudi akafika kwa wale watu mia mbili waliokuwa wamechoka sana kumfuata na ambao waliachwa nyuma kwenye Bonde la Besori. Wakatoka kwenda kumlaki Daudi na wale watu aliokuwa nao. Daudi na watu wake walipowakaribia, akawasalimu.

22Lakini watu wote waovu na wakorofi miongoni mwa wafuasi wa Daudi wakasema, “Kwa sababu hawakuenda pamoja nasi, hatutagawana nao nyara tulizorudisha. Lakini, kila mtu aweza kuchukua mkewe na watoto wake na kuondoka.”

23Daudi akajibu, “La, ndugu zangu, kamwe hamwezi kufanya hivyo kwa kile ambacho Bwana ametupatia. Yeye ametulinda na kuweka mikononi mwetu majeshi yale yaliyokuja kupigana dhidi yetu.

24Ni nani atasikiliza yale mnayosema? Fungu la mtu aliyekaa na vyombo litakuwa sawa na la yule aliyeenda vitani. Wote watashiriki sawa.”

25Daudi akafanya hili liwe amri na agizo kwa Israeli kutoka siku ile hata leo.

26Daudi alipofika Siklagi, akatuma baadhi ya nyara kwa wazee wa Yuda, waliokuwa rafiki zake, akasema, “Tazama, hapa kuna zawadi kwa ajili yenu kutoka nyara za adui za Bwana .”

27Akazituma kwa wale waliokuwa Betheli, Ramoth-Negebu na Yatiri;

28kwa wale walio Aroeri, Sifmothi, Eshtemoa

29na Rakali; kwa wale waliokuwa katika miji ya Wayerameeli na ya Wakeni;

30na kwa wale walio Horma, Bori-Ashani, Athaki,

31na kwa wakazi wa Hebroni; na kwa wale waliokuwa mahali pengine pote ambako Daudi na watu wake walitembelea.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.