2 Nyakati 8

2 Nyakati 8

Shughuli nyingine za Sulemani

(1Fal 9:10‑28)

1Miaka ishirini ilipopita, ambayo katika hiyo Sulemani alilijenga Hekalu la Bwana na jumba lake mwenyewe la kifalme,

2Sulemani akajenga tena vijiji vile ambavyo Hiramu alikuwa amempa, naye akawapa Waisraeli waishi humo.

3Kisha Sulemani akaenda Hamath-Soba na kuuteka.

4Pia akajenga mji wa Tadmori katika jangwa, na miji yote ya kuhifadhia vitu katika Hamathi.

5Akajenga tena Beth-Horoni ya Juu na Beth-Horoni ya Chini, miji yenye ngome, kuta, malango na makomeo.

6Sulemani pia akajenga Baalathi na miji yake yote ya kuhifadhia vitu, na miji kwa ajili ya magari yake ya vita na kwa ajili ya farasi wake, chochote alichotaka kujenga katika Yerusalemu, katika Lebanoni na katika nchi yote aliyotawala.

7Watu wote waliosalia kutoka kwa Wahiti, Waamori, Waperizi, Wahivi na Wayebusi (haya mataifa hayakuwa Waisraeli),

8yaani wazao wao waliobakia katika nchi, ambao Waisraeli hawakuwa wamewaangamiza: hawa Sulemani akawalazimisha kuwa watumwa katika shokoa, kama ilivyo hadi leo.

9Lakini Sulemani hakuwafanya Waisraeli watumwa kwa ajili ya kazi yake; hao ndio walikuwa wapiganaji wake, majemadari wake, maafisa wake, majemadari wa magari yake ya vita, na wapanda farasi wake.

10Pia walikuwa maafisa wakuu wa Mfalme Sulemani, maafisa wakaguzi mia mbili na hamsini waliosimamia watu.

11Sulemani akampandisha mke wake binti Farao kutoka Mji wa Daudi na kumleta jumba la kifalme alilokuwa amemjengea, kwa kuwa alisema, “Mke wangu hataishi katika jumba la kifalme la Daudi mfalme wa Israeli, kwa sababu mahali ambapo Sanduku la Bwana limefika ni patakatifu.”

12Mfalme Sulemani akamtolea Bwana dhabihu za kuteketezwa juu ya madhabahu ya Bwana ambayo alikuwa ameijenga mbele ya ukumbi,

13kulingana na mahitaji ya kila siku kwa ajili ya sadaka zilizoamriwa na Musa kwa ajili ya Sabato, Mwezi Mwandamo na sikukuu nyingine tatu za mwaka: Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, Sikukuu ya Majuma na Sikukuu ya Vibanda.

14Kwa kushika maagizo ya Daudi baba yake, aliweka migawanyo ya makuhani kwa ajili ya kazi zao, nao Walawi kuongoza kusifu na kusaidia makuhani kufuatana na mahitaji ya kila siku. Pia akaweka mabawabu katika migawanyo kwa ajili ya malango mbalimbali, kwa sababu hivi ndivyo Daudi mtu wa Mungu alivyokuwa ameagiza.

15Nao hawakuziacha amri za mfalme alizoamuru makuhani au Walawi katika jambo lolote, ikiwa ni pamoja na zile za hazina.

16Kazi yote ya Mfalme Sulemani ilifanyika kuanzia siku msingi wa Hekalu la Bwana ulipowekwa hadi kukamilika kwake. Kwa hiyo Hekalu la Bwana likamalizika kujengwa.

17Ndipo Sulemani akaenda Esion-Geberi na Elathi katika pwani ya Edomu.

18Naye Hiramu alimpelekea meli zilizoongozwa na maafisa wake mwenyewe, watu waliokuwa na ujuzi wa baharini. Hawa watu pamoja na wale wa Sulemani wakasafiri kwa bahari hadi Ofiri, wakaleta kutoka huko talanta mia nne na hamsini za dhahabu, ambazo walimkabidhi Mfalme Sulemani.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.