The chat will start when you send the first message.
1Yoashi alikuwa na umri wa miaka saba alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu kwa miaka arobaini. Mama yake aliitwa Sibia aliyekuwa ametoka Beer-Sheba.
2Yoashi akafanya yaliyo mema machoni pa Bwana miaka yote ya Yehoyada kuhani.
3Yehoyada akamwoza wake wawili, akazaa watoto wa kiume na wa kike.
4Baada ya muda, Yoashi akaamua kukarabati Hekalu la Bwana .
5Akawaita pamoja makuhani na Walawi akawaambia, “Nendeni katika miji ya Yuda mkakusanye fedha wanazopaswa kulipa kila mwaka kutoka kwa Israeli wote, ili kukarabati Hekalu la Mungu wenu. Fanyeni hivyo sasa.” Lakini Walawi hawakufanya upesi.
6Kwa hiyo mfalme akamwita Yehoyada kuhani mkuu na kumwambia, “Kwa nini hukuwaambia Walawi walete kutoka Yuda na Yerusalemu kodi iliyowekwa na Musa mtumishi wa Bwana pamoja na kusanyiko la Israeli kwa ajili ya Hema la Ushuhuda?”
7Kwa kuwa wana wa yule mwanamke mwovu Athalia, walikuwa wamevunja na kuingia katika Hekalu la Mungu, nao wakawa wamevitumia hata vile vitu vilivyowekwa wakfu kwa Bwana kwa mabaali.
8Kwa amri ya mfalme, likatengenezwa kasha, nalo likawekwa nje kwenye lango la Hekalu la Bwana .
9Tangazo likatolewa katika Yuda na Yerusalemu, kwamba inapasa wamletee Bwana kodi ambayo Musa, mtumishi wa Bwana , alikuwa amewaagiza Israeli huko jangwani.
10Maafisa wote na watu wote wakaleta michango yao kwa furaha, wakaweka kwenye kasha hadi likajaa.
11Ikawa kila wakati kasha lilipoletwa ndani na Walawi kwa maafisa wa mfalme na kuona kwamba kuna kiasi kikubwa cha fedha, mwandishi wa mfalme na afisa wa kuhani mkuu walikuwa wanakuja na kumimina, kisha kulirudisha mahali pake. Walifanya hivi mara kwa mara, nao wakakusanya fedha nyingi sana.
12Mfalme na Yehoyada wakawapa wale watu waliofanya kazi iliyotakiwa katika Hekalu la Bwana . Wakawaajiri waashi na maseremala ili kutengeneza Hekalu la Bwana , pia wafanyakazi za chuma na shaba ili kukarabati Hekalu la Bwana .
13Watu walioshughulika na kazi walikuwa wenye bidii, nayo kazi ya kukarabati ikaendelea vizuri mikononi mwao. Wakalitengeneza upya Hekalu la Bwana likarudi katika hali yake ya awali, na wakaliimarisha.
14Walipokamilisha kazi hiyo ya kukarabati, wakaleta fedha zilizobaki wakampa mfalme na Yehoyada, nao kwa hizo wakatengeneza vyombo kwa ajili ya Hekalu la Bwana : Vyombo kwa ajili ya huduma na kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa, pia mabakuli na vitu vingine vya dhahabu na fedha. Wakati wote Yehoyada akiwa hai, sadaka za kuteketezwa zilitolewa wakati wote katika Hekalu la Bwana .
15Basi Yehoyada alikuwa mzee aliyeshiba siku alipofariki. Alikufa akiwa na umri wa miaka mia moja na thelathini.
16Wakamzika pamoja na wafalme katika Mji wa Daudi, kwa sababu ya mema aliyokuwa ametenda katika Israeli kwa ajili ya Mungu na Hekalu lake.
17Baada ya kifo cha Yehoyada, wakuu wa Yuda walikuja kumpa mfalme heshima, naye akawasikiliza.
18Wakaacha Hekalu la Bwana , Mungu wa baba zao, wakaabudu nguzo za maashera na sanamu. Kwa sababu ya hatia yao, hasira ya Mungu ikawajia Yuda na Yerusalemu.
19Ingawa Bwana aliwatuma manabii wawarudishe watu kwake na ingawa waliwaonya, hawakuwasikiliza.
20Ndipo Roho wa Bwana akaja juu ya Zekaria mwana wa Yehoyada kuhani. Akasimama mbele ya watu akasema, “Hili ndilo asemalo Mungu, ‘Kwa nini mnakataa kuzitii amri za Bwana ? Hamtafanikiwa kwa kuwa mmemwacha Bwana , naye amewaacha ninyi.’ ”
21Lakini wakapanga njama dhidi yake, na kwa amri ya mfalme wakampiga kwa mawe hadi akafa katika ua wa Hekalu la Bwana .
22Mfalme Yoashi hakukumbuka wema aliotendewa na Yehoyada baba yake Zekaria, ila alimuua mwanawe, ambaye alisema wakati akiwa amelala akingojea kufa, “Bwana na alione hili na alipize kisasi.”
23Mwishoni mwa ule mwaka, jeshi la Waaramu likaja dhidi ya Yoashi, likavamia Yuda na Yerusalemu na kuwaua viongozi wote wa watu. Wakapeleka nyara zao zote kwa mfalme wao huko Dameski.
24Ingawa jeshi la Waaramu lilikuwa limekuja na watu wachache tu, Bwana akatia mikononi mwao jeshi kubwa kuliko lao. Kwa sababu Yuda walikuwa wamemwacha Bwana , Mungu wa baba zao, hukumu ilitekelezwa juu ya Yoashi.
25Waaramu walipoondoka, walimwacha Yoashi akiwa mgonjwa sana. Maafisa wake wakapanga njama dhidi yake kwa sababu alikuwa amemuua mwana wa Kuhani Yehoyada, nao wakamuua kitandani mwake. Hivyo akafa, wakamzika katika Mji wa Daudi, lakini si katika makaburi ya wafalme.
26Wale waliopanga njama dhidi yake walikuwa Zabadi mwana wa Shimeathi mwanamke Mwamoni, na Yehozabadi mwana wa Shimrithi mwanamke Mmoabu.
27Kwa habari za wanawe, unabii mwingi kumhusu na kumbukumbu za kutengenezwa upya kwa Hekalu la Mungu, zimeandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme. Amazia mwanawe akawa mfalme baada yake.