The chat will start when you send the first message.
1Malkia wa Sheba aliposikia habari za umaarufu wa Sulemani, akaja Yerusalemu kumjaribu kwa maswali magumu. Alifika akiwa na msafara mkubwa sana, wenye ngamia waliobeba vikolezo, dhahabu nyingi, na vito vya thamani. Alikuja kwa Sulemani na kuzungumza naye mambo yote aliyokuwa nayo moyoni mwake.
2Sulemani alimjibu maswali yake yote, wala hakukuwa na jambo lolote lililokuwa gumu kwake hata asiweze kumwelezea.
3Malkia wa Sheba alipoona hekima yote ya Sulemani, na jumba la kifalme alilokuwa amejenga,
4chakula kilichokuwa mezani pake, jinsi maafisa wake walivyokaa, wahudumu katika majoho yao, wanyweshaji wake na sadaka za kuteketezwa alizotoa katika Hekalu la Bwana , alipatwa na mshangao mkubwa.
5Akamwambia mfalme, “Taarifa niliyosikia kwenye nchi yangu mwenyewe kuhusu mafanikio na hekima yako ni kweli.
6Lakini sikuamini mambo yaliyosemwa hadi nilipokuja na kuona kwa macho yangu mwenyewe. Naam, sikuambiwa hata nusu yake; katika hekima na mali umezidi sana kuliko ile taarifa niliyoisikia.
7Heri watu wako! Heri hawa maafisa wako wanaosimama mbele yako daima na kusikia hekima yako!
8Ahimidiwe Bwana Mungu wako, ambaye amependezwa sana nawe, na akakuweka kwenye kiti chake cha ufalme utawale kwa niaba ya Bwana Mungu wako. Kwa sababu ya upendo wa Mungu wako kwa Israeli na shauku yake ya kuwathibitisha milele, amekufanya wewe mfalme juu yao, ili kudumisha haki na uadilifu.”
9Naye akampa mfalme talanta mia moja na ishirini za dhahabu, kiasi kikubwa cha vikolezo na vito vya thamani. Haikuwahi kamwe kuletwa vikolezo vizuri kama vile malkia wa Sheba alivyompa Mfalme Sulemani.[#9:9 Talanta 120 za dhahabu ni sawa na tani 4.5.]
10(Watumishi wa Hiramu na wa Sulemani wakaleta dhahabu kutoka Ofiri, tena wakaleta shehena kubwa ya miti ya msandali na vito vya thamani.
11Mfalme akatumia hiyo miti ya msandali kuwa ngazi kwa ajili ya Hekalu la Bwana na kwa jumba la kifalme, pia kwa kutengeneza vinubi na zeze kwa ajili ya waimbaji. Kiasi hicho kingi cha msandali hakijawahi kuingizwa Yuda tangu siku ile.)
12Mfalme Sulemani akampa malkia wa Sheba kila kitu alichotamani na kukiomba, zaidi ya vile alivyokuwa amemletea mfalme. Kisha malkia akaondoka na kurudi katika nchi yake, yeye na watumishi wake.
13Uzito wa dhahabu ambayo Sulemani alipokea kwa mwaka ulikuwa talanta mia sita sitini na sita (666),[#9:13 Talanta 666 za dhahabu ni sawa na tani 25.]
14mbali na mapato yaliyoletwa na wafanyabiashara na wachuuzi. Wafalme wote wa Arabuni na watawala wa nchi wakamletea Sulemani dhahabu na fedha.
15Mfalme Sulemani akatengeneza ngao kubwa mia mbili kwa dhahabu iliyofuliwa. Kila ngao ilikuwa na dhahabu yenye uzito wa shekeli mia sita.[#9:15 Shekeli 600 za dhahabu ni sawa na kilo 3.5.]
16Akatengeneza pia ngao ndogo mia tatu za dhahabu iliyofuliwa, kila ngao ikiwa na uzito wa mane tatu za dhahabu. Mfalme akaziweka katika Jumba la Kifalme la Msitu wa Lebanoni.[#9:16 Mane tatu za dhahabu ni sawa na kilo 1.7.]
17Kisha mfalme akatengeneza kiti kikubwa cha kifalme kwa kutumia pembe za ndovu na kukifunika kwa dhahabu safi.
18Kiti hicho kilikuwa na ngazi sita na mahali pa kuwekea miguu vyote vya dhahabu. Kila upande wa kiti ulikuwa na mahali pa kuegemeza mkono, na simba aliyesimama kando kila upande.
19Simba kumi na wawili walisimama kwenye ngazi sita, mmoja katika kila upande wa kila ngazi. Hakuna kitu kama hicho kilichokuwa kimefanyika kwenye ufalme mwingine wowote.
20Vikombe vyote vya Mfalme Sulemani vya kunywea vilikuwa vya dhahabu na vyombo vyote vya nyumbani katika Jumba la Kifalme la Msitu wa Lebanoni vilikuwa vya dhahabu safi. Hakukuwa na kitu kilichotengenezwa kwa fedha, kwa sababu fedha ilionekana ya thamani ndogo wakati wa Sulemani.
21Mfalme alikuwa na meli nyingi za biashara baharini zilizoendeshwa na watu wa Hiramu. Kwa mara moja kila miaka mitatu zilirudi, zikiwa zimebeba dhahabu, fedha, pembe za ndovu na nyani wakubwa na wadogo.[#9:21 au: za Tarshishi (taz. 1Fal 10:22; 22:48; 2Nya 20:36; Isa 2:16; 60:9).]
22Mfalme Sulemani alikuwa mkuu zaidi kwa utajiri na hekima kuliko wafalme wote wa dunia.
23Wafalme wote wa dunia wakatafuta kukutana na Sulemani ili kusikia hekima ambayo Mungu alikuwa ameiweka katika moyo wake.
24Mwaka baada ya mwaka, kila mmoja ambaye alikuja, alileta zawadi, vyombo vya fedha na dhahabu, majoho, silaha na vikolezo, farasi na nyumbu.
25Sulemani alikuwa na mabanda elfu nne kwa ajili ya farasi na magari ya vita, na farasi elfu kumi na mbili ambao aliwaweka katika miji ya magari ya vita, na wengine akawa nao huko Yerusalemu.
26Sulemani akatawala juu ya wafalme wote kuanzia Mto hadi kwenye nchi ya Wafilisti na kuendelea hadi mpaka wa Misri.[#9:26 yaani Mto Frati.]
27Mfalme akafanya fedha kuwa kitu cha kawaida kama mawe huko Yerusalemu, mierezi akaifanya kuwa mingi kama mikuyu chini ya vilima.
28Farasi wa Sulemani waliletwa kutoka Misri na kutoka nchi nyingine zote.
29Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Sulemani, kuanzia mwanzo hadi mwisho, je, hayakuandikwa katika kumbukumbu za nabii Nathani, katika unabii wa Ahiya Mshiloni na katika maono ya Ido mwonaji kuhusu Yeroboamu mwana wa Nebati?
30Sulemani alitawala Israeli yote miaka arobaini akiwa Yerusalemu.
31Kisha Sulemani akalala na baba zake, naye akazikwa katika mji wa Daudi, baba yake. Naye Rehoboamu mwanawe akawa mfalme baada yake.