1 Timotheo 3

1 Timotheo 3

Sifa za waangalizi

1Hili ni neno la kuaminiwa, kwamba mtu akitamani kuwa askofu, atamani kazi nzuri.[#3:1 yaani mwangalizi wa kanisa]

2Basi, imempasa askofu awe mtu asiye na lawama, mume wa mke mmoja, mwenye kiasi, anayejitawala, anayeheshimika, mkarimu, ajuaye kufundisha,

3asiwe mlevi, wala mkali bali awe mpole, asiwe mgomvi wala mpenda fedha.

4Lazima aweze kuisimamia nyumba yake mwenyewe vizuri na kuhakikisha kwamba watoto wake wanamtii na kuwa na heshima kwa kila njia.

5(Kwa maana kama mtu hajui jinsi ya kusimamia nyumba yake mwenyewe, atawezaje kuliangalia kanisa la Mungu?)

6Asiwe mtu aliyeongoka karibuni asije akajivuna na kuangukia kwenye hukumu ile ile ya ibilisi.

7Inampasa pia awe na sifa njema kwa watu walio nje, ili asije akalaumiwa na kuanguka kwenye mtego wa ibilisi.

Sifa za mashemasi

8Vivyo hivyo, mashemasi nao wawe watu wanaostahili heshima, wasiwe wenye kauli mbili au wenye kujifurahisha kwa mvinyo, wala wanaotamani faida isiyo halali.[#3:8 yaani watumishi wa kanisa ; walisaidia kutoa huduma kwa waumini kwa njia mbalimbali]

9Inawapasa kushikamana sana na ile siri ya imani kwa dhamiri safi.

10Ni lazima wapimwe kwanza; kisha kama hakuna neno dhidi yao, basi na waruhusiwe kuhudumu kama mashemasi.

11Vivyo hivyo, wake zao wawe wanawake wanaostahili heshima, wasio wasingiziaji, bali wawe na kiasi na waaminifu katika kila jambo.

12Shemasi awe mume wa mke mmoja, na aweze kusimamia watoto wake na watu wa nyumbani mwake vyema.

13Wale ambao wamehudumu vyema katika huduma ya ushemasi hujipatia msimamo bora na ujasiri mkubwa katika imani yao ndani ya Kristo Yesu.

14Ingawa ninatarajia kuja kwako hivi karibuni, ninakuandikia maagizo haya sasa ili,

15nikikawia, utajua jinsi iwapasavyo watu kuenenda katika nyumba ya Mungu, ambayo ndiyo kanisa la Mungu aliye hai, lililo nguzo na msingi wa kweli.

16Bila shaka yoyote, siri ya utauwa ni kubwa:

Alidhihirishwa katika mwili,

akathibitishwa kuwa na haki katika Roho,

akaonekana na malaika,

akahubiriwa miongoni mwa mataifa,

akaaminiwa ulimwenguni,

akachukuliwa juu katika utukufu.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.