2 Nyakati 26

2 Nyakati 26

Uzia mfalme wa Yuda

(2Fal 14:21‑22; 15:1‑7)

1Kisha watu wote wa Yuda wakamchukua Uzia, aliyekuwa na umri wa miaka kumi na sita, nao wakamfanya mfalme mahali pa Amazia baba yake.

2Ndiye aliijenga upya Elathi na kuirudisha kwa Yuda baada ya Amazia kulala na baba zake.

3Uzia alikuwa na umri wa miaka kumi na sita alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu kwa miaka hamsini na mbili. Mama yake aliitwa Yekolia, kutoka Yerusalemu.

4Akatenda yaliyo mema machoni pa Bwana , vile Amazia baba yake alivyofanya.

5Akamtafuta Mungu katika siku za Zekaria, aliyemwelekeza kumcha Mungu. Wakati wote alipomtafuta Bwana , Mungu alimfanikisha.

6Alipigana vita dhidi ya Wafilisti na kubomoa kuta za Gathi, Yabne na Ashdodi. Kisha akajenga upya miji karibu na Ashdodi, na mahali pengine katikati ya Wafilisti.

7Mungu akamsaidia dhidi ya Wafilisti na dhidi ya Waarabu walioishi Gur-Baali na dhidi ya Wameuni.

8Waamoni wakamletea Uzia ushuru, na umaarufu wake ukaenea hadi mpaka wa Misri, kwa sababu alikuwa na nguvu sana.

9Uzia akajenga minara huko Yerusalemu katika Lango la Pembeni, katika Lango la Bondeni na katika pembe, mahali kuta zikutanapo, kisha akaijengea ngome.

10Akajenga pia minara jangwani na kuchimba visima vingi vya maji, kwa sababu alikuwa na mifugo mingi chini ya vilima na katika nchi tambarare. Alikuwa na watu waliofanya kazi katika mashamba yake, na kwenye mashamba yake ya mizabibu huko vilimani na katika ardhi zenye rutuba, kwa kuwa aliupenda udongo.

11Zaidi ya hayo, Uzia alikuwa na jeshi lililofunzwa vizuri, lililokuwa tayari kwenda vitani kwa vikosi kufuatana na idadi yao kama walivyokusanywa na Yeieli mwandishi na Maaseya msimamizi chini ya maelekezo ya Hanania, mmoja wa maafisa wa mfalme.

12Idadi yote ya viongozi wa jamaa waliowaongoza wapiganaji walikuwa elfu mbili na mia sita.

13Chini ya uongozi wao kulikuwa na jeshi la watu elfu mia tatu na saba na mia tano waliofundishwa kwa ajili ya vita, jeshi lenye nguvu la kumsaidia mfalme dhidi ya adui zake.

14Uzia akalipatia jeshi lote ngao, mikuki, chapeo, dirii, pinde na mawe ya kombeo.

15Huko Yerusalemu watu wenye utaalamu mkubwa wakatengeneza mitambo iliyotumika katika minara na kwenye pembe za ulinzi ili kurusha mishale na kuvurumisha mawe makubwa. Sifa zake zikaenea mbali sana kwa sababu alisaidiwa mno hadi akawa na nguvu sana.

16Lakini baada ya Uzia kuwa na nguvu sana, majivuno yake yakamsababishia kuanguka. Alikosa uaminifu kwa Bwana Mungu wake, naye akaingia hekaluni mwa Bwana ili afukize uvumba kwenye madhabahu ya kufukizia uvumba.

17Azaria kuhani akiwa pamoja na makuhani wengine themanini wa Bwana wenye ujasiri wakamfuata ndani.

18Wakamkabili na kumwambia, “Siyo sawa kwako, Uzia, kumfukizia Bwana uvumba. Hiyo ni kazi ya makuhani, wazao wa Haruni, ambao wamewekwa wakfu ili kufukiza uvumba. Ondoka mahali patakatifu, kwa kuwa umekosa uaminifu nawe hutaheshimiwa na Bwana Mungu.”

19Uzia, aliyekuwa na chetezo mkononi mwake tayari kufukiza uvumba, akakasirika. Alipokuwa anawaghadhibikia makuhani mbele ya madhabahu ya kufukizia uvumba katika Hekalu la Bwana , ukoma ukamtokea kwenye paji la uso wake.

20Azaria kuhani mkuu pamoja na makuhani wengine wote walipomtazama wakaona kwamba alikuwa na ukoma pajini lake, wakaharakisha kumtoa nje. Naam, hata yeye mwenyewe alitamani kuondoka kwa sababu Bwana alikuwa amempiga.

21Mfalme Uzia alikuwa na ukoma hadi siku ya kufa kwake. Akatengwa katika nyumba ya pekee akiwa mwenye ukoma, naye akawa ametengwa kutoka Hekalu la Bwana . Yothamu mwanawe akawa msimamizi wa jumba la mfalme, pia akawaongoza watu wa nchi.

22Matukio mengine ya utawala wa Uzia, kuanzia mwanzo hadi mwisho, yameandikwa na nabii Isaya mwana wa Amozi.

23Uzia akalala na baba zake, akazikwa karibu nao katika shamba la kuzikia lililokuwa mali ya wafalme, kwa kuwa watu walisema, “Alikuwa na ukoma.” Yothamu mwanawe akawa mfalme baada yake.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.