2 Nyakati 12

2 Nyakati 12

Shishaki ashambulia Yerusalemu

(1Fal 14:25‑28)

1Baada ya ufalme wa Rehoboamu kuimarika naye akawa na nguvu, yeye na Waisraeli wote waliiacha sheria ya Bwana .

2Kwa sababu hawakuwa waaminifu kwa Bwana , Shishaki mfalme wa Misri akashambulia Yerusalemu katika mwaka wa tano wa utawala wa Mfalme Rehoboamu.

3Akiwa na magari ya vita elfu moja mia mbili, wapanda farasi elfu sitini, na idadi isiyohesabika ya majeshi ya Walibia, Wasukii na Wakushi waliokuja pamoja naye kutoka Misri.

4Akateka miji ya Yuda yenye ngome, akaendelea hadi Yerusalemu.

5Ndipo nabii Shemaya akaja kwa Rehoboamu na kwa viongozi wa Yuda waliokuwa wamekusanyika huko Yerusalemu kwa ajili ya hofu ya Shishaki naye akawaambia, “Hivi ndivyo asemavyo Bwana , ‘Ninyi mmeniacha, kwa hiyo, mimi nami sasa ninawaacha mkononi mwa Shishaki.’ ”

6Viongozi wa Israeli na mfalme wakajinyenyekeza na kusema, “Bwana Mungu ni mwenye haki.”

7Bwana Mungu alipoona kwamba wamejinyenyekeza, neno hili la Bwana likamjia Shemaya: “Maadamu wamejinyenyekeza, sitawaangamiza, bali hivi karibuni nitawapatia wokovu. Ghadhabu yangu haitamwagwa juu ya Yerusalemu kupitia kwa Shishaki.

8Hata hivyo, watamtumikia Shishaki ili wapate kujifunza tofauti kati ya kunitumikia mimi na kuwatumikia wafalme wa nchi nyingine.”

9Shishaki mfalme wa Misri alipoishambulia Yerusalemu, alichukua hazina za Hekalu la Bwana na hazina za jumba la kifalme. Akachukua kila kitu, pamoja na zile ngao za dhahabu ambazo Sulemani alikuwa amezitengeneza.

10Kwa hiyo Mfalme Rehoboamu akatengeneza ngao za shaba badala ya zile za dhahabu na kuzikabidhi kwa majemadari wa ulinzi wa zamu kwenye ingilio la jumba la mfalme.

11Kila wakati mfalme alipoenda katika Hekalu la Bwana walinzi walienda pamoja naye wakiwa wamebeba hizo ngao na baadaye walizirudisha kwenye chumba cha ulinzi.

12Kwa sababu Rehoboamu alijinyenyekeza, hasira ya Bwana ikageukia mbali naye, hakuangamizwa kabisa. Kukawa na hali nzuri katika Yuda.

13Mfalme Rehoboamu akajiweka imara katika Yerusalemu na akaendelea kuwa mfalme. Alikuwa na umri wa miaka arobaini na moja alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miaka kumi na saba, mji ambao Bwana alikuwa ameuchagua miongoni mwa makabila yote ya Israeli ili aliweke Jina lake humo. Mama yake aliitwa Naama, na alikuwa Mwamoni.

14Rehoboamu akatenda maovu kwa sababu hakuuelekeza moyo wake katika kumtafuta Bwana Mungu.

15Kwa habari ya matukio katika utawala wa Rehoboamu, kuanzia mwanzo hadi mwisho, je, hayakuandikwa katika kumbukumbu za nabii Shemaya na mwonaji Ido zinazohusiana na vizazi? Kulikuwa na vita vya mara kwa mara kati ya Rehoboamu na Yeroboamu.

16Rehoboamu akalala na baba zake, akazikwa katika Mji wa Daudi. Naye Abiya mwanawe akawa mfalme baada yake.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.