2 Nyakati 25

2 Nyakati 25

Amazia mfalme wa Yuda

(2Fal 14:2‑20)

1Amazia alikuwa na umri wa miaka ishirini na tano alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu kwa miaka ishirini na tisa. Mama yake aliitwa Yehoadani kutoka Yerusalemu.

2Akatenda yaliyo mema machoni pa Bwana , lakini sio kwa moyo wake wote.

3Baada ya ufalme kuimarika mkononi mwake, aliwaua maafisa waliomuua mfalme baba yake.

4Hata hivyo hakuwaua watoto wao, lakini akafanya sawasawa na ilivyoandikwa katika Sheria, katika Kitabu cha Musa, ambako Bwana aliamuru: “Baba hawatauawa kwa ajili ya watoto wao, wala watoto hawatauawa kwa ajili ya baba zao. Kila mmoja atakufa kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe.”[#25:4 Kum 24:16]

5Amazia akawaita watu wa Yuda pamoja, akawaweka chini ya majemadari wa maelfu na majemadari wa mamia kufuatana na jamaa zao katika Yuda yote na Benyamini. Kisha akawahesabu wale wenye umri wa miaka ishirini au zaidi na akakuta kwamba walikuwa wanaume elfu mia tatu walio tayari kwa utumishi wa jeshi, wenye uwezo wa kutumia mkuki na ngao.

6Akawaajiri pia wapiganaji elfu mia moja kutoka Israeli kwa talanta mia moja za fedha.[#25:6 Talanta 100 za fedha ni sawa na tani 3.75.]

7Lakini mtu wa Mungu akamjia na kumwambia, “Ee mfalme, haya majeshi kutoka Israeli kamwe usiyaruhusu yaende pamoja na wewe, kwa kuwa Bwana hayuko pamoja na Israeli, wala hayupo pamoja na yeyote wa watu wa Efraimu.

8Hata ukienda na kupigana kwa ujasiri katika vita, Mungu atakufanya ukimbie mbele ya adui, kwa kuwa Mungu anao uwezo wa kusaidia au wa kuangusha.”

9Amazia akamuuliza yule mtu wa Mungu, “Lakini itakuwaje kwa zile talanta mia moja za fedha nilizolipa kwa ajili ya haya majeshi ya Israeli?”

Yule mtu wa Mungu akajibu, “Bwana aweza kukupa zaidi ya hizo.”

10Hivyo Amazia akayaondoa yale majeshi yaliyokuwa yamekuja kutoka Efraimu na kuyarudisha nyumbani. Waliwakasirikia sana Yuda, nao wakarudi nyumbani wakiwa na hasira kali.

11Ndipo Amazia akajitia nguvu na kuliongoza jeshi lake hadi Bonde la Chumvi, ambako aliwaua watu elfu kumi wa Seiri.

12Jeshi la Yuda pia likawateka watu elfu kumi wakiwa hai, likawapandisha juu ya jabali na kuwatupa chini kwa nguvu, wote wakavunjika vipande vipande.

13Wakati huo, wanajeshi waliorudishwa na Amazia, ambao hakuwaruhusu kushiriki katika vita, walivamia miji ya Yuda kuanzia Samaria hata Beth-Horoni. Wakawaua watu elfu tatu na kuchukua nyara nyingi sana.

14Amazia aliporudi kutoka kuwaua Waedomu, alileta pia kutoka huko miungu ya watu wa Seiri. Akaisimamisha kama miungu yake mwenyewe, akaisujudia na kuitolea sadaka za kuteketezwa.

15Hasira ya Bwana ikawaka dhidi ya Amazia, naye akamtuma nabii kwake, ambaye alisema: “Kwa nini unauliza kwa miungu ya hawa watu, ambayo haikuweza kuwaokoa watu wake wenyewe kutoka mkononi mwako?”

16Nabii alipokuwa angali anazungumza, mfalme akamwambia, “Je, wewe tumekuchagua kuwa mshauri wa mfalme? Nyamaza! Kwa nini uuawe?”

Hivyo nabii akanyamaza lakini akasema, “Najua kuwa Mungu ameazimia kukuangamiza kwa sababu umefanya jambo hili na hukusikiliza ushauri wangu.”

17Baada ya Amazia mfalme wa Yuda kushauriana na washauri wake, akatuma ujumbe kwa Yehoashi mwana wa Yehoahazi, mwana wa Yehu, mfalme wa Israeli, kusema: “Njoo tukabiliane uso kwa uso.”

18Lakini Yehoashi mfalme wa Israeli akamjibu Amazia mfalme wa Yuda, “Mbaruti uliokuwa Lebanoni ulituma ujumbe kwa mwerezi uliokuwa Lebanoni, ‘Mtoe binti yako aolewe na mwanangu.’ Kisha mnyama wa mwituni aliyekuwa Lebanoni akaja na kuukanyaga ule mbaruti.

19Wewe unasema moyoni mwako kwamba umemshinda Edomu, nawe sasa unajigamba na kujivuna. Lakini kaa nyumbani mwako! Kwa nini utafute matatizo na kujiletea anguko lako mwenyewe na la Yuda pia?”

20Hata hivyo, Amazia hakutaka kusikia, kwa kuwa Mungu alifanya hivyo ili awatie mikononi mwa Yehoashi, kwa sababu waliitafuta miungu ya Edomu.

21Hivyo Yehoashi mfalme wa Israeli akakwea kuwashambulia. Yeye na Amazia mfalme wa Yuda wakakabiliana uso kwa uso huko Beth-Shemeshi katika Yuda.

22Yuda ikashindwa na Israeli na kila mtu akakimbilia nyumbani mwake.

23Yehoashi mfalme wa Israeli akamteka Amazia mfalme wa Yuda, mwana wa Yoashi, mwana wa Ahazia, huko Beth-Shemeshi. Kisha Yehoashi akamleta Yerusalemu na kuubomoa ukuta wa Yerusalemu kuanzia lango la Efraimu hadi Lango la Pembeni, sehemu yenye urefu wa kama dhiraa mia nne.[#25:23 Dhiraa 400 ni sawa na mita 180.]

24Akachukua dhahabu yote, fedha na vyombo vyote vilivyopatikana katika Hekalu la Mungu, ambavyo vilikuwa chini ya uangalizi wa Obed-Edomu, pamoja na hazina za jumba la mfalme na mateka, kisha akarudi Samaria.

25Amazia mwana wa Yoashi mfalme wa Yuda aliishi miaka kumi na tano baada ya kifo cha Yehoashi mwana wa Yehoahazi mfalme wa Israeli.

26Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Amazia, kuanzia mwanzo hadi mwisho, je, hayakuandikwa katika kitabu cha wafalme wa Yuda na wa Israeli?

27Kuanzia wakati Amazia alipogeuka na kuacha kumfuata Bwana , walipanga njama dhidi yake huko Yerusalemu, naye akakimbilia Lakishi. Lakini wakawatuma watu wamfuatilie huko Lakishi, nao wakamuua huko.

28Akarudishwa kwa farasi, akazikwa na baba zake katika Mji wa Yuda.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.