2 Nyakati 5

2 Nyakati 5

1Hivyo Sulemani alipomaliza kazi ya Hekalu la Bwana , akaviingiza ndani vile vitu ambavyo Daudi baba yake alikuwa ameviweka wakfu: yaani fedha, dhahabu na samani; kisha akaviweka katika hazina za Hekalu la Mungu.

Sanduku la Agano laletwa Hekaluni

(1Fal 8:1‑9)

2Kisha Sulemani akawaita huko Yerusalemu wazee wa Israeli, viongozi wote wa makabila, na wakuu wa jamaa za Waisraeli, ili walilete Sanduku la Agano la Bwana kutoka Sayuni, Mji wa Daudi.

3Nao wanaume wote wa Israeli wakakusanyika kwa mfalme wakati wa sikukuu ya mwezi wa saba.

4Wazee wote wa Israeli walipofika, Walawi wakajitwika Sanduku la Agano,

5nao wakalipandisha Sanduku na Hema la Kukutania pamoja na vyombo vyote vitakatifu vilivyokuwa ndani yake. Makuhani, waliokuwa Walawi, walivibeba vitu hivyo,

6naye Mfalme Sulemani na kusanyiko lote la Israeli waliokuwa wamemzunguka wakasimama mbele ya hilo Sanduku, nao wakatoa dhabihu za kondoo na ngʼombe nyingi kiasi kwamba idadi yao haikuweza kuandikwa au kuhesabika.

7Makuhani wakalileta Sanduku la Agano la Bwana hadi mahali patakatifu ndani ya Hekalu, pale Patakatifu pa Patakatifu, na kuliweka chini ya mabawa ya makerubi.

8Makerubi yalitandaza mabawa yao juu ya mahali pa Sanduku la Agano na kufunika Sanduku na mipiko yake ya kubebea.

9Mipiko hiyo ilikuwa mirefu sana kiasi kwamba ncha zake zilizojitokeza kutoka Sanduku, nazo zilionekana ukiwa mbele ya Patakatifu pa Patakatifu, lakini sio nje ya Mahali Patakatifu. Hiyo mipiko ipo hata leo.

10Ndani ya Sanduku hapakuwa na kitu kingine chochote isipokuwa vile vibao viwili ambavyo Musa aliviweka ndani yake huko Horebu, mahali Bwana alipofanya agano na Waisraeli baada ya kutoka Misri.

11Basi makuhani wakaondoka hapo Mahali Patakatifu. Makuhani wote waliokuwa huko walikuwa wamejiweka wakfu, bila kujali migawanyo yao.

12Walawi wote waliokuwa waimbaji, yaani Asafu, Hemani, Yeduthuni, wana wa ndugu zao, walisimama upande wa mashariki wa madhabahu, wakiwa wamevaa kitani safi huku wakipiga matoazi, vinubi na zeze. Walikuwa pamoja na makuhani mia moja na ishirini wakipiga tarumbeta.

13Wapiga tarumbeta na waimbaji wakaungana katika sauti linganifu, ikawa kama vile ni sauti moja, wakimsifu na kumshukuru Bwana . Nao wakapaza sauti zao, pamoja na tarumbeta na matoazi na vyombo vingine vya uimbaji, wakamsifu Bwana , wakisema:

“Yeye ni mwema;

fadhili zake zadumu milele.”

Ndipo Hekalu la Bwana likajazwa na wingu,

14nao makuhani hawakuweza kufanya huduma yao kwa sababu ya lile wingu, kwa kuwa utukufu wa Bwana ulijaza Hekalu la Mungu.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.