2 Nyakati 10

2 Nyakati 10

Waisraeli wamwasi Rehoboamu

(1Fal 12:1‑20)

1Rehoboamu akaenda Shekemu, kwa kuwa Waisraeli wote walikuwa wameenda huko kumfanya mfalme.

2Yeroboamu mwana wa Nebati aliposikia hili (alikuwa bado yuko Misri alikokuwa amekimbilia awe mbali na Mfalme Sulemani), akarudi kutoka Misri.

3Kwa hiyo wakatuma watu kumwita Yeroboamu; yeye na Waisraeli wote wakamwendea Rehoboamu na kumwambia,

4“Baba yako aliweka nira nzito juu yetu, lakini sasa tupunguzie kazi za kikatili na nira nzito aliyoweka juu yetu, nasi tutakutumikia.”

5Rehoboamu akajibu, “Nendeni kwa muda wa siku tatu na kisha mnirudie.” Basi watu wakaenda zao.

6Kisha Mfalme Rehoboamu akataka ushauri kwa wazee ambao walimtumikia Sulemani baba yake wakati wa uhai wake akawauliza, “Mnanishauri niwajibu nini watu hawa?”

7Wakajibu, “Kama leo utakuwa mtumishi wa watu hawa na kuwahudumia na kuwapa jibu linaloridhisha, watakuwa watumishi wako daima.”

8Lakini Rehoboamu akakataa ushauri aliopewa na wazee, na akataka ushauri kwa vijana wa rika lake waliokuwa wakimtumikia.

9Akawauliza, “Ninyi ushauri wenu ni nini? Tutawajibuje watu hawa wanaoniambia, ‘Ifanye nyepesi nira baba yako aliyoweka juu yetu’?”

10Wale vijana wa rika lake wakamjibu, “Watu hawa walikuambia, ‘Baba yako aliweka nira nzito juu yetu, lakini ifanye nira yetu nyepesi,’ Wewe waambie, ‘Kidole changu kidogo ni kinene kuliko kiuno cha baba yangu.

11Baba yangu aliweka nira nzito juu yenu, mimi nitaifanya hata iwe nzito zaidi. Baba yangu aliwapiga mijeledi; mimi nitawapiga kwa nge.’ ”

12Siku tatu baadaye, Yeroboamu na watu wote wakamrudia Rehoboamu, kama mfalme alivyokuwa amesema, “Rudini kwangu baada ya siku tatu.”

13Mfalme akawajibu watu kwa ukatili. Alikataa ushauri aliopewa na wazee,

14akafuata ushauri wa vijana wa rika lake na kusema, “Baba yangu alifanya nira yenu kuwa nzito, mimi nitaifanya kuwa nzito zaidi. Baba yangu aliwapiga mijeledi; mimi nitawapiga kwa nge.”

15Kwa hiyo mfalme hakuwasikiliza watu, kwa kuwa jambo hili lilitoka kwa Mungu ili kutimiza neno ambalo Bwana alikuwa amenena na Yeroboamu mwana wa Nebati kupitia kwa Ahiya Mshiloni.

16Israeli wote walipoona kuwa mfalme amekataa kuwasikiliza, wakamjibu mfalme:

“Je, tuna fungu gani kwa Daudi?

Tuna urithi gani kwa mwana wa Yese?

Nendeni kwenye mahema yenu, ee Israeli,

angalia nyumba yako mwenyewe, ee Daudi!”

Hivyo Waisraeli wakaenda kwenye mahema yao.

17Lakini kwa habari ya Waisraeli walioishi katika miji ya Yuda, Rehoboamu akaendelea kuwatawala bado.

18Mfalme Rehoboamu akamtuma Adoniramu aliyekuwa msimamizi wa wale waliofanya kazi ngumu kwa kulazimishwa, lakini Israeli wote wakampiga kwa mawe hadi akafa. Hata hivyo, Mfalme Rehoboamu akafanikiwa kuingia kwenye gari lake la vita, akatorokea Yerusalemu.[#10:18 au Adoramu ; Kiebrania ni Hadoramu.]

19Hivyo, Israeli wakaasi dhidi ya nyumba ya Daudi hadi leo.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.