2 Nyakati 4

2 Nyakati 4

Vifaa vya Hekalu

(1Fal 7:23‑51)

1Mfalme Sulemani akatengeneza madhabahu ya shaba yenye urefu wa dhiraa ishirini, upana wa dhiraa ishirini na kimo chake dhiraa kumi.[#4:1 Dhiraa 20 ni sawa na mita 9.; #4:1 Dhiraa 10 ni sawa na mita 4.5.]

2Akatengeneza Bahari ya kusubu, yenye umbo la mviringo, ya dhiraa kumi kutoka ukingo hadi ukingo na kimo cha dhiraa tano. Kamba ya urefu wa dhiraa thelathini ingeweza kuizunguka.[#4:2 Dhiraa 30 ni sawa na mita 13.5.]

3Chini ya huo ukingo, kulikuwa na mafahali kuizunguka, yaani mafahali kumi katika kila dhiraa moja. Hayo mafahali waliyasubu katika safu mbili yakiwa ya kitu kimoja na hiyo Bahari.[#4:3 Dhiraa moja ni sawa na sentimita 45.]

4Bahari hiyo ilikaa juu ya mafahali kumi na wawili, mafahali watatu walielekeza nyuso zao kaskazini, watatu magharibi, watatu kusini, na watatu mashariki. Bahari hiyo ilikaa juu ya hao mafahali, nazo sehemu zao za nyuma zilielekeana.

5Unene wake ulikuwa nyanda moja, na ukingo wake ulifanana na ukingo wa kikombe, kama ua la yungiyungi iliyochanua. Ingejazwa na bathi elfu tatu.[#4:5 nyanda moja ni sawa na sentimita 7.5; #4:5 Bathi 3,000 ni sawa na lita 60,000.]

6Kisha akatengeneza masinia kumi kwa ajili ya kuoshea vifaa, naye akayaweka matano upande wa kusini na matano upande wa kaskazini. Ndani yake ndimo walioshea vifaa vya kutumika katika sadaka za kuteketezwa, lakini ile Bahari ilikuwa ya makuhani kunawia.

7Akatengeneza vinara kumi vya taa vya dhahabu kama ilivyoainishwa na kuviweka hekaluni, vinara vitano upande wa kusini, na vitano upande wa kaskazini.

8Akatengeneza meza kumi na kuziweka hekaluni, tano upande wa kusini na tano upande wa kaskazini. Pia akatengeneza mabakuli mia moja ya dhahabu ya kunyunyizia.

9Akatengeneza ukumbi wa makuhani, na ukumbi mwingine mkubwa na milango yake, naye akaifunika hiyo milango kwa shaba.

10Akaiweka ile Bahari upande wa kusini, kwenye pembe ya kusini-mashariki mwa nyumba.

11Huramu pia akatengeneza masufuria, masepetu na mabakuli ya kunyunyizia.

Kwa hiyo Huramu akakamilisha kazi katika Hekalu la Mungu kama vile Mfalme Sulemani alikuwa amemwagiza:

12zile nguzo mbili;

yale mataji mawili yaliyokuwa juu ya hizo nguzo,

zile nyavu mbili za kupamba hayo mataji mawili yenye umbo la bakuli yaliyowekwa juu ya zile nguzo;

13yale makomamanga mia nne kwa ajili ya hizo nyavu mbili (safu mbili za makomamanga kwa kila wavu yakipamba hayo mataji mawili yenye umbo la bakuli juu ya hizo nguzo);

14vishikio pamoja na masinia yake;

15hiyo Bahari na hao mafahali kumi na wawili chini yake;

16pia hayo masufuria, masepetu, uma za nyama na vyombo vingine vyote vilivyohusiana.

Vitu vyote ambavyo Huram-Abi alimtengenezea Mfalme Sulemani kwa ajili ya Hekalu la Bwana vilikuwa vya shaba iliyosuguliwa.

17Mfalme aliagiza wavisubu vitu hivi kwenye kalibu za udongo wa mfinyanzi katika uwanda wa Yordani kati ya Sukothi na Sereda.[#4:17 au Sarethani.]

18Vitu hivi vyote Mfalme Sulemani alivyotengeneza vilikuwa vingi sana hivi kwamba uzani wa shaba haungekadirika.

19Sulemani pia akatengeneza samani zote zilizokuwa ndani ya Hekalu la Mungu:

madhabahu ya dhahabu;

meza za kuweka mikate ya Wonesho;

20vinara vya taa vya dhahabu safi pamoja na taa zake ili ziwake mbele ya mahali patakatifu kama ilivyoelekezwa;

21maua ya dhahabu yaliyofanyizwa, taa na makoleo (vilikuwa vya dhahabu bora kabisa);

22mikasi ya dhahabu safi, mabakuli ya kunyunyizia, masinia na vyetezo; milango ya dhahabu ya Hekalu: yaani milango ya ndani ya Patakatifu pa Patakatifu, na milango ya ukumbi mkuu.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.